Kitu ambacho binadamu wote tunaweza kuwa sawa kwenye maisha ni kwamba kila binadamu anapenda furaha. Hakuna mtu ambae lengo lake kuu kwenye maisha ni kuwa na kisirani ama mabalaa kila siku.

  Kila mtu anapenda kufurahia maisha na kuishi kwa raha mustarehe. Na kufurahia maisha ndiko kunatufanya tufanye kazi kwa bidii na maarifa. Kufurahia maisha ndiko kunatufanya tuwe wabunifu wa kugundua njia mbalimbali za kurahisisha maisha.

furaha3

  Kutokana na furaha kuwa lengo la msingi la kila binadamu, kuna njia mbalimbali za kutufanya tuyafurahie maisha. Njia hizi zipo ambazo zinatuletea furaha ya muda mfupi na kuna ambazo zinatuletea furaha ya muda mrefu ama ya kudumu.

  Tatizo kubwa tunalokutana nalo kwenye maisha yetu ya kila siku ni kwamba watu wengi tunashindwa kutofautisha furaha ya muda mfupi(starehe) na furaha ya muda mrefu.

  Kwa kushindwa kutofautisha starehe na furaha wengi wetu tumejikuta tukizama kwenye starehe na mwishowe kukosa kabisa furaha. Kwa kuwa watu tunapenda sana furaha ni rahisi sana kutumbukia kwenye starehe na kudhani ndio furaha kwenye maisha.

  Kama utaendekeza furaha za muda mfupi(starehe) itakuwa ni kikwazo kwako kupata furaha ya kweli kwenye maisha.

  Kuna baadhi ya vitu ambavyo huwa tunavipenda kwa kuwa vinatupatia starehe ya muda mfupi bila kuangalia madhara yake kwenye furaha ya kweli kwenye maisha.

  Moja ya vitu hivyo ni utumiaji wa vileo. Hapa namaanisha vileo vya aina zote, unywaji, uvutaji na hata utumiaji wa dawa za kulevya. Ukiangalia chanzo cha wengi kuanza kutumia vileo ni kutafuta furaha ama kukimbia matatizo. Ni kweli mtu anapokuwa na ulevi anasahau matatizo yake na anakuwa katika hali ya furaha, lakini nini kinatokea ulevi unapoisha?

  Baada ya ulevi kuisha matatizo bado yako palepale, baadae mtu anamua kuongeza kiwango cha ulevi ili kuongeza furaha zaidi. Mwisho wa siku maisha ya mtu yanaharibika kutokana na ulevi wa kupindukia au kuwa mteja wa madawa ya kulevya. Yote haya yalianza taratibu kama njia ya kutafuta furaha.

  Kitu kingine ambacho watu tunapenda kufanya ili kupata furaha ya muda mfupi ni mapenzi. Ni kweli kufanya mapenzi kunaleta furaha, ila inakaa kwa muda gani? Furaha hii ya muda mfupi inayotokana na kufanya mapenzi imewafanya baadhi ya watu kuendekeza mapenzi kupita kiasi. Mwisho wa siku ni kutumia gharama nyingi na kuishia kupata magonjwa yanayodhuru afya zetu na bado hatupati furaha ya kudumu.

  Ufanye nini ili upate furaha ya kudumu kwenye maisha?

Kuwa na malengo na maisha yako.

Kuwa dereva na kiongozi mkuu wa maisha yako.

Jua kwa nini upo hapa duniani na ukiondoka utaacha nini.

Wapende wale wanaokupenda, onesha upendo wa kweli kwa watu wako wa karibu.

Kama kuna tatizo litafutie suluhisho na sio kulikwepa.

Furahia kile unachofanya na ufanye kwa juhudi na maarifa.

Bobea kwenye kile unachofanya, fanya kwa utofauti na ubunifu mkubwa.

Wasaidie watu na badili maisha ya watu kupitia kile unachofanya.

Usiweke fedha mbele kwenye kile unachofanya, kuweka fedha kama lengo lako kuu hutopata furaha ya kweli.

  Kwa kufanya hayo na mengine mengi utajikuta unaishi maisha unayofurahia kila siku, hata unapokutana na vikwazo haviwezi kukukatisha tamaa kwa sababu unajua hicho ni kitu kidogo sana kwenye maisha yako.

  Furaha ni haki yako ya kuzaliwa ambayo huwezi kunyanganywa na mtu mwingine yeyote. Jua jinsi ya kuishi maisha yako ili uwe na furaha kila siku.