Leo ni siku ya mwisho ya mwezi wa kwanza kwa mwaka huu 2014. Ni juzi tu tulikuwa tukisherekea mwaka mpya ila sasa mwaka ni kama umeshazeeka. Mwaka huu uliufanya wa kipekee kwako na kuamua uwe mwaka wa mabadiliko kwenye maisha yako.
Mpaka kufikia leo zimeshapita siku 30, je umefanya nini ndani ya siku hizo 30? Je umefikia wapi kwenye malengo uliyojiwekea mwaka huu na mwezi huu?
Hebu tenga muda leo na ukae upitie malengo yako uliyoandika na kisha uanze kufanya tathmini. Yapitie malengo yako huku ukijiuliza maswali hayo ya msingi ili ujue upo kwenye uelekeo gani.
Tafiti zinaonesha kwamba asilimia kubwa ya watu wanaoweka malengo huwa wanayasahau kabisa wiki sita baada ya kuyaweka. Pia inasemekana asilimia kubwa ya watu wanaoweka malengo ya kutofanya vitu flani huanza kuyavunja siku inayofuata. Tafiti zimekwenda mbali zaidi na kugundua asilimia kubwa ya watu wanaoweka malengo ya kupunguza uzito huwa unapungua kidogo ila baadae huongezeka zaidi ya waliokuwa nao mwanzo.
Matokeo hayo ya tafiti mbalimbali yanaonesha kuna tatizo kubwa kwenye uwekaji na utekelezaje wa malengo. Tulishazungumzia hapa jinsi ya kuweka malengo makubwa utakayoyafikia na makosa makubwa unayofanya wakati wa kuweka malengo yako. Pamoja na kusoma yote hayo bado unarudia makosa yale yale kwenye kuweka na kutekeleza malengo yako.
Pia inawezekana mpaka sasa bado hujaona umuhimu wa kuweka malengo. Pamoja na kusoma hii ndio hasara kubwa unayoipata kwa kutoweka malengo bado umeamua kuwa mbishi na kuendelea na maisha ambayo hayana malengo.
Leo nakukumbusha kupitia malengo yako na uone kama uko kwenye njia sahihi ya kuyafikia au la. Kama bado hujaweka malengo au umeweka malengo ila inakuwa shida kwako kuyafikia tafadhali bonyeza hapa na usome makala mbalimbali zinazohusiana na malengo.
Kama ndani ya siku hizi 30 uliyasahau malengo yako, leo unapata nafasi ya kurudi kwenye mstari. Kama hukuanza kabisa basi usiumie sana bali anza sasa, anza kwa kuweka malengo leo na weka mipango na mikakati ya kuyafikia. Hakuna kuchelewa kwenye safari ya mafanikio bali kuna kujifunza.
Usiseme kwamba kwa kuwa ulishindwa kuweka malengo mwanzoni mwa mwaka basi inabidi usubiri mpaka mwaka ujao. Unaweza kuweka malengo kwenye kipindi chochote cha maisha yako. Hivyo weka malengo leo na uanze kuyatekeleza. Muda unakwenda haraka sana hivyo usiupoteze kwa kufanya mambo ambayo hayana msaada kwenye maisha yako.
Na ili ujue mambo yenye msaada kwenye maisha yako na yasiyo na msaada kwenye maisha yako ni lazima uwe na malengo. Kama huna malengo chochote kitakachokuja mbele yako utakiparamia. Na kama uko tayari kuparamia chochote kinachokuja mbele yako basi maisha yako hayana thamani kubwa.
Bado unazo siku 334 za kufanya mambo makubwa sana kwenye mwaka huu 2014, usikate tamaa, songa mbele.