Mara nyingi huwa tunaweka malengo na mipango mikubwa kwenye maisha yetu. Na tunakuwa na mipango yote ya kufanya ila inapofikia wakati wa kutekeleza tunashindwa kufanya hivyo.
Kuna wakati unapanga kuanza kufanya jambo fulani ili kuboresha maisha yako, au wakati mwingine unapanga kuacha tabia fulani ambazo zinakuzuia kufikia malengo yako makubwa. Unaweka mipango mizuri ila kwenye utekelezaji unashindwa kabisa.
Kila siku una mambo mengi ya kufanya na muda unaonekana hautoshi, kila mara ukijaribu kupangilia muda wako bado kuna vitu unashindwa kuvifanya.
Kama unapitia moja au yote kati ya hayo(ni lazima unapitia) ni vyema ukajifunza njia za kuepukana na hali hizo. Kwa sababu usipojifunza njia za kuepuka utajikuta kila siku unaweka malengo na mipango mikubwa ila utekelezaji unakuwa sifuri. Hii itakufanya ujisikie vibaya na ukose furaha.
Watu wengi wana mipango mingi na mizuri ila wanashindwa kuitekeleza kutokana na tabia ya kuahirisha mambo ya muhimu. Wanapokutana na jambo linalohitaji kufikiri ama kufanya kazi hupata sababu ya kutolifanya na baadae kujikuta hawajalifanya kabisa.
Kwenye shughuli yoyote unayofanya iwe ajira, biashara au hata masomo kuna mambo machache ukiyafanya utapata majibu makubwa na mazuri kushinda mambo mengine. Mara nyingi mambo haya ndio yanakuwa na uahirishaji mkubwa.
Leo nakushirikisha kitabu kinachoitwa EAT THAT FROG kilichoandikwa na Brian Tracy. Kitabu hiki kinaelezea njia ishirini na moja unazoweza kutumia kuacha kuahirisha mambo muhimu kwako na kuweza kufanya mambo mengi ndani ya muda mfupi.
Katika kitabu hiki Brian anasema kwamba kama ingekuwa kila siku asubuhi kitu cha kwanza kwako ni kula chura mzima isingesaidia kama ungemwangalia chura huyo kwa muda mrefu. Kwa kuwa unajua lazima umle chura huyo basi ni vyema ukamla mara moja na ukaendelea na mambo mengine.
Chura anayemzungumzia hapa ni jukumu kubwa lililoko mbele yako kila siku. Jukumu hilo unaweza kuwa hulipendi sana ila ndio jukumu muhimu kwako kufikia malengo yako au kufanikiwa.
Brian ametoa njia 21 za kukusaidia kuacha tabia ya kuahirisha mambo, kupangilia muda wako vizuri na kuweza kukamilisha mambo mengi ndani ya muda mfupi.
Kisome kitabu hiki na anza kutumia mafundisho yake kwenye maisha yako na utaona mabadiliko makubwa ndani ya muda mfupi. Kitabu hiki ni kifupi sana na unaweza kukisoma ndani ya masaa mawili na kikawa kimeisha.
Kama wewe ni bingwa wa kuahirisha mambo tafadhali usiahirishe kusoma kitabu hiki. Hebu katika mambo yote unayoahirisha kitabu hiki kisiwe moja ya mambo hayo. Maana kitabu hiki kitakusaidia kuacha tabia hiyo ya kuahirisha mambo ambayo imekuzuia kufikia mafanikio unayotazamia. Kama utaahirisha kusoma kitabu hiki basi wewe hakuna jambo kubwa utakaloweza kulifanya bila ya kuahirisha.
Pata kitabu hiki kwa kubonyeza maandishi ya kitabu EAT THAT FROG.
Endelea kuwepo kwenye mtandao huu wa amka mtanzania ili uendelee kupata mambo mazuri. Kama bado hujajiunga na mtandao huu bonyeza maandishi haya kisha uweke email yako ili uweze kupokea vitabu na makala nzuri zitakazobadili maisha yako.
Nakutakia kila la kheri kwenye usomaji wa kitabu hiki na nina imani kwamba baada ya kumaliza kukisoma utaanza kula vyura uliokuwa unawakwepa kwa muda mrefu.
Kupata kitabu hiki bonyeza maandishi haya na utakidownload kitabu.