Huu ndio wakati ambao vyuo vya elimu ya juu na vyuo vingine vya elimu Tanzania vinaelekea kwenye mwisho wa mwaka wa masomo. Kuna vyuo vingine tayari mwaka wa masomo umeshakwisha wakati wengine bado wanafanya mitihani.
Kila mwaka wakati kama huu kuna wanafunzi ambao wanahitimu masomo yao kwa ngazi mbali mbali. Kuna ambao wanahitimu kwa ngazi ya cheti, wengine ngazi ya stashahada, shahada na sahahada za uzamili mpaka uzamivu.
Kama nilivyoahidi kwa miezi miwili, mwezi huu wa saba na mwezi wa nane kila siku ya jumatano nitakuwa naweka makala moja kwenye AMKA MTANZANIA yenye ushauri wa kina kwa wahitimu ambao ndio wanaingia mtaani. Jumatano ya leo tunaanza na pongezi. Kama wewe unahitimu au unamfahamu anayehitimu tafadhali mshauri awe anasoma makala hizi, atajifunza kitu hata kama ni kidogo. Kwa kuzisoma tu anaweza kupata picha ya tofauti na kuweza kujua maisha yake yanaelekea wapi.
Unastahili pongezi.
Kwa ngazi yoyote ile ya elimu uliyohitimu unastahili pongezi kubwa sana kwa sababu kazi uliyoifanya sio kazi ndogo. Tukichukua kwa waliomaliza kwa ngazi ya stashahada au shahada utakuta wametumia zaidi ya miaka kumi na tano kwenye mfumo wa elimu. Darasa la awali mwaka mmoja, shule ya msingi miaka saba, shule ya sekondari miaka sita na chuo miaka miwili, mitatu mpaka mitano.
Miaka kumi na saba uliyokaa darasani sio haba, ni kazi kubwa sana umefanya na pia umekuwa na uvumilivu mkubwa sana mpaka kufikia hatua hii. Kuna wengine wengi waliishia njiani ila wewe uliendelea kupambana. Ulikutana na vikwazo mbalimbali vilivyotishia safari yako lakini hukukata tamaa. Hongera sana, tena sana.
Umedanganywa.
Pamoja na kazi kubwa uliyofanya ya kusoma kwa juhudi kubwa, kuna kitu kimoja mpaka sasa huenda hujakijua, UMEDANGANYWA. Nasema umedanganywa kwa sababu vitu ambavyo umekuwa unahubiriwa kwa miaka hiyo kumi na saba ni kwamba havifanyi tena kazi au havipo na vimeshapitwa na wakati.
Familia yako na jamii kwa ujumla ilikuwa na wakati mzuri sana wa kukupa ushauri kwamba soma kwa bidii, faulu vizuri na utapata kazi nzuri na kuwa na mafanikio. Walimu waliokufundisha kila ngazi walikuwa wanakuimbia wimbo huo huo kila mwaka na ulipofika chuoni mwalimu alikuwa anakuambia ukifika kazini utafanya hivi na hivi.
Watakuwa wamekupa hadithi nzuri sana za watu waliosoma na wakawa na mafanikio makubwa. Na pia watakuwa wamekupa hadithi nzuri sana za watu ambao walikataa kusoma na maisha yao yakawa mabovu. Tatizo ni kwamba walikuwa wanasisitiza hapo tu na hawakuongelea upande mwingine ambao una watu wengi zaidi ya hao waliowataja. Kuna watu wengi waliosoma ila maisha yao ni magumu sana na kuna watu wengi ambao hawajasoma sana ila maisha yao ni ya mafanikio.
Umedanganywa kwa sababu ulimwengu wa kazi nzuri zenye kuleta mafanikio uliokuwa unahubiriwa kwa sasa umeshapotea. Kama huniamini siku chache zijazo utalishuhudia hili kwa uchungu sana.
Mmedanganyana.
Licha ya kudanganywa, wewe na wenzako hamkuwa nyuma kwenye kudanganyana. Kuna hadithi nzuri sana huwa zinazunguka kwenye karibu kila chuo Tanzania hii. “Nikimaliza chuo nitapata kazi kwenye shirika au taasisi fulani nitakuwa nalipwa laki saba yangu, nitakopa gari na kupanga nyumba sehemu fulani”. Hongera kwa ndoto nzuri, tatizo hiko unachokiota rafiki hakipo kabisa, yaani nafasi hiyo ni finyu sana.
Mliendelea kudanganyana kwa kuangalia watu wachache waliowaacha chuoni ambao mambo yao yamekuwa mazuri. “Umemuona John, amemaliza kozi hii niliyosoma mwaka juzi na sasa ameajiriwa kwenye kampuni kubwa na analipwa vizuri sana, tayari ana gari na nyumba.” Asante sana kwa kuwamfuatiliaji mzuri wa waliokutangulia, lakini tatizo ni moja hapa, mbona unawafuatilia wachache sana ambao ndio wamefikia viwango hivyo ulivyotaja hapo. Vipi kuhusu darasa zima la John, unakumbuka wale wenzake zaidi ya elfu moja waliosoma kozi hiyo wako wapi? Vipi kuhusu waliomaliza kozi hiyo na nyingine nyingi kwenye vyuo vingine? Wako wapi? Ni vyema ukaacha kuangalia wachache sana waliofikia mafanikio na kuangalia pande zote ili kupata ukweli halisi wa mtaani.
Kuna vitu vingi sana ambavyo umedanganywa na wewe ulikuwa unadanganyana na wenzako. Sasa unapata nafasi ya kuingia mtaani kwenda kuona uhalisia wa mambo, sitaki kukutisha kwamba mambo yatakuwa magumu. Nachoweza kukuambia ni kwamba NENDA MTAANI UKAJIFUNZE UPYA MAANA YA MAFANIKIO.
Kama ukiweza kutengeneza maana mpya ya mafanikio utaishi maisha yenye mafanikio na utakayoyafurahia. Kama utasubiri jamii ikupe maana yake ya mafanikio utaishi maisha ya mbio za panya mpaka muda wako wa kuishi utakapokwisha.
Mambo machache ambayo nataka uondoke nayo hapa leo;
1. Maisha uliyokuwa ukihadithiwa wakati uko chuo yana tofauti sana na yale ambayo utakwenda kukutana nayo mtaani.
2. Kuna wenzako wengi wapo mtaani waliomaliza mwaka jana, mwaka juzi na hata miaka mingine.
3. Huu ndio wakati wa kutengeneza mafanikio yako na kuchukua hatua juu ya maisha yako.
Kwa kumaliza naomba nikupe mambo mawili ya kufanya. Naomba uchukue muda wako kidogo kusoma na kurudia kusoma tena makala hizi mbili;
1. Kabla hujaanza kuzunguka na bahasha soma hapa.
2. Barua ya wazi kwa wahitimu ambao bado wanatafuta ajira.
Soma makala hizo mbili mara nyingi uwezavyo na utaanza kupata mwanga wa nini kinaendelea mtaani.
Nakusuhi pia ujinge na KISIMA CHA MAARIFA ambapo utajifunza vitu vingi sana ikiwemo kutengeneza tabia za mafanikio.
Kwa msomaji yeyote mwenye ushauri kwa wenzetu ambao wamehitimu masomo naomba aniandikie ili tuweze kuwashirikisha wengine. Kumbuka hapa tunasaidiana mbinu mbalimbali za kuboresha maisha yetu ili tuweze kuendelea kama taifa. Hivyo kama kuna mbinu ulizotumia wewe ulipotoka chuoni na ukaweza kufanikiwa naomba uniandikie kwenye email amakirita@gmail.com hata kama wewe sio muandishi mzuri nitakusaidia kupangilia mawazo yako vizuri.
Ombi la mwisho kama wewe ni mhitimu au hata kama sio mhitimu Tafadhali peleka ujumbe huu kwa watu wengi uwezavyo ili uweze kuwasaidia wengi.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kuboresha maisha yako.
TUKO PAMOJA.