Msimu wa sikukuu umekwisha na sasa ni mwezi wa kwanza ambapo hali ya watu wengi sio nzuri hasa kifedha. Watu wengi walifanya matumizi makubwa sana na ya hovyo wakati wa msimu wa sikukuu. Matumizi hayo makubwa yamewaacha katika hali mbaya ya kutokuwa na fedha huku majukumu yakiwa mengi hasa wakati huu wa mwanzo wa mwaka.
  Naona watu wengi mtaani huku wakihaha kutokana na kukosa fedha kwenye mwezi huu. Na mwezi huu ndio wenye majukumu makubwa kwa kuwa watoto wanatakiwa kwenda shule hivyo ada na fedha nyingine za mahitaji zinatakiwa haraka. Kuna wengine wanatakiwa kulipa kodi za nyumba ama ofisi. Kuna wengine wanatakiwa kulipa madeni mbalimbali wanayodaiwa na kadhalika. Mambo yote haya yanafanya watu wengi wawe kwenye hali mbaya sana. Wengine wanafikia hatua ya kupaniki na kuchukua mikopo zaidi ama kuuza baadhi ya vitu wanavyomiliki.
                stress2
  Pamoja na kuandika
mambo matano muhimu ya kufanya msimu huu wa sikukuu huenda hukupata nafasi ya kusoma au ulisoma ila ukashindwa kufuata ushauri ule. Sasa msimu wa sikukuu umekwisha na umebaki ‘mweupe’ yaani huna fedha na una majukumu makubwa yako mbele yako. Umeshafikiri sana ila bado hupati jibu na unazidi kuumia kwa msongo wa mawazo uliotokana na matumizi yako ambayo hayakuwa ya busara. Kabla na wewe hujapaniki na kujiingiza kwenye madeni ama kuuza vitu unavyomiliki ni vyema ukafanya mambo haya matatu ili usiendelee kuwa kwenye hali hiyo mbaya.
1. Kubali kwamba ulikosea kwa kufanya matumizi bila ya kufikiri kwa kina.
  Ni vigumu sana kukubali kwamba ulikosea katika matumizi yako ya fedha wakati wa sikukuu. Na kutokubali huko kutakufanya urudie makosa hayo kila mwaka na uendelee kuumia kila mwaka. Kubali ulikosea, ndio ulikosea sana. Hivi wakati unafanya anasa wakati wa sikukuu ulikuwa na mpango gani wakati mgumu kama huu? Ulifikiri ndio mwisho wa dunia? Ulikosea sana kutokuwa na mpango na ndio maana sasa hivi unateseka. Kubali kwamba ulikosea na amua kutorudia tena makosa uliyoyafanya kwenye sikukuu zijazo.
2. Anza kujilipa wewe kwanza.
 Huenda ulikuwa hujajua umuhimu wa kuanza kujilipa wewe kwanza katika kipato chochote unachotengeneza. Ndio maana uliweza kutumia akiba yako hovyo kwenye msimu wa sikukuu. Ni muhimu sana kuanza kujilipa wewe binafsi na kutotumia fedha hizo katika matumizi yoyote. Kujua zaidi juu ya kujilipa wewe kwanza soma; unawalipa watu wote kasoro huyu mmoja wa muhimu.
3. Kuwa makini kwenye njia unazotumia kupata fedha za haraka. 
  Kwa kuwa unahitaji kubwa la fedha na la haraka kutokana na majukumu yaliyoko mbele yako ni rahisi sana kuingia kwenye mtego wa kupata fedha isivyo halali au kupata hasara kwa kuingia kwenye mkopo mbaya au kuuza kitu chako cha thamani kwa bei ya kutupa. Kipindi hiki watu wengi wanauza vitu vya thamani kwa bei za kutupwa kutokana na uhitaji mkubwa wa fedha walioko nao. Pia wengine wanaingia kwenye madeni wanayojikuta wanalipa riba kubwa kutokana na kuhitaji fedha kwa haraka. Wengi pia wanajikuta wakitafuta fedha kwa njia zisizo halali kama kuiba, kuomba rushwa na kudhulumu wengine.
  Kuwa makini sana mahitaji yako ya fedha yasikuingize kwenye mitego hii ambayo itakufanya uishi maisha ambayo sio ya furaha. Kama utahitaji kuchukua mkopo hakikisha unaujua vizuri mkopo huo na una njia nzuri za kuulipa. Kama utahitaji kuuza baadhi ya vitu unavyomiliki basi uza vitu ambavyo sio muhimu sana kwako na unayemuuzia usimuoneshe kwamba una uhitaji mkubwa sana wa hela kwa sababu kufanya hivyo kutampa nafasi ya kukulangua.
  Tumia nyakati ngumu kama hizi kujifunza na usipoteze somo unalolipata. Usiumie sana bali panga kutorudia makosa makubwa uliyoyafanya.
  Pia hudhuria semina yetu itakayofanyika jumamosi tarehe 18/01/2014 ili ujifunze zaidi na uondokane na majuto uliyoko nayo. Kujua zaidi kuhusu semina hiyo bonyeza maandishi haya.