Siku moja nilikuwa nazungumza na rafiki yangu ambaye ni mwalimu wa sekondari wa shule ya serikali. Nilimuuliza kuhusu changamoto mbalimbali anazokutana nazo kwenye kazi yake na kwa kuwa bado ni mchanga kazini nilitaka kujua malengo yake kwenye kazi hiyo. Tulizungumza mengi sana ila kuna kitu kimoja aliniambia ambacho kilinifanya nifikiri zaidi. Kitu hiki kimekuwa kinafanywa na waajiriwa wengi hasa wa taasisi za umma.

  Mwalimu huyo aliniambia yeye hahangaiki akitaka anafundisha asipotaka anazuga tu, watoto wakifaulu au wakifeli yeye haimpunguzii chochote. Cha msingi ni yeye kuonekana yupo kazini na mwisho wa mwezi anapokea mshahara wake. Jambo hili halikunishtua sana kwa sababu watumishi wengi hasa kwenye sekta za umma ndio wana mtizamo huo. Kilichonifanya nifikiri zaidi ni kwamba tutakwenda hivi mpaka lini na tunapeleka wapi taifa kwa kuwa na watu wengi wenye mtizamo wa aina hii.

              penda kazi yako

  Katika kufikiri, pia nilijiuliza ni nani anayepoteza zaidi katika hali ile kati ya mwajiriwa na mwajiri. Nilichogundua ni kwamba mwajiriwa anaumia zaidi ya mwajiri.

  Kama na wewe umeajiriwa na hufanyi kazi kutoka moyoni kwako una shida kubwa. Kama unafanya tu kazi ili uonekane uko kazini usifikiri unamkomoa mwajiri wako, unajikomoa wewe mwenyewe. Katika vita ya aina hiyo ambayo umeianzisha wewe mwenyewe tayari umeshajipangia kushindwa.

 

 Kwa nini utashindwa kwenye vita hii?

 

  Utashindwa kwenye vita hii kwa sababu zifuatazo;

1. Utapata lawama nyingi kutoka kwa wanaohitaji huduma yako. Kazi inayohesabiwa ni wewe umeifanya. Kama kazi itakuwa nzuri kila mtu ataiona na kuisifia na kama itakuwa mbovu kuna watu wengi sana watakaoathirika na siku zote watakulaumu wewe. Kuwa na watu wengi wanaokulaumu itakufanya ujione huna thamani mbele ya watu.

2. Utakosa furaha kwenye kazi yako.  Kwa kufanya kazi bila ya kuwa na moyo utatoa majibu ambayo hata wewe mwenyewe huyafurahii. Kutokufurahishwa na majibu ya kazi yako ni chanzo moja wapo cha kukosa furaha kwenye maisha na kupata msongo wa mawazo. Kama hakuna kitu ambacho watu wanakisifia kutokana na kazi yako ni lazima utaona kazi yako ni kama kisirani kwako. Hii itakufanya uzidi kuichukia kazi na kila mara upate hasira kali kila unapofanya kazi.

3. Huwezi kufanikiwa. Kama tulivyowahi kuona kwenye makala zilizopita kama unataka kufanikiwa usifanye kazi. Ili ufanikiwe inabidi ufanye kitu unachokipenda, kwa kufanya hivyo utafanya kazi kwa moyo na kwa ubunifu. Hii itakusaidia kutoa majibu mazuri na pia kufanikiwa sana kupitia kazi yako.

4. Utakosa kitu cha kusimamia. Mwisho wa siku ambapo maisha yameshakwenda sana kuna kipindi utahitaji kuangalia nyuma na kuona kuna mchango gani ulioutoa kwenye jamii yako au kwa dunia kiujumla. Kama hutaona kazi ya maana uliyofanya na ambayo watu wengi iliwasaidia utakuwa katika hali mbaya sana. Utajiona kama maisha yako duniani hayakuwa na thamani yoyote.

5. Unaua vipaji vyako na unadidimiza uwezo wako. Wewe ni wa pekee na una uwezo mkubwa sana. Kama hutoipenda kazi yako huwezi kudugua uwezo mkubwa pamoja na ubunifu na vipaji vikubwa vilivyoko ndani yako. Hii itadidimiza uwezo wako na kuua vipaji vyako kwa sababu havitumiki. Dunia itakosa mchango mkubwa sana kutoka kwako.

  Pamoja na kwamba ajira zimekuwa ngumu na waajiri hawajali tena waajiriwa bado kushindana na mwajiri wako kwa kutumia utendaji kazi wako wewe ndiye utakayeshindwa. Kazi yoyote unayofanya ifanye kwa moyo mmoja na mapenzi makubwa. Kama unaona kazi hiyo haikuridhishi ni bora ukaiacha na kwenda kufanya kile kinachokuridhisha. Kuendelea kuing’ang’ania ni kuendelea kujimaliza.

 

Soma; DALILI 8 ZA KUTOFANIKIWA KWA KILE UNACHOFANYA.