Hofu ni kitu ambacho kila binadamu anakipitia kwenye maisha yake katika nyakati tofauti. Hata watu ambao wanaonekana ni mashujaa ama wamefanikiwa sana kuna nyakati wanakuwa na hofu. Jinsi tunavyokabiliana na hofu zetu za kila siku ndiyo inaleta tofauti kati ya wanaoshindwa na kuonekana wanyonge na wanaoshinda na kuwa mashujaa.

  Baadhi ya hofu tunazokuwa nazo watu wengi ni hofu ya kushindwa, hofu ya mafanikio, hofu ya kukataliwa, hofu ya kifo, hofu ya kutokujua kuhusu kesho na hofu ya makosa uliyofanya nyuma.

          hofu

  Wanaofanikiwa wako tayari kuzikabili hofu zao na kufanya yale wanayohofia. Wanaoshindwa wanakubaliana na hofu na hivyo kutofanya chochote.

  Hofu ni USHAHIDI WA UONGO UNAOONEKANA KAMA UKWELI. Hofu ya aina yoyote ile ni uongo, kwa sababu mara nyingi huwa hatuna hakika na vitu tunavyohofia ila bado tunakuwa na hofu kubwa.

  Kutokana na hofu umeshindwa kufanya mambo makubwa kwenye maisha yako. Kutokana na hofu kila siku umekuwa ukiishi maisha ambayo sio ya furaha. Hofu imekufanya ushindwe kufikia ndoto zako kubwa unazoota.

  Leo nataka nikuoneshe ni jinsi gani unavyoweza kunufaika na hofu yoyote unayokuwa nayo kwenye maisha yako. Hofu inatuambia ni kitu gani cha kufanya. Mara nyingi yale mambo ambayo yana faida kubwa kwenye maisha yetu kama tungeyafanya ndio tunakuwa na hofu kubwa. Kwa kujua hivyo kila unapokuwa na hofu kuhusu jambo fulani basi inabidi uanze kulifanya mara moja maana litakupatia mafanikio makubwa.

  Kwa kuwa mafanikio yenyewe yana hofu, jambo lolote ambalo linaweza kutuletea mafanikio makubwa huwa tunalihofia. Vitu ambavyo unahofia kuvifanya ndio vitu ambavyo ukivifanya utafanikiwa kwa kiasi kikubwa. Vitu ambavyo unahofia kuvifanya ndio vitu ambavyo vimechukua nguvu zako.

  Kwa kuwa unahofia kufanya jambo fulani basi unajikuta unaamini huwezi kufanya jambo hilo. Huu ni ushahidi wa uongo ambao umerudiwa sana mpaka unaaminika kuwa ukweli.

  Anza sasa kukabiliana na hofu yako kwa kufanya yale mambo ambayo unahofia kuyafanya. Kama una hofu ukifanya biashara utapata hasara, anza sasa kufanya biashara hiyo kwa ngazi ndogo huku ukijifunza. Kama unahofu ukianza kuishi maisha ya ndoto yako watu wengi watakushangaa na kukutenga, anza mara moja kuishi maisha hayo.

  Usipoteze muda wako wa thamani kwa kuhofia vitu ambavyo huna uhakika navyo. Fanya kile unachohitaji kufanya na usiipe nafasi hofu kukuzuia kufikia mafanikio yako.

  Kumbuka; “mambo unayohofia kufanya ndio inabidi uyafanye ili ufanikiwe