Kwa kipindi kirefu tumekuwa tukiaminishwa kwamba kusoma kwa bidii na kufaulu sana ndio kutakuwezesha kupata kazi nzuri na kuwa na maisha mazuri. Hivyo watu walikazana kusoma na hata kwa kukariri ili kupata matokeo mazuri na kupata kazi nzuri. Na baada ya kuhitimu mafunzo wengi wanaweka kujifunza pembeni na kufanya kazi tu. Hii ilifanya kazi sana kipindi cha nyuma ila kwa ulimwengu huu na ujao inafanya kazi kwa kiwango kidogo sana na inaelekea kufa kabisa. Kama bado unafikiri hivi nina habari mbaya na nzuri kwako. Kabla ya kukupa habari hizi naomba nikupe mfano halisi uliotokea siku sio nyingi.

  Miezi michache iliyopita afisa mmoja kutoka kampuni ya Google alikuwa akihojiwa na chombo kimoja cha habari na swali aliloulizwa ni kigezo gani kampuni hiyo kubwa duniani inatumia kuajiri watu? Afisa huyu alisema kigezo wanachokitumia wao ni uwezo na nia ya kujifunza ya mtu pamoja na uwezo wa kujiongoza mwenyewe. Alipoulizwa kuhusu ufaulu mkubwa wa darasani alisema ufaulu wa darasani hausadifu uwezo wa kufanya kazi na kutoa majibu mazuri. Alisema mazingira ya kufaulu darasani ni tofauti sana na mazingira ya kufaulu kwenye maisha ya kazi na changamoto mbalimbali. Alisema waligundua hilo baada ya kuwa wanaajiri kwa vigezo vya ufaulu wa darasani na ikawafanya kuwa wanapata wafanyakazi ambao ni mzigo kwao.

kujifunza

  Ukiacha Google, makampuni mengi duniani hivi sasa yanatumia vigezo tofauti na ufaulu kwenye kuajiri. Hali hii imeshafika hata Tanzania ambapo kampuni nyingi zinazopewa kazi ya kusaili maombi ya ajira zimekuwa zikitumia vigezo vingi zaidi tu ya ufaulu wa darasani.

  Ukweli ni kwamba aina nyingi za kazi zinabadilika kutokana na mabadiliko ya teknolojia na maisha pia. Hivyo mtu anayeweza kujifunza na kuweza kubadilika na mabadiliko haya anakuwa wa thamani kubwa kuliko ambae hawezi.

  Kama nilivyokwambia nitakuwa na habari mbaya na habari nzuri kwako. Naanza kwa kukupa habari mbaya halafu nitamalizia na habari nzuri.

Habari mbaya kwako

Dunia inabadilika kwa kasi kubwa sana, kama na wewe hubadiliki nayo unaachwa nyuma ama umeshaachwa nyuma.

  Kama ulifikiri kujifunza mambo mapya kuliisha siku ulipohitimu mafunzo uko kwenye njia ya kupotea. Kama umeshapata ajira na nafasi pekee ya wewe kujifunza mambo mapya ni mpaka uandaliwe semina na mwajiri wako na tena ulipwe utaachwa nyuma muda sio mrefu. Utashangaa unabaki kwenye ngazi hiyo hiyo ya ajira, wanakuja vijana wanapanda ngazi na kukuacha unashangaa.

  Kama upo masomoni au umeshamaliza ila bado hujapata ajira na unaendelea kutumia kile tu ulichojifunza itakuwia vigumu sana kupata ajira. Utaitwa kwenye usaili wa ajira mbalimbali ila utakosa nafasi licha ya kuwa na matokeo mazuri.

  Katika hali yoyote uliyopo sasa ni muhimu kujifunza vitu vya ziada na kuonesha uwezo wako wa ziada.

Habari nzuri kwako

  Habari njema kwako ni kwamba unaweza kujifunza vitu hivi vya ziada na ukaongeza uwezo wako na thamani yako. Kuna njia mbili za kujifunza mambo mapya;

1. Kujifunza kwa kujaribu mambo mapya, kufanya makosa na kutokuyarudia makosa hayo. Hii ni kwa wale walioajiriwa, waliojiajiri au ambao wanafanya biashara. Ni vigumu kujifunza vitu vipya kama kila siku unakuwa unafanya mambo yale yale unayofanya. Kuna umuhimu wa kuwa mbunifu zaidi kujaribu mbinu mpya ambazo zitakupelekea kushindwa na katika kushindwa utajifunza zaidi.

2. Kujifunza vitu vipya kwa kujisomea na kutumia mafunzo hayo. Hii inawezekana kwa wote ambao wanafanya kazi, wanaosoma bado au ambao wameshamaliza masomo ila bado hawajapata ajira. Dunia ya sasa ina njia nyingi sana rahisi za kujifunza. Unaweza kujifunza kwa kujisomea vitabu, kusoma kwenye mtandao, kuangalia video, kujiandikisha kwenye kozi zinazotolewa na hata kuangalia wanachofanya waliofanikiwa na kuiga.

  Njia zote hizi zinaweza kukupatia elimu ambayo itakuwezesha kwenda na kasi ya mabadiliko ya dunia ya sasa.

  Kama unaona ni vigumu kwako kujifunza kutoka kwenye vyanzo hivyo vingi au hujui uanzie wapi kuna njia rahisi kwako kuanza kujifunza mambo ambayo ni ya msingi kwenye maisha, kazi na biashara. Njia hiyo ni kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ukiwa ndani ya kisima cha maarifa utapata mafunzo mbalimbali kwa lugha rahisi ya kiswahili na kuweza kuanza kuyatumia kuboresha maisha yako. Kama unataka kujiunga na kisima cha maarifa bonyeza maandishi haya kupata maelezo zaidi.

  Kwa kazi ama biashara yoyote unayoifanya kujifunza kila mara ndio nguzo kuu ya kuweza kupata mafanikio makubwa. Kama utaamua kuacha kujifunza utabaki nyuma na kuachwa kabisa na kasi ya mabadiliko ya dunia.