Wiki iliyopita tuliona jinsi ya kuweza kupata masaa mawili ya ziada kila siku. Masaa haya tuliyapata sio kwa miujiza bali kwa kubadilisha vipaumbele vyetu. Mara nyingi unajikuta unafanya mambo ambayo hayana msaada wowote kwako ila ndio umeyapa kipaumbele kikubwa.
Katika njia nyingi za kupata muda wa ziada kila siku kuna moja ya muhimu sana, kuamka mapema. Kwa wastani watu wengi huwa wanachelewa kulala, na kuchelewa huku hakutokani na jambo lenye umuhimu sana kwao bali kwa kuangalia tv na matumizi ya simu. Kwa kuchelewa kulala, moja kwa moja unachelewa kuamka na unapochelewa kuamka siku yako nzima unaipeleka kwa kasi sana kitu ambacho kinazidi kukuletea matatizo.
Anza kutengeneza tabia hii kwa kuamka dakika kumi au tano kabla ya muda wako uliozoea kuamka kila siku. Nenda ukiongeza muda wa dakika mbili au tano kila siku mpaka ufike wakati ambapo unaamka saa moja kabla ya muda wako uliozoea kuamka. Wakati huo huo jitahidi uwahi kulala angalau saa moja kabla ya muda uliozoea kulala.
Asubuhi na mapema ni muda ambao umetulia sana kuweza kufanya kazi zako zinazohitaji utulivu wa hali ya juu. Asubuhi na mapema ni wakati ambao hakuna usumbufu kutoka kwa watu au mawasiliano kwa sababu watu wengi wanakuwa wamelala. Ukiweza kupata angalau saa moja kila siku asubuhi kwa mwezi mmoja au miwili utajikuta utaona mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yako.
Nitumie muda huu wa ziada kufanya nini?
Najua hili ndio swali ambalo unajiuliza, baada ya yote haya nafanya nini na huu muda wa ziada nilioupata? Jibu ni rahisi sana, unakumbuka yale mambo mazuri unayoshauriwa kila siku kufanya ila unajishawishi kwamba huna muda? Mara nyingi umeshauriwa kujisomea, kufanya mazoezi, kupanga malengo na mipango ya maisha yako? Sasa umepata muda mzuri wa kufanya mambo hayo.
Katika saa moja ya ziada utakayoipata kwenye muda uliopangilia vizuri hasa ya asubuhi nakushauri ufanye mambo haya muhimu;
1. Pitia malengo ya maisha yako na pangilia siku yako.
Utakuwa unashangaza sana mpaka sasa kama bado huna malengo uliyoweka kwenye maisha yako. Na kuwa na malengo tu hakutoshi, bali unahitaji kuwa na mipango ua utekelezaji wa malengo yako. Tumia muda mchache kila siku asubuhi kupitia malengo yako uliyoandika. Ninaposema upitie namaanisha pia ujue ni kiasi gani cha hatua umepiga kwenye kila lengo ulilojiwekea. Kwa njia hii utajikuta unayakumbuka malengo yako na utaweza kuyafikia kwa urahisi. Kizuizi kikubwa cha watu kufikia malengo yao ni kuyasahau malengo yao. Kwa maelezo zaidi juu ya kuweka na kufikia malengo bonyeza hapa na usome makala zinazohusiana na kuweka malengo.
Pia muda huu wa asubuhi ni muda mzuri wa kuipangilia siku yako. Usianze siku yako kwa mazoea, panga unataka siku yako iweje na amua kuwa na siku yenye mafanikio. Kwa kufanya hivi utakuwa na siku yenye uzalishaji mkubwa na mafanikio makubwa, ila kama unaanza siku yako kwa mazoea utajikuta unaendesha na matukio yanayoendelea.
