Jiji la Dar es salaam linasifika kwa kuwa na foleni ndefu sana za magari. Ni kitu ambacho kimekuwepo kwa muda mrefu na kinaonekana kuendelea kuwepo kwa muda mrefu ujao.
Siku za hivi karibuni foleni imeongezeka sana na kuwa maradufu. Kwa mfano safari ya kutoka ubungo mpaka posta inaweza kuchukua masaa mawili mpaka matatu. Safari ambayo kwa hali ya kawaida ingetakiwa kuchukua nusu saa.
Foleni hizi pia huwa ndefu sana nyakati za asubuhi ambapo watu wengi wanakwenda kwenye shughuli zao na nyakati za jioni ambapo watu wengi wanarudi majumbani.
Tunapokuwa kwenye foleni hizi hasa tunapokuwa kwenye usafiri wa jumuia(daladala) kila mtu anakuwa analalamika ni jinsi gani serikali inavyoshindwa kupunguza tatizo hili la foleni. Wakati mwingine huibuka mabishano mbalimbali ya kisiasa ama mambo mengine na baadhi ya abiria huonekana kuwa na uchungu sana ama kukerwa sana na hali ya mambo. Baada ya safari kila mtu anaenda na mambo yake na hakuna chochote kinachobadilika kutokana na lawama hizo ama malalamiko hayo.
Nilichojifunza kutokana na foleni hizi ni kwamba popote ninapotaka kwenda kwa usafiri itanichukua sio chini ya saa moja kutokana na foleni. Na pia hata ulalamike kiasi gani bado utaendelea kuwepo kwenye foleni na utazidi kujipa hasira.
Hivyo nilichukua hatua ya kutumia foleni kwa manufaa. Kwa kuwa nina uhakika wa kupoteza masaa matatu kila siku kwenye usafiri tu niliamua kutopoteza muda huo bure kabisa. Niliamua kutumia muda huo kwa kujifunza.
Nilichogundua ni kwamba kwa masaa matatu kwa siku ninaweza kujifunza vitu vingi sana.
Muda ninaokuwa kwenye foleni nimekuwa nikisoma vitabu kwa kutumia simu na mara nyingi nimekuwa nikisikiliza vitabu vilivyosomwa (audio books).
Badala ya kukaa na kulalamikia ubaya wa foleni ama kubishana vitu ambavyo siwezi kuviathiri nimetumia muda huu kujifunza. Kwa masaa matatu kwa siku nimekuwa najifunza vitu vingi mno ambavyo vimesaidia kubadili maisha yangu kwa kiasi kikubwa.
Kila siku nina uhakika wa kusikiliza kitabu kimoja na kunifanya niwe na mtizamo tofauti na kufikiri zaidi. Hata kama nimesimama kwenye daladala bado naweza kujifunza mengi kwa kusikiliza vitabu mbalimbali.
Nafasi hii ya kujifunza imenifanya niipende sana foleni. Nimeamua kutumia mazingira mabovu kwa manufaa(best use of bad situation)
Kama na wewe unapoteza muda mwingi kwenye foleni unaweza kutumia muda huo kujifunza. Hata kama unatumia usafiri wako mwenyewe ama usafiri wa daladala bado una nafasi kubwa ya kujifunza kwa kusikiliza vitabu vilivyosomwa(audio books)
Natoa memory card yenye vitabu 25 ambayo unaweza kusikiliza kwenye simu au hata redio ya gari. Kujua vitabu vilivyopo kwenye memory card hiyo na jinsi yakuipata bonyeza maandishi haya.
Pia kama simu yako ina uwezo wa kusoma vitabu(pdf) jiunge na mtandao huu na utatumiwa vitabu mbalimbali vya kujisomea. Kujiunga na mtandao huu bonyeza maandishi haya.
Tumia muda unaopoteza kwenye foleni kwa manufaa kwako. Tafuta njia yoyote unayoweza kujifunza unapokuwa kwenye foleni.