Karibu sana msomaji kwenye kipengele cha TABIA ZA MAFANIKIO ambapo tunashauriana jinsi ya kujenga tabia za kutusaidia kufikia mafanikio tunayotazamia. Kila mwezi tunajadili tabia moja muhimu ya kufikia mafanikio. Mwezi huu wa saba tunazungumzia fedha, upatikanaji wake na jinsi ya kuzitunza. Kutokana na umuhimu na upana wa somo hili tutajadili kwa miezi miwili badala ya mwezi mmoja kama ilivyo kwenye tabia nyingine.

Kabla hatujaanza naomba unijibu swali moja.

Fedha ni nini?

A/. Sabuni ya roho

B/. Maua

C/. Mwana haramu

D/. Shetani.

Jibu lako ni nini hapo juu? Inawezekana ukawa na jibu moja au jibu zaidi ya moja. Unaweza ukasema jibu ni A leo lakini mwaka ujao nikikuuliza swali hili ukasema jibu ni C.

Nimeuliza swali hilo kwa sababu kuu mbili; kwanza hatuna maana moja ya fedha na pili tuna mtizamo mbaya sana kuhusu fedha. Vitu hivi viwili vimefanya tuone fedha ndio chanzo cha matatizo yote. Sio kweli kwamba fedha ndio chanzo cha matatizo, bali sisi wenyewe ndio chanzo cha matatizo linapokuja swala la fedha.

Unapokuwa huna fedha na unafanya kazi kwa nguvu sana ili uzipate ukiulizwa fedha ni nini utasema fedha ni mwanaharamu. Hii ni kwa sababu inakubidi utoke jasho kuipata lakini bado unayoipata haikutoshi. Ikitokea umepata fedha za kutosha mahitaji yako na nyingine zikabaki ukiulizwa fedha ni nini utasema fedha ni sabuni ya roho. Kwa maelezo haya utashawishika kutumia hovyo kwa sababu unaamini inasafisha roho yako. Ukitumia hovyo zikaisha haraka ukiulizwa fedha ni nini utajibu fedha ni maua kwa sababu zinakuja na kupotea kama maua yanavyochanua na kunyauka. Na ikitokea ukafanya mambo mabaya kutokana na fedha ulizonazo ukiulizwa fedha ni nini utasema fedha ni shetani. Inakuwaje fedha hii moja inakuwa na maana nyingi na tofauti kwa mtu mmoja? Kuna tatizo kubwa hapa ambalo bado hujalijua vizuri.

Mtazamo mbaya juu ya fedha.

Kinachosababisha kuwe na maana nyingi za fedha ni mtazamo wako linapokuja swala la fedha. Watu wengi sana wana mtizamo hasi ambao unawazuia kutengeneza fedha za kutosha na pia kushindwa kuzitunza fedha zao. Mtazamo huo hasi tumejengewa kwenye familia zetu na jamii zetu na tumekuwa tunaimbiwa kila siku mpaka imeshakuwa sehemu ya maisha yetu.

Unaweza kuwa unajiuliza sana kwa nini hufikii mafanikio ya kifedha unayotarajia licha ya kujaribu njia mbalimbali. Unashindwa kufanikiwa kwa sababu ya mtizamo wako hasi ulionao kuhusu fedha.

Tuchukulie mfano wa wafanyakazi. Katika kampuni au taasisi moja kunakuwa na wafanyakazi wa ngazi tofauti na wote wana mishahara tofauti. Kunakuwa na mfanyakazi anayelipwa labda shilingi laki mbili kwa mwezi na kuna mwingine analipwa laki tano, mwingine nane na hata mwingine anaweza kuwa analipwa shilingi milioni moja kwa mwezi. Je inapofika mwisho wa mwezi nani anayekuwa ameishiwa zaidi? Anayelipwa laki mbili au milioni moja? Kwa hali ya kawaida wote wanakuwa wameishiwa sawa. Ni kitu gani hasa kinasababisha watu wawili wenye mishahara miwili tofauti kabisa mwisho wa mwezi wanakuwa wameishiwa sawa sawa?

Mara kwa mara makampuni au taasisi zimekuwa zikiongeza mishahara(hata kama ni kidogo), je ni mabadiliko gani makubwa yanayotokea kwa mfanyakazi anayeongezewa mshahara? Mara nyingi matatizo ndio yanazidi.

Kutokana na mtazamo wetu mbaya kuhusu fedha, tunajikuta hata tukipata kiasi gani cha fedha bado hakiwezi kututosheleza. Kwa mtazamo mmbaya ambao umezaa tabia mbaya ya matumizi yako ya fedha, kila unapoongeza kipato na matumizi nayo yanaongezeka. Hii ndio sababu kubwa ninayosema kwamba tatizo sio fedha bali tatizo ni wewe binafsi linapokuja swala la fedha.