2. Fanya mazoezi.
Mazoezi ya viungo ni mazuri sana kwa afya yako ya mwili na hata afya ya akili. Kwa kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi kila siku asubuhi unajijengea afya imara, kujikinga na magonjwa na pia kuongeza uwezo wa kufikiri. Mazoezi ninayozungumzia sio lazima yawe makubwa sana ya kulipia fedha, hapana. Unaweza kufanya mazoezi kwa kukimbia kidogo au kutembea, unaweza kuruka kamba na pia unaweza kufanya push up. Usianze mpango wako wa mazoezi kwa kufanya kwa kiwango kikubwa, anza kidogo na endelea kuongeza kadiri muda unavyokwenda.
Unapofanya mazoezi kuna kemikali inayozalishwa kwenye ubungo ambayo inakufanya uwe umehamasika kufanya shughuli zako na pia inakusaidia kuwa na mawazo mazuri.
3. Jifunze kwa kujisomea.
Hapa ndipo ugomvi unapoanzia hasa kwa watanzania. Watu hawataki kabisa kujifunza mambo mapya yanayoweza kuwasaidia kwenye maisha yao, kuna watu wachache wanafaidika sana kwa watanzania wengi kutojielewa. Ukimwambia mtu jisomee kitabu na kitabu unampatia anakuambia hana muda wa kusoma, ana mambo mengi. Ila mtu huyo huyo yuko tayari kusoma magazeti ya udaku, kusoma habari za michezo, au hata kusoma matangazo mbalimbali ya biashara yaliyobandikwa barabarani. Kwa uaminifu kabisa naomba nikuambie kama unakosa muda wa kujisomea vitabu vizuri ila unapata muda wa kusoma mabango ya matangazo yaliyowekwa njiani huna maisha.
Hakuna kitu kizuri kama kujisomea. Kwa shughuli yoyote unayofanya iwe umeajiriwa, kujiajiri au kufanya biashara kuna mambo mengi sana ambayo huyajui. Ni kupitia vitabu na mtandao ndio unaweza kujifunza mbinu mbalimbali za kuboresha maisha yako na kuongeza ubora wa kazi zako
Huhitaji masaa matano kukaa na kusoma ndio ufaidike, unaweza kuanza na kusoma ukurasa mmoja wa kitabu kwa siku, ambayo itakuwa chini ya dakika mbili, baadae unaendelea kuongeza ukubwa mopaka ufikie kile kiwango ambacho ni kizuri kwako kujisomea kwa siku.
4. Pata muda maalumu wa kuwa na wewe.
Ni jambo la kushangaza sana kwamba unampa kila mtu muda wako ila hujawahi kujipa muda wewe mwenyewe. Hujajipa muda wa kutulia na kutofikiria chochote kingine, muda huu ni muda wa kusafisha mawazo yako na akili yako. Muda huu sio sawa na muda wa kupitia malengo yako, huu ni muda wa utulivu kwako binafsi na nafsi yako.
Katika muda huu tulia na jaribu kutofikiria jambo lolote zaidi ya muda huo hapo ulipo. Kuna takataka nyingi sana zinaingia kwenye mawazo yako kila siku, usipokuwa na njia ya kuziondoa utajikuta kadiri siku zinavyozidi kwenda mawazo yako yanabadilika na yanakuwa ya hovyo zaidi. Kitendo hiki cha kutulia bila ya kufikiria jambo lolote kinaitwa tajuhudi au kwa lugha ya kizungu MEDITATION. Wakati unafanya meditation, kaa sehemu isiyo ya kuegemea, simamisha mgongo wako, fumba macho yako na elekeza mawazo yako kwenye pumzi zako. Hesabu kila unapoingiza pumzi ndani na kutoa nje ya mwili, mwanzoni utaona ni zoezi gumu ila muda unavyokwenda utaanza kuona jinsi unavyoweza kuondoa mawazo mengi ambayo yanakuzuia wewe kufikia malengo yako.
5. Pata muda wa kupumzika.
Pamoja na kwamba unapoteza zaidi ya masaa matatu kwa siku kwa kutojua unachofanya kwenye masaa hayo, cha kushangaza hupati hata muda wa kupumzika. Kwenye huu ulimwengu ambao kuna kila aina ya kelele ni vigumu sana kupata mapumziko ya maana. Unatoka kwenye kazi zako unakimbilia kwenye mitandao ya kijamii, kuangalia tv au kufuatilia vitu vingine. Kwa tabia hii unajikuta unahamisha akili yako kutoka jambo moja na kwenda jingine na kufanya akili yako irukeruke kama chura.
Hata usingizi umekuwa hauna maana tena kwako, unaenda na simu kitandani, hivyo kabla hujalala unapoteza kama saa moja ya kuingia kwenye mitandao ya kijamii au kuwasiliana na watu mbalimbali. Kama hiyo haitoshi unalala huku umeiacha simu imewashwa hivyo kutoa ruhusa kwa mtu yeyote atakayeamua kukupigia simu saa nane za usiku aweze kukupata. Kama hufanyi kazi kwenye kitengo cha dharura, na tena uwe kwenye zamu, nakushauri zima simu yako au iweke kwenye muito wa kimya wakati wa kulala. Utapata faida kubwa sana tofauti na sasa ambapo umeamua kuiacha dunia iingilie mpaka usingizi wako.
Kupumzika ni muhimu sana kwa akili na mwili wako kwa sababu huwezi kufanya kazi kwa muda mrefu bila ya akili na mwili kuchoka. Unapoendelea kufanya kazi huku umechoka akili na mwili unajikuta unafanya makosa mengi na kushindwa kuwa makini.
Baadhi ya vitu tulivyozungumza hapa tutakuja kuvijadili kwenye kujenga tabia husika. Wakati huo tutajadili kwa kina zaidi kuhusiana na tabia inayohusiana na jambo hilo.
Zoezi la wiki hii.
Kwa wiki hii inayokuja fanya zoezi la kuamka mapema kabla ya muda wako wa kawaida kuamka. Anza na muda kidogo sana, dakika kumi tu. Kama umezoea kuamka saa kumi na moja asubuhi kesho amka saa kumi na dakika hamsini. Ili kuweza kuamka kwa muda uliopanga weka alarm na iweke mbali sana na kitanda kiasi kwamba itakulazimika kuamka ndio ukaizime.
Katika dakika hizi kumi zigawe kwenye dakika mbili mbili.
Dakika mbili za kwanza tafakari
Dakika mbili za pili fanya mazoezi, anza na push up kumi au ruka kamba mara kumi.
Dakika mbili za tatu pitia lengo lako moja na weka mpango wa jambo moja kuhimu utakalofanya siku hiyo.
Dakika mbili za nne soma kitabu kizuri, soma ukurasa mmoja tu.
Dakika mbili za tano fanya meditation kama tulivyojadili hapo juu.
Baada ya hapo endelea na ratiba zako za kawaida. Fanya hivi kila siku kwa wiki moja nzima, fanya kwa dakika hizo kumi tu kwa siku saba, usipunguze wala kuongeza. Baada ya wiki ndio unaweza kuanza kuongeza muda kidogo kidogo mpaka ufikie kiwango unachokiona ni bora kwako.
Cha msingi sana ni kutokupita siku hujafanya hivyo, utakuwa umejiondoa kwenye mstari wa kuelekea kwenye mafanikio. Kama umeanza kufikiria ni kitu cha ajabu nachokushauri ufanye tafakari mara mbili maana itakuwa vigumu sana kwako kufikia mafanikio unayotazamia kama utashindwa kufuata misingi hii kirahisi.
Fanya haya kwa wiki moja na kila siku tushirikishane changamoto na mafanikio tuliyofikia kwenye zoezi hili kwa kuandika hapa kwenye FORUM-MAJADILIANO ndani ya kisima cha maarifa, tafadhali sana usiache kutushirikisha kwenye majadiliano. Bonyeza hilo neno FORUM-MAJADILIANO ili kuweza kutushirikisha unayokutana nayo kila siku katika kufanya zoezi hili.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kuboresha maisha yako.
Kumbuka TUKO PAMOJA kwenye safari hii.