Kama tulivyoona kwenye makala zilizopita, ili kuweza kuanzisha na kukuza biashara ni muhimu sana kutengeneza thamani. Ni muhimu kutengeneza kitu ambacho watu wanakihitaji na wana uwezo wa kulipia bei unayouza ili kukipata kitu hicho. Katika kuanzisha biashara ubunifu mkubwa unahitajika ila huna haja ya kubuni kitu ambacho haipo kabisa kwenye mazingira ama dunia ya sasa.
Katika mazingira yoyote kuna njia kumi na mbili za kutengeneza thamani, hapa namaanisha kuna njia kumi na mbili za kuweza kuanzisha biashara ambayo itakua sana kama utajipanga vizuri. Zisome njia hizi kisha angalia ni ipi unaweza kuitumia na kisha jifunze zaidi kuhusu njia hiyo.
1. Kutengeneza bidhaa.
Hapa unatengeneza bidhaa inayoonekana ama kutumika na kuiuza kwa watu wengine. Katika aina hii ya biashara unatakiwa kutengeneza bidhaa yako kwa gharama ndogo na baadae kuuza kwa bei ya juu kidogo ukilinganisha na gharama uliyotengenezea, hapo ndipo unapoweza kutengeneza faida.
Uzuri wa biashara ya bidhaa ni kwamba baadhi ya bidhaa unaweza kutengeneza mara moja tu na baada ya hapo ukawa unazalisha bidhaa nyingine kutoka kwenye hiyo moja.
2. Kutoa Huduma.
Hii ni biashara ambapo unamsaidia mtu na yeye anakulipa fedha. Ili kuweza kutengeneza biashara ya kutoa huduma inabidi uwe na ujuzi au uzoefu ambao watu wengine hawana ila wanahitaji sana. Kwa njia hii wanakuwa tayari kukupa fedha ili kunufaika na huduma yako. Huduma za ushauri, bishara za saluni, huduma za afya ni baadhi ya biashara ambazo zinatoa huduma muhimu kwa watu.
3. Vitu vinavyotumika na watu wengi.
Hii ni biashara ambapo mtu ananunua au kutengeneza vitu ambavyo vinaweza kutumika na watu wengi kwa wakati mmoja au kwa kubadilishana. Aina hii ya biashara inahitaji uwekezaji mkubwa mwanzoni ila baada ya hapo mmiliki anakuwa anakusanya mapato makubwa. Biashara kama sehemu za kufanyia mazoezi(gym club) au sehemu za burudani kama fukwe zilizotengenezwa vizuri ni mifano ya aina hii ya biashara.
4. Kujisaliji/kujiunga.
Hii ni aina ya biashara ambapo wateja wanajisajili kupata huduma fulani kwa kipindi fulani na kulipia usajili wao. Ili kutengeneza biashara ya aina hii ni muhimu mtu kuwa na huduma ambayo watu wanaihitaji na kuiboresha kadiri ya siku zinavyokwenda. Ili kukuza biashara hii ya kujisajili ni muhimu kwa mfanyabiashara kushawishi watu wengi zaidi kujisajili/kujiunga na biashara hiyo. Huduma za ving’amuzi vya tv ni mfano wa biashara hii. Kila mwezi unalipa ada fulani ili kuweza kuona chanel nzuri za tv. KISIMA CHA MAARIFA pia ni aina hii ya biashara ambapo ulilipia ili kujiunga na mtandao huu ambao unakupa maarifa mbalimbali ya kukunufaisha kwenye maisha.
5. Uchuuzi.
Uchuuzi ndio aina maarufu ya biashara katika mazingira yetu. Katika uchuuzi mfanyabiashara ananunua bidhaa kutoka kwa mzalishaji au muuzaji wa jumla kwa bei ndogo kisha kuziuza kwa mtumiaji wa mwisho kwa bei kubwa kidogo ili kutengeneza faida. Ili kuweza kutengeneza na kukuza biashara ya uchuuzi ni muhimu mfanya biashara kupata bidhaa zake kwa bei ndogo sana na kuweza kuziuza kwa bei kubwa ambayo soko litaweza kustahimili ili aweze kutengeneza faida. Maduka ya mahitaji muhimu kwenye mitaa yetu ni aina ya biashara ya uchuuzi.
6. Kupangisha/kukodisha.
Hii ni aina ya biashara ambapo mtu anatengeneza na kumiliki kitu ambacho watu wengine wanaweza kukitumia na kulipia. Ili kuwa na biashara ya aina hii unahitaji kumiliki kitu ambacho watu wengine hawawezi kumiliki ila wanahitaji kutumia hivyo wanakulipa wewe fedha kwa ajili ya kutumia kitu hicho. Kupanga nyumba za kuishi ni mfano mzuri wa biashara hii. Pia kukodisha vifaa au magari ni aina hii ya biashara.