Unaitawala fedha au fedha inakutawala?

Kama wewe ni muumini wa dini nina hakika ulishakutana na usemi huu, UMEUBWA KUTAWALA DUNIA NA VYOTE VILIVYOMO. Sasa naomba unijibu swali moja ni kipi ambacho unakitawala? Tuanze na fedha ambayo unaitumia kila siku kwenye maisha yako, je unaitawala fedha au fedha inakutawala?

Umeitawala fedha pale ambapo;

1. Unakwenda kufanya kazi au biashara ili kutoa huduma kwa watu wengine ambao wanazihitaji, hivyo lengo lako kuu sio kupata tu fedha bali pia kuwasaidia wengine.

2. Hufanyi matumizi ya fedha kwa sababu tu unazo ila kwa vile una mpango wa matumizi hayo.

3. Unaweza kuitunza fedha uliyopata na kuifanya ikuzalishie zaidi.

Fedha imekutawala pale ambapo;

1. Unakwenda kufanya kazi au biashara kwa sababu unataka kupata fedha, hujali kama huduma unayotoa ina msaada kwa wengine au la.

2. Unatumia fedha kwa sababu unazo, hivyo kila unapopata ya ziada matumizi yako nayo yanaongezeka.

3. Unaishi kipato kwa kipato, kama umeajiriwa unaishi mshahara kwa mshahara na mara nyingi mishahara haikutani. Kama umejiajiri au unafanya biashara unatumia kile ambacho umekipata ndani ya siku hiyo ya biashara.

Kama umetawaliwa na fedha hata ungepewa fedha kiasi gani bado itakuwa vigumu sana kwako kuweza kuwa na uhuru wa kifedha. Kama umeitawala fedha huwezi kuteseka kwa sababu unajua unaipataje, unaitumiaje na unaitunzaje ili kuweza kufikia mafanikio makubwa.

LEO UMEJIFUNZA NINI?

Katika yote haya niliyoeleza hapa nataka uondoke na kitu kimoja ambacho utaanza kukitumia kwenye maisha yako sasa ambacho kitabadili mtazamo wako kuhusu fedha na kuweza kuwa na uhuru wa kifedha.

1. Jua fedha ni nini. Kwa mfano kwangu mimi, fedha ni bidhaa ya mabadilishano na thamani ya kitu au huduma.

2. Jua hakuna kikomo cha wewe kupata fedha ikiwa unatoa bidhaa au huduma yenye thamani ya kulipiwa na inayoweza kusaidia maisha ya wengine.

3. Jua kuwa na uhuru wa kifedha sio dhambi au tamaa ni haki yako na ni kitu ambacho unaweza kukipanga.

4. Jua matumizi ya fedha ni muhimu ukaweza kuyadhibiti. Usitumie tu fedha kwa sababu unazo, zitumie kwa sababu una mahitaji ya msingi ya kuzitumia.

5. Kama unaishi kipato kwa kipato wewe ni mtumwa mkubwa wa fedha na unahitaji ukombozi wa haraka sana.

Kuanzia leo badili kabisa mtizamo wako juu ya fedha, acha kuona kwamba kuna uhaba wa fedha, achana na kauli kwamba fedha haiwezi kununua furaha au fedha ni mwanaharamu na tengeneza uhuru wako wa kifedha.

ZOEZI LA WIKI.

Wiki hii nakuomba sana usome kitabu Choose to Be Wealthy, 8 Habits of the Happy Millionaire kilichoandikwa na Bo Sanchez. Kitabu hiki kimeeleza tabia nane za kuweza kujenga ili kuwa na uhuru wa kifedha na kuwa na furaha pia. Katika kitabu hiki utajifunza vitu vingi sana kuanzia kubadili mtazamo wako kuhusu fedha na jinsi ya kutunza fedha zako na kuzizalisha zaidi ili uweze kuwa na uhuru wa kifedha. Kitabu hiki kimeondoa ile dhana kwamba kuwa tajiri sana ni dhambi au kinyume na mafundisho ya dini.

Nakuomba hata kama kuna kitabu hujamalizia kusoma, kiache na usome kwanza kitabu hiki mara moja. Ni kitabu kifupi sana na kimeandikwa kwa mfumo rahisi wa kusoma kwani kina vipengele vidogo vidogo na haikwezi kukuchosha kusoma. Nilikisoma kitabu hiki mara mbili tu nikakimaliza kwa sababu nilikuwa siwezi kukiacha kwa uzuri wa mafundisho yake na uzuri wa mpangilio wake.

Pia karibu kwenye FORUM-MAJADILIANO ili tuweze kujadili yale ambayo tumejifunza hapa na kwenye kitabu tunachoendelea kusoma.

Nakutakia kila la kheri kwenye safari yako ya mafanikio na kuwa na uhuru wa kifedha.

TUKO PAMOJA.