Kama Unafanya Hivi Hakuna Unayemkomoa, Unajikomoa Mwenyewe

  Siku moja nilikuwa nazungumza na rafiki yangu ambaye ni mwalimu wa sekondari wa shule ya serikali. Nilimuuliza kuhusu changamoto mbalimbali anazokutana nazo kwenye kazi yake na kwa kuwa bado ni mchanga kazini nilitaka kujua malengo yake kwenye kazi hiyo. Tulizungumza mengi sana ila kuna kitu kimoja aliniambia ambacho kilinifanya nifikiri zaidi. Kitu hiki kimekuwa kinafanywa na waajiriwa wengi hasa wa taasisi za umma.

  Mwalimu huyo aliniambia yeye hahangaiki akitaka anafundisha asipotaka anazuga tu, watoto wakifaulu au wakifeli yeye haimpunguzii chochote. Cha msingi ni yeye kuonekana yupo kazini na mwisho wa mwezi anapokea mshahara wake. Jambo hili halikunishtua sana kwa sababu watumishi wengi hasa kwenye sekta za umma ndio wana mtizamo huo. Kilichonifanya nifikiri zaidi ni kwamba tutakwenda hivi mpaka lini na tunapeleka wapi taifa kwa kuwa na watu wengi wenye mtizamo wa aina hii.

              penda kazi yako

  Katika kufikiri, pia nilijiuliza ni nani anayepoteza zaidi katika hali ile kati ya mwajiriwa na mwajiri. Nilichogundua ni kwamba mwajiriwa anaumia zaidi ya mwajiri.

  Kama na wewe umeajiriwa na hufanyi kazi kutoka moyoni kwako una shida kubwa. Kama unafanya tu kazi ili uonekane uko kazini usifikiri unamkomoa mwajiri wako, unajikomoa wewe mwenyewe. Katika vita ya aina hiyo ambayo umeianzisha wewe mwenyewe tayari umeshajipangia kushindwa.

 

 Kwa nini utashindwa kwenye vita hii?

 

  Utashindwa kwenye vita hii kwa sababu zifuatazo;

1. Utapata lawama nyingi kutoka kwa wanaohitaji huduma yako. Kazi inayohesabiwa ni wewe umeifanya. Kama kazi itakuwa nzuri kila mtu ataiona na kuisifia na kama itakuwa mbovu kuna watu wengi sana watakaoathirika na siku zote watakulaumu wewe. Kuwa na watu wengi wanaokulaumu itakufanya ujione huna thamani mbele ya watu.

2. Utakosa furaha kwenye kazi yako.  Kwa kufanya kazi bila ya kuwa na moyo utatoa majibu ambayo hata wewe mwenyewe huyafurahii. Kutokufurahishwa na majibu ya kazi yako ni chanzo moja wapo cha kukosa furaha kwenye maisha na kupata msongo wa mawazo. Kama hakuna kitu ambacho watu wanakisifia kutokana na kazi yako ni lazima utaona kazi yako ni kama kisirani kwako. Hii itakufanya uzidi kuichukia kazi na kila mara upate hasira kali kila unapofanya kazi.

3. Huwezi kufanikiwa. Kama tulivyowahi kuona kwenye makala zilizopita kama unataka kufanikiwa usifanye kazi. Ili ufanikiwe inabidi ufanye kitu unachokipenda, kwa kufanya hivyo utafanya kazi kwa moyo na kwa ubunifu. Hii itakusaidia kutoa majibu mazuri na pia kufanikiwa sana kupitia kazi yako.

4. Utakosa kitu cha kusimamia. Mwisho wa siku ambapo maisha yameshakwenda sana kuna kipindi utahitaji kuangalia nyuma na kuona kuna mchango gani ulioutoa kwenye jamii yako au kwa dunia kiujumla. Kama hutaona kazi ya maana uliyofanya na ambayo watu wengi iliwasaidia utakuwa katika hali mbaya sana. Utajiona kama maisha yako duniani hayakuwa na thamani yoyote.

5. Unaua vipaji vyako na unadidimiza uwezo wako. Wewe ni wa pekee na una uwezo mkubwa sana. Kama hutoipenda kazi yako huwezi kudugua uwezo mkubwa pamoja na ubunifu na vipaji vikubwa vilivyoko ndani yako. Hii itadidimiza uwezo wako na kuua vipaji vyako kwa sababu havitumiki. Dunia itakosa mchango mkubwa sana kutoka kwako.

  Pamoja na kwamba ajira zimekuwa ngumu na waajiri hawajali tena waajiriwa bado kushindana na mwajiri wako kwa kutumia utendaji kazi wako wewe ndiye utakayeshindwa. Kazi yoyote unayofanya ifanye kwa moyo mmoja na mapenzi makubwa. Kama unaona kazi hiyo haikuridhishi ni bora ukaiacha na kwenda kufanya kile kinachokuridhisha. Kuendelea kuing’ang’ania ni kuendelea kujimaliza.

 

Soma; DALILI 8 ZA KUTOFANIKIWA KWA KILE UNACHOFANYA.

5 thoughts on “Kama Unafanya Hivi Hakuna Unayemkomoa, Unajikomoa Mwenyewe

 1. Mlay Josephu January 29, 2014 / 9:53 am

  kwa kweli inaumiza kuona mtu anafanya kazi ya muhimu kwa jamii kama part time, huuma iwe nzuri isiwe nzuri yeye hajali hilo…hii imenikuta sana katika mashirika ya umma ambapo watoa hudumu wapo kama picha za matangazo pale darajani manzese hawana ujuzi wa kutoa huduma bora…wanarudisha nyuma maendeleo…

  Like

 2. Anonymous January 29, 2014 / 1:47 pm

  walimu wengi wanakubukwa kwa viboko na mimba walizowapa wanafunzi. Its Terrible.

  Like

 3. Anonymous January 29, 2014 / 1:50 pm

  Kweli Mkuu. Halafu hapohapo tunalalamika maisha magumu mishahara ipandishwe na hata ikipandishwa inaonekana haikidhi mahitaji. Tumesahau the law of sowing and reaping.

  Like

 4. Japhet Mutayoba March 14, 2014 / 6:15 am

  Ni kweli mkuu, ninachojua kazi yoyote ni wito….hadi unaamua kuisomea kazi fulani ina maana umeipenda kwa dhati. Ila tatizo siku hizi, watu hawana wito na kazi tena na kinachofanyika, tunaangalia wapi ni rahisi kupata ajira na mshahara wa haraka. Kwa mfano, siku hizi ualimu ajira zake nje nje….hivyo, hata kama wito wangu ni uanajeshi na bahati mbaya vigezo sina, inabidi niingie kwenye ualimu nile mshahara, maisha mbele kwa mbele…..nitafanya ualimu kama uanajeshi full mchakamchaka, viboko nk full kukwepa kazi na hatimaye utendaji kazi kuwa wa ili mradi nipo.
  KAZI YOYOTE NI WITO….

  Like

 5. Makirita Amani March 14, 2014 / 2:38 pm

  Ni kweli mkuu, kuweka fedha mbele imekuwa tatizo la watu kufanya kazi wasizozipenda. Matokeo yake kazi zinawatesa na wanashindwa kufanya vizuri na kutoa majibu mazuri.

  Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s