Kama umefanya zoezi la wiki iliyopita mpaka sasa utakuwa unajua ni wapi fedha zako zinatoka na muhimu zaidi ni wapi fedha zako zinakwenda. Kama ulikuwa mwaminifu kwenye kuandika vizuri mapato na matumizi yako utakuwa umeanza kupata picha ni kiasi gani cha fedha unapoteza kila siku.

Kama hukupata nafasi ya kufanya zoezi lile nakusihi ulifanye kwanza kabla ya kuendelea hapa. Unawezakulifanya kwa kusoma makala hii; Fedha; zinatoka wapi na zinakwenda wapi? Ukishafanya zoezi hili ndio tunaweza kwenda vizuri kwenye zoezi muhimu tutakalofanya wiki hii.

Wiki hii tutaangalia jinsi ya kujenga tabia ya kujiwekea akiba ambayo ndio hatua muhimu na ya kwanza kabisa ili kufikia uhuru wa kifedha. Kwa kazi yoyote unayofanya, iwe umeajiriwa au umejiajiri huna ujanja, ni muhimu sana kuanza kujiwekea akiba kama unataka kuwa na uhuru wa kifedha na kusahau matatizo ya kifedha yanayokuzonga sasa.

Nitaanzaje kuweka akiba wakati kipato changu ni kidogo?

Najua pingamizi lako la kwanza ni kwamba siwezi kuweka akiba sasa hivi kwa sababu kipato changu ni kidogo. Nitaanza kuweka akiba kipato changu kikiongezeka. Naweza kukubaliana na wewe kwamba kipato chako ni kidogo ila napingana na wewe kwamba huwezi kuanza kuweka akiba kwa sababu hiyo. Katika kipato hiko hiko kidogo ndio unatakiwa uanze kujifunza kuweka akiba. Kama unashindwa kuweka akiba kwenye kipato kidogo basi hata kikiwa kikubwa hutaweza kuweka akiba.

Kuweka akiba ni tabia na sio kipato.

Unaweza kujisingizia kwamba kwa sasa huweki akiba kwa sababu kipato hcko ni kidogo, ila sio kweli. Huweki akiba kwa sababu huna tabia hiyo ya kuweka akiba. Labda nikupe mfano mmoja ambao utanielewa vizuri;

Kwa mtu yeyote ambaye anafanya kazi ya kuajiriwa hata mshahara uwe mdogo kiasi gani huwa una makato, si ndio? Yaani kwa mfano mtu ameajiriwa na akaambiwa mshahara wake ni shilingi laki mbili, mwisho wa mwezi huwa hapokei hiyo laki mbili kwa sababu kuna makato yanafanywa hapo na hivyo kupokea fedha chini ya hapo. Kama umewahi kufanya kazi au unamjua mtu anayefanya kazi utakuwa umenielewa kwenye hili. Sasa swali langu kubwa ni je umewahi kusikia mtu amekufa kwa sababu ya makato ya kwenye mshahara? Kwa upande wangu sijawahi kusikia, kitu ambacho kinanifanya niamini kwamba tunaweza kutumia sheria hii hii ya makato kujenga tabia ya kuweka akiba.

Anza kuweka sehemu kidogo ya kipato chako kama akiba.

Jiwekee utaratibu kwamba sehemu fulani ya mapato yako itakwenda kwenye akiba. Kwa mfano unaweza kuanza na asilimia kumi ya kipato chako. Kila unapopata kipato chako weka pembeni asilimia kumi kama akiba. Kama kipato chako ni shilingi laki moja basi shilingi elfu kumi inakwenda pembeni moja kwa moja. Ukiweza kujenga tabia hii muhimu utajikuta baada ya muda una kiasi kikubwa cha fedha uliyoweka akiba.

TAHADHARI; Ukishaweka kiasi hiki akiba kisahau kabisa kwenye matumizi yako. Yaani usije ukafikiri hata mara moja kwamba utakapokosa fedha ya matumizi utatumia fedha hii, hapana hii ina kazi muhimu sana ambayo tutaiona baadae. Ukishaweka fedha hii isahau kama vile ulienda dukani na kununua nguo au ulinunua chakula na hivyo huwezi kwenda kuidai tena.

CHANGAMOTO; Kama kipato chako ni kidogo kwamba ukiondoa asilimia kumi basi huwezi kuishi kwenye asilimia tisini iliyobaki basi hata ungetumia hiyo asilimia mia moja bado haitakutosheleza. Hivyo badala ya kuacha kuweka akiba nakushauri uangalie jinsi ya kuongeza kipato chako. Asilimia kumi ya mapato yako ni malipo yako halali ambayo hayatakiwi kwenda kwenye matumizi mengine yoyote.

Mgawanyo mzuri wa mapato yako.

Katika kipato chochote unachopata kuna mgawanyo mzuri sana mabao kama ukiweza kuutumia utakuwa na mlinganyo mzuri kwenye maisha yako. Kigawe kipato chako katika mafungu manne;

1. Asilimia 70 kwenye matumizi yako ya kawaida na kila siku.

2. Asilimia 10 sadaka au misaada kwa watu wanaohitaji kusaidiwa.

3. Asilimia 10 akiba yako binafsi, hii ndio umejilipa wewe.

4. Asilimia 10 uwekezaji, hii unawekeza ili ziendelee kuzaliana zaidi.

Tutajadili zaidi mgawanyo huu kwenye makala ya wiki ijayo.

Kosa kubwa unalofanya na utakalofanya katika kuweka akiba.

Huenda umeshajifunza sana kuhusu kuweka akiba na kuanza na asilimia kumi. Ila kila unapojaribu kuweka akiba kwa mpango huu unashindwa kwa sababu fedha inakuwa imekwisha kutokana na matumizi.

Unashindwa kwa sababu unafanya kosa moja kubwa sana ambalo unatakiwa uache kabisa kulifanya kwanzia leo kama unataka kupata uhuru wa kifedha. Kuna njia mbili za kuweza kufikia kwenye kuweka akiba.

1. Njia ya kwanza ni kupokea kipato chako, kufanya matumizi yako yote halafu fedha itakayobaki uweke akiba.

2. Njia ya pili ni kupokea kipato chako, kuweka akiba kwanza na inayobaki ndio unaweka kwenye matumizi.

Kama unatumia njia ya kwanza kila siku utashindwa kujiwekea akiba kwa sababu kama tunavyojua matumizi huwa hayana mwisho. Kadiri fedha inavyokuwepo ndipo matumizi nayo yanaongezeka.

Ukitumia njia ya pili wala hutaumiza kishwa wakati wa kