Msomaji wa muda mrefu wa AMKA MTANZANIA, Anna Mpululu alinishirikisha muhtasari wa kitabu kinachoitwa THE GREATEST SALESMAN IN THE WORLD. Muhtasari huu umeelezea kwa kifupi sana sheria kumi za mafanikio ambazo mtu yeyote mwenye kiu ya mafanikio anatakiwa kuzifuata kila siku.
Kitabu The Greatest Salesman In The World kilichoandikwa na Og Mandino ni kitabu kilichojaa busara nyingi sana kuhusu mafanikio kwenye kuuza(sales) na hata mafanikio kwenye jambo lolote mtu analofanya. Kitabu hiki nilikisoma mwaka jana na kimekuwa nguzo kubwa sana kwangu kufikia mafanikio ambayo sikuwahi kufikiri kama ningeweza kuyafikia.
Leo nakupa muhtasari wa kitabu hiki ambao tumeshirikishwa na Anna Mpululu na nakushauri uusome kila siku kabla hujaanza siku yako. Muhtasari huu umeelezea sheria kumi za kuishi nazo kila siku kwa kifupi sana. Una kurasa nne na hivyo itakuchukua dakika tano tu kuusoma kila siku lakini thamani utakayoipata ni kubwa mno.
Kwa kifupi naomba nizitaje sheria zilizozungumziwa kwenye muhtasari huu, kwa maelezo ya kila sheria tafadhali soma muhtasari ambao nakutumia.
1. Kushindwa hakutonishinda kama hamu yangu ya kufanikiwa ni dhabiti.
2. Nitajenga tabia nzuri na kuwa mtumwa wa tabia hizo.
3. Nitaisalimu siku ya leo kwa upendo kutoka moyoni.
4. Nitang’ang’ana mpaka nifanikiwe.
5. Nitaongeza ujuzi wangu wa dunia na yale ninayofanya.
6. Nitaishi siku ya leo kama vile ndio siku yangu ya mwisho.
7. Leo nitakuwa msimamizi wa hisia zangu.
8. Nitacheka na kufurahi.
9. Leo nitaongeza thamani yangu kwa mamia.
10. Nitatenda sasa.
Mwisho anamalizia na sala muhimu ya mafanikio unayotakiwa kuisema kila siku.
Kwa kifupi hizo ndio sheria zilizopo kwenye muhtasari huu ambazo ni vizuri sana kuzisema na kuziishi kila siku. Kwenye muhtasari wametoa maelezo kidogo ya jinsi gani unaweza kutekeleza sheria husika.
Nakusihi tena hata kama hujawahi kusoma kitabu chochote kwenye maisha yako soma huu muhtasari wa kurasa nne kila siku na utekeleze yale unayoyasoma utaona mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.
Kupata muhtasari huu BONYEZA MAANDISHI HAYA na utaanza kudownload.
Nakutakia kila la kheri kwenye harakati za kuelekea kwenye mafanikio.
Tuko pamoja.