7. Uwakala/Udalali.
Hii ni biashara ambapo mtu anauza kitu ambacho hamiliki yeye moja kwa moja. Katika aina hii ya biashara, mfanya biashara anamtafuta mtu ambaye tayari ana bidhaa au huduma kisha kushirikiana nae kutafuta soko la huduma hiyo. Kama akifanikiwa kupata mteja na kuuza, wakala au dalali anapata asilimia fulani ya faida kutokana na makubaliano. Mawakala wa kampuni za bima na madalali wa nyumba, magari na hata mazao ni mifano ya aina hii ya biashara.
8. Kuuza hadhira(audience)
Hii ni aina ya biashara ambapo unakusanya hadhira kutokana na huduma fulani muhimu unayotoa kisha unauza hadhira hiyo kwa mtu mwingine anayehitaji kuitumia. Mfano mzuri wa biashara ya aina hii ni mitandao inayojiendesha kwa kuweka matangazo ya biashara. Katika mitandao hii kwanza huanza kwa kutoa huduma au taarifa ambazo ni muhimu kwa watu wengi, baada ya kuwa na watu wengi wanaotembelea mtandao huo anaweza kushawishi kampuni kuweka matangazo yake kwenye mtandao huo na kuwafikia watu hao wengi. Vyombo vingi vya habari na mitandao mingi kama blog zinajiendesha kwa kutegemea matangazo.
9. Mikopo.
Hii ni biashara ambapo mtu mwenye mali au fedha anampa mtu mwingine aweze kuzitumia baadae anamrudishia fedha au thamani ya mali hiyo pamoja na malipo ya ziada yanayojulikana kama riba. Mikopo ya fedha, nyumba, magari na vitu vingine ni aina hii ya biashara. Biashara ya mikopo imekuwa maarufu sana kwa siku za hivi karibunu kutokana na mazingira magumu ya kupata fedha au mali husika moja kwa moja.
10. Uchaguzi.
Hii ni biashara inayompatia mteja uwezo wa kuchagua kufanya jambo fulani au kutokulifanya kama atakuwa na jambo lingine muhimu la kufanya. Biashara hii sio maarufu sana katika mazingira yetu ila imeanza kukua kwa kasi. Mfano mzuri wa biashara hii ni uuzaji wa tiketi za maonyesho ya sinema au maonyesho mengine. Kwa mteja kununua tiketi kabla ya siku ya onyesho kunampatia haki ya kuweza kuhudhuria onyesho hilo ila pia hakumlazimishi kufanya hivyo. Kama akiwa na jambo jingine muhimu la kufanya anaweza asihudhurie onyesho hilo. Hii inampa mteja uwezo wa kuchagua kuchukua hatua.
11. Bima.
Hii ni biashara ambapo mtu anahamisha hatari au hasara kutoka kwake na kwenda kwa mtu mwingine. Mtu anayefanya biashara ya bima, anakusanya fedha kwa wateja wake na baadae kuwafidia kama jambo baya litatokea kwa mteja wake na kwa jambo ambalo mteja amekatia bima. Mifano ya biashara hii ni bima ya afya, bima ya magari, bima ya nyumba na nyingine nyingi. Kwenye bima ya afya mteja analipa fedha kabla hajaumwa ili baadae ikitokea akaumwa aweze kutibiwa hata kama hana fedha.
12. Mitaji.
Hii ni biashara ambayo mtu anatoa mtaji kwenye biashara nyingine na baadae anapata sehemu ya faida ya biashara hiyo kulingana na mtaji aliochangia. Ili kuweza kufanya biashara ya aina hii unahitaji kuwa na fedha au rasilimali ambazo unaweza kuzitoa na zikanufaisha biashara nyingine na wewe kuwa mshikadau au mwanahisa wa biashara hiyo. Mfano wa biashara hii ni ununuaji wa hisa katika makampuni mbalimbali. Unaponunua hisa unachangia mtaji na kampuni inapopata faida unapewa gawio kulingana na mtaji uliochangia.
Hizo ndio aina kumi na mbili za kutengeneza thamani kwenye biashara. Biashara yoyote unayofanya au unayotazamia kufanya lazima inaingia kwenye moja ya aina hizo kumi na mbili. Jua upo kwenye kundi gani kisha jifunze zaidi kuhusiana na kundi hilo la biashara ili uweze kufanikiwa zaidi. Baadae tutakuja kuchambua kundi moja moja na kuona faida na hasara zake na jinsi gani ya kuweza kufanikiwa katika kundi hilo la biashara.
Kumbuka kuna uwezekano wa biashara moja ikawa kwenye kundi zaidi ya moja kwenye makundi hayo kumi na mbili. Biashara inaweza kuwa inazalisha bidhaa au inatoa huduma na wakati huo huo inauza kwa njia ya uwakala au udalali.
Kwa maoni au mchango wowote tafadhali weka maoni yako hapo chini.