Kama unataka kuanza biashara au unataka kukuza biashara yako ni vyema kupima soko unaloingia kabla ya kuingia. Hii itakupa mwanga wa kitu gani unakwenda kukutana nacho. Ni muhimu kufanya utafiti wa soko ili kujipanga jinsi utakavyoingia kwenye soko hilo. Kwa bidhaa ama huduma yoyote unayotoa au unayopanga kutoa pima soko kwa kutumia vigezo hivi kumi
1. Uhitaji.
Ni kwa kiasi gani watu wanahitaji bidhaa au huduma unayotoa. Na wanaitaka kwa haraka kiasi gani? Kama unachotoa kina uhitaji mkubwa ni dalili nzuri kwamba unaweza kufanya biashara nzuri.
2. Ukubwa wa soko.
Je watu wenye uhitaji wa bidhaa yako ni wengi kiasi gani? Kama kuna watu wachache wanaohitaji bidhaa yako ni dhahiri itakuwa vigumu kwako kufanya biashara kwa muda mrefu. Jua ukubwa wa soko kabla ya kuingia ili usijekupata hasara kubwa.
3. Uwezo wa bei.
Ni gharama kubwa kiasi gani mnunuaji wa kawaida yuko tayari kutoa ili kupata bidhaa au huduma yako. Kama watu wako tayari kulipa bei ambayo itawezesha wewe kukidhi gharama zako na kubaki na faida hapo kuna biashara. Ila kama bei ambayo mnunuaji wa kawaida yuko tayari kutoa ni ndogo itakuwa vigumu sana kwako kufanya biashara.
4. Gharama ya kumpata mteja.
Ni gharama kiasi gani utaingia ili kuweza kupata wateja? Kuna biashara ambazo zitakuhitaji kutangaza kwenye vyombo mbalimbali vya habari ili watu wajue ipo. Ila biashara nyingine zinakuwepo tu na watu wanaziona na kuzifuata. Kwa mfano sheli ya mafuta iliyojengwa kando ya barabara itatumia gharama ndogo kupata wateja kuliko iliyopo mbali na barabara.
5. Gharama ya kufikisha bidhaa au huduma.
Ni gharama kiasi gani itakutoka ili uweze kuzalisha bidhaa au huduma yako mpaka inapomfikia mteja? Kama gharama ni kubwa itapelekea bei kuwa kubwa na inaweza kupunguza wateja. Kama gharama ni ndogo unaweza kuuza kwa bei ya kawaida na ukapata wateja wengi.
6. Upekee wa bidhaa.
Je bidhaa au huduma unayotoa ina utofauti gani wa kipekee ukilinganisha na inayotolewa na watu wengine? Kama huna tofauti na wafanyabishara wengine utajikuta kwenye ushindani mkubwa wa kugombania wateja kitu ambacho kitakufanya ushindwe kukuza biashara yako. Kama unatoa kitu cha kipekee tofauti na wengine utaweza kuwavutia wateja bila ya kuingia kwenye ushindani mkubwa.
7. Kasi ya kuingia sokoni.
Itakuchukua muda gani kutengeneza bidhaa au huduma mpaka kuifikisha sokoni? Kuna baadhi ya biashara unaweza kuliteka soko haraka na biashara nyingine ikakuchukua muda sana.
8. Uwekezaji.
Ni kiasi gani inabidi uwekeze kabla ya kuanza kuuza bidhaa au huduma yako? Hapa unazungumzia fedha, muda na rasilimali nyingine. Kama unahitaji uwekezaji mkubwa inabidi kujipanga kwa hilo.
9. Uwezo wa kuuza bidhaa nyingine.
Je una uwezo wa kuuza bidhaa au huduma nyingine pamoja na hiyo unayouza au unayopanga kuuza? Kuna baadhi ya bidhaa zinaweza kuuzwa pamoja na hii kuongeza biashara. Kwa mfano mtu akinunua kompyuta unaweza kumuuzia na flash disk, antivirus na hata spika za nje. Jinsi ambavyo bidhaa au huduma yako inaweza kuuzwa na bidhaa nyingine ndivyo biashara yako inavyoweza kukua.
10. Mahitaji ya ziada.
Baada ya kutoa bidhaa au huduma yako ni gharama kiasi gani itakuingia kuendelea kuuza? Baadhi ya bidhaa unaweza kuzalisha mara moja na ikabaki kuuza ila bidhaa nyingine zinahitaji kuendelea kufanya kazi kubwa. Kwa mfano mtu anayetoa huduma ya ushauri anahitaji kuendelea kufanya kazi ili alipwe ila anayeandika kitabu hahitaji kuendelea kukiandika tena kinaendelea kuchapwa tu.
Angalia biashara yako au wazo lako la biashara kwa kutumia vigezo hivyo na ukiona inakidhi vigezo vingi(zaidi ya nusu) unaweza kuwa na biashara nzuri. Kama inakidhi vigezo vichache inakubidi uboreshe au uangalie njia nyingine. Unaweza kuwa na watu wanohitaji sana bidhaa fulani ila ukipiga gharama za kuifikisha sokoni inakuwa bei kubwa kuliko uwezo wa wahitaji. Katika hali kama hii ni rahisi kushindwa kukuza biashara.
Kama kuna lolote linalohitaji ufafanuzi tafadhali weka maoni yako hapo chini.