Karibu sana kwenye kipengele cha TABIA ZA MAFANIKIO ewe msomaji na msafiri mwenzangu katika safari ya mafanikio makubwa sana. Kama nilivyoahidi kila mwezi tutakuwa tukijadili tabia moja ya mafanikio na kuona jinsi gani inatuzuia kufikia mafanikio na njia zipi tunaweza kutumia kuboresha tabia hiyo ili tuweze kufikia mafanikio makubwa. Kila wiki siku ya jumanne kutakuwa na makala moja inayozungumzia tabia husika hivyo kila mwezi utakuwa na makala nne.Unaweza kuona makala nne ni fupi sana ila utapata vitu vingi sana ambavyo ukiweza kuvitumia utabadili maisha yako kwa kiwango kikubwa sana.
Kitu kikubwa sana kwenye kipengele hiki kipya cha KUJENGA TABIA ZA MAFANIKIO ni kwamba tutakuwa na mazoezi ya kufanya, yaani kuna vitu utahitajika kufanya ili uweze kwenda vizuri na mabadiliko haya ya tabia.
Mwezi huu wa tano tunazungumzia muda, kitu ambacho kinaonekana hakina thamani kubwa ila kinachoweza kuzuia au kutufikisha kwenye mafanikio yetu.
Kila mtu anapoteza muda.
Ni jambo lisilopingika kwamba kila mtu anapoteza muda, hata uwe makini kiasi gani kuna muda ambao utaupoteza, hilo sio tatizo hasa kwa anayejua kwamba kuna muda anaupoteza. Ila wewe kama hujui kuna muda unaupoteza uko kwenye hatari kubwa.
Nasema kila mtu anapoteza muda kwa sababu mipango sio matumizi. Umepanga ukutane na mtu saa nane inafika saa nane humuoni unampigia simu anakwambia nakuja sasa hivi nisubiri, unakaa saa nzima ndio anatokea, kuna matukio mengi sana ambayo yanatufanya tupoteze muda kidogo katika masaa yetu 24.
Tofauti kubwa ya waliofanikiwa na wanaosukuma maisha.
Tofauti kubwa kati ya waliofanikiwa na wanaosukuma siku ziende ni matumizi ya muda. Zipo tofauti nyingi sana kitabia ambazo tutazijadili ndani ya KISIMA CHA MAARIFA, ila iliyo kubwa na ya muhimu sana ni muda.
Binadamu wote tumepewa masaa 24 kwa siku, ila ndani ya masaa haya 24 kuna ambao wanafanya mambo makubwa sana na kuna ambao wanaishia kufanya vitu ambavyo hawajui hata vina msaada gani. Ili uweze kufikia mafanikio unayotarajia ni lazima uwe mtumiaji mzuri sana wa muda.
Matumizi ya muda ya mtanzania wa kawaida.
Kwa maisha ya kawaida kabisa ya kitanzania ambayo karibu asilimia 90 wanaishi matumizi yao ya muda yako hivi, angalia vizuri halafu utaniambia hapo chini kwenye maoni kama una tofauti kubwa.
Siku za kufanya kazi. Kwa mtanzania wa kawaida ambaye ameajiriwa au anafanya shughuli zake kama biashara ndogo ndogo na hata za kati siku zake za kazi zinakuwa ni tano au sita kwa wiki. Kwa wale ambao hawaendi kazini siku mbili kwa wiki tukihesabu kwa mwaka kuna wiki 52 hivyo ukizidisha kwa mbili unapata siku 104. Tukiongeza siku za sikukuu, mwaka mpya(1), mapinduzi(1), karume(1), pasaka(2), muungano(1), wafanyakazi(1), sabasaba(1), nanenane(1), maulidi(1), iddi(2), nyerere(1), krismasi(2), Jumla tunapata siku 15, kwa hiyo tukijumlisha tunapata siku 129. Hizi ni siku ambazo wengi hawafanyi kazi.
Tukija kwenye siku ya kufanya kazi, wafanyakazi wengi wanafanya kazi masaa 8 kwa siku, pia tuweke masaa 8 ya kulala, na masaa mengine 4 ya kupumzika na hapa ana masaa mengine manne kwa siku ambayo hajui huwa yanaishia wapi. hivyo kwa siku tano kwa wiki anakuwa na masaa 20, kwa mwaka yanakuwa masaa 1040 ambayo ni sawa na siku 43. Siku hizi 43 ukijumlisha na zile 129 unapata siku 182. Yaani kwa mwaka mzima una siku 182 zilizojaa ambazo unazipoteza moja kwa moja bila ya kufanya jambo lolote la kuboresha maisha yako au kufanya kazi yenye manufaa kwa wengine. Hapo sijaweka likizo ya siku 28 ambayo kila mfanyakazi anapewa kwa mwaka, utajikuta unafikisha siku 200 ambazo hufanyi kazi. Hapo bado hujaumwa, hujapata matatizo ambayo yatakuzuia kufanya kazi.
Mwaka una siku 365 ambayo nusu yake ni siku 182, hii ina maana kwamba kama utaendelea kuishi maisha kwa matumizi ya muda kama hapo juu ina maana nusu ya maisha yako unaipoteza na vibaya zaidi hujui unaipotezea wapi.
Sasa hebu niambie unawezaje kufanya mambo makubwa kama nusu ya maisha yako huishi?
Kama unajipa ahueni kwamba jumamosi unakwenda kazini na jumapili unakwenda kusali bado tukipiga hesabu hizi vizuri una zaidi ya siku 100 unazipoteza kila mwaka. Huoni kwamba hizi siku 100 ni nyingi sana kuzipoteza?
Muda unapotelea wapi na wakati niko bize siku nzima?
Hili ni swali ambalo wengi hujitetea nalo wanapoambiwa wanapoteza muda. Unafikiria siku nzima upo bize, mpaka unachelewa kulala sasa huu muda unaopoteza ni upi? Cha kwanza unachotakiwa kuelewa ni kwamba kuwa bize sio sawa na kufanya kazi, hii inawachanganya wengi sana. Unaweza kuwa bize sana na watu wakakuona uko bize ila kazi unayofanya ikawa kidogo sana.
Muda mwingi sana unaupoteza kwenye kufanya mambo ambayo hayana msingi wowote kwenye maisha yako. Kama ulisoma makala ya MAISHA YA BWANA MIKE utakuwa umeshapata mwanga muda mwingi wa maisha yako unaupotezea wapi. Kama hujaisoma bonyeza hayo maandishi ya herufi kubwa kisha uisome, wengi wa walioisoma wameniandikia kuniambia ni jinsi gani maisha yao yanavyofanana na maisha ya bwana mike.
ZOEZI LA WIKI HII.
Kwanzia leo jumanne asubuhi mpaka kufikia jumatatu jioni utafanya zoezi moja la kunakili kila sehemu ambapo unatumia muda wako. Nunua kijitabu kidogo kama notebook na uwe nacho pamoja na kalamu kila sehemu utakayokwenda kwa wiki hii nzima. Nakili muda unaoanza kufanya jambo mpaka unapomaliza. Kwa mfano kama umetoka nyumbani saa kumu na mbili asubuhi andika, kama umefika kazini saa moja na nusu andika, kama ulipofika umeanza kwa kupiga story andika muda wa kuanza story na kumaliza. Kama ulichungulia facebook kidogo andika muda ulioingia na utakaotoka, kama ulikuwa unafanya kazi ila ukafika katikati ukajisikia kuingia kwenye mtandao kidogo andika muda ulioingia na uliotoka. Kama umeongea na simu nakili muda uliotumia kuandika na pia nakili idadi ya meseji ulizosoma na kutuma kwa siku. Nakili hivi kwa kila unachofanya mpaka mwisho wa siku na muda unaoingia kitandani mpaka tena unapoamka.
Tumia muda huu wa kuandika bila ya mtu yeyote kujua kwa sababu kama wenzako wakijua watakukatisha tamaa na utaacha zoezi hili mara moja.Utakapoacha wewe ndiye utakayekuwa na hasara maana wao hawaoni umuhimu wa unachofanya.
Wiki ijayo tutakutana hapa kujua ni sehemu gani tunapoteza muda wetu mwingi na jinsi gani tunaweza kuukomboa. Nasisitiza fanya hivi kwa wiki nzima na pia tumia kalamu na karatasi kuandika, sio kompyuta wala simu, tumia karatasi. Kama utapenda kutushirikisha mambo unayoyaona yanakula muda wako wakati unaendelea na zoezi hili unaweza kuingia kwenye mjadala hapa kwenye kisima cha maarifa na kutushirikisha. Katika mjadala wa hapa sio lazima utumie jina lako unaweza kuweka jina lolote na kuweka ujumbe wako, kushiriki mjadala huo bonyeza maneno FORUM-MAJADILIANO
Kama unajiambia kwamba hiki ninachokushauri ufanye kwa wiki moja tu ni utoto au ushamba endelea kupoteza muda na maisha yako yaendelee kuwa magumu. Ukiweza kufanya zoezi hili utakuwa umetoka kwenye gereza la kwanza la matumizi mabovu ya muda wako.
Nakutakia kila la kheri katika safari hii nzuri ya kuboresha maisha yetu, KUMBUKA TUKO PAMOJA.