Kila mtu ndani ya nafsi yake anaweza kuota ndoto kubwa sana. Kila mmoja wetu ana picha kubwa sana anayoiona kila siku ya jinsi maisha yake na ya wanaomzunguka yanaweza kuwa bora kwa kufanya vitu fulani. Hata wewe una picha fulani ya maisha unayoipata kwenye fikra zako mara kwa mara. Unajiona ukifanya kitu unachokipenda, ukiwa na watu wanaokupenda na pia unajiona ukiwa na maisha ya furaha.

  Pamoja na kuiona picha hiyo mara kwa mara kwa nini mambo hayo hayatokei kwenye maisha yako? Umewahi kujiuliza swali hilo? Tunashindwa kufikia maisha tunayoyaona kwenye ndoto zetu kwa sababu mbalimbali. Hapa nitazungumzia sababu kubwa mbili ambazo zinamuadhiri kila mtu na zimekuwa kikwazo kikubwa sana kwenye maisha yako. Kwa kuzijua sababu hizo leo na kuanza kuzifanyia kazi maisha yako yatabadilika kwa kiasi kikubwa sana na utaanza kuona ndoto zako zikitokea kwenye maisha yako. Hazitatokea tu zenyewe bali utafanya kazi kuzifanya ndoto zako ziwe kweli.

  Unashindwa kufikia ndoto kubwa unazoziota kwenye maisha yako kwa sababu kuu mbili zifuatazo.

 

1. Hakuna mtu mwingine kwenye jamii anayeota ndoto kama zako.

  Mara nyingi unajikuta unafanya mambo ambayo kila mtu kwenye jamii anayafanya, au mambo ambayo yamezoeleka kufanywa kwenye jamii yako. Hivyo kama hakuna anayefanya yale unayoyaona kwenye ndoto zako unashawishika kwamba hayawezekani kufanyika. Hii ni sababu kubwa sana inayoua ndoto za watu wengi sana. Unapenda kufanya vitu ambavyo vimezoeleka kufanyika kwenye jamii yako, asilimia kubwa ya watu kwenye jamii wanafanya mambo wanayofanya sio kwa sababu wanapenda kuyafanya bali kwa sababu ndio watu wa aina yao kwenye jamii wanayafanya. Kuna watu wanakwenda kazini sio kwa sababu kazi hiyo ina maana kwako bali kwa sababu kila mtu kwenye jamii anakwenda kazini. Kuna watu wengi wanakunywa pombe sio kwa sababu wanafurahia bali kwa sababu marafiki zao wote wanakutana jioni kunywa pombe.

  Kwa kuangalia ni kitu gani kinafanyika kwenye jamii kumekufanya mpaka sasa ushindwe kufanya jambo la tofauti ambalo litabadili maisha yako. Acha sasa kuangalia ni vitu gani watu wanafanya na anza kufanya vitu unavyoviona kwenye ndoto zako. Kama ndoto zako haziendi kinyume na sheria na taratibu za maisha, kama ukiamua kutoifata jamii utazifikia.

          USIFUATE KUNDI

  Kwenye maisha ni kama kila mtu anafuata kundi ambalo hajui hata linaelekea wapi. Acha kufuata kundi, tengeneza njia yako mwenyewe ambayo itakufikisha kwenye ndoto zako kubwa. Yeyote anayefuata kundi ana hasara kubwa kwa sababu hawezi kwenda zaidi ya kundi linavyokwenda. Swali la kujiuliza je kundi linamfuata nani? Nani ni kiongozi wa kundi? Jibu ni hakuna, kundi linajiendea tu kusikojulikana. Usitake kuwa mmoja wa watu ambao hawajui ni wapi wanakwenda na maisha yao.

2. Unamsikiliza kila mtu anayetoa maoni kwenye maisha yako.

  Tatizo jingine kubwa linalokufanya ushindwe kuishi maisha ya ndoto zako ni kusikiliza maoni ya kila mtu na kudhani ndio ukweli. Unapofanya jambo lolote la tofauti kwenye maisha yako na ambalo hakuna aliezoea kuona linafanyika kwenye jamii watu wengi sana watakupinga na kukuambia unapotea. Na kwakuwa hatujui tunakubaliana nao na kuona wako sahihi hivyo tunaacha kuzikimbiza ndoto zetu. Kama jambo unalolifanya haliendi kinyume na sheria ama taratibu za jamii na kama umeshaweka mipango ya kufikia jambo hilo ni vyema usisikilize mtu yeyote anayekukatisha tamaa. Yeyote anayekuambia hapana au huwezi hayo ni maoni yake na wala hayapo karibu na ukweli. Kwanza yeye mwenyewe anafuata kundi ambalo hajui linampeleka wapi, atawezaje kujua kama wewe unaelekea kubaya?

  Kingine kikubwa ni kufikiri labda kuna watu wanajali sana kuhusu maisha yetu. Kuna siri moja unayotakiwa kujua, hakuna mtu anayejali kuhusu maisha yako, kila mtu anayafikiria maisha yake na changamoto anazokutana nazo. Hivyo anavyokukatisha tamaa sio kwamba atakwenda kuumiza kichwa aje kukupa ushauri mzuri, hapana, na yeye ataendelea na maisha yake ambayo bado yanamsumbua. Usifikiri kuna mtu anayekosa usingizi kwa sababu ya maisha yako wewe, wewe pekee ndiye unayepaswa kuyafikiria maisha yako na ndoto zako.

  Unapofanya jambo la tofauti kwenye jamii wengi watakupinga na kukukatisha tamaa. Kama ukikubaliana nao hutofanya lolote na utakuwa na maisha yasiyo na maana kama hao wanaokukatisha tamaa. Kama usipokubaliana nao na ukaendelea na mipango yako na ukafanikiwa(na ni lazima ufanikiwe) watakuwa wa kwanza kukusifia na kutoa kauli nzuri kwamba walijua utaweza.

  Usiangalie sana watu wanafanya nini na usisikilize sana watu wanaongea nini, angalia kwa kujifunza na sikiliza kwa kujifunza ila usikatishwe tamaa na mambo hayo mawili kwa sababu wewe unayajua maisha yako zaidi ya mtu mwingine yeyote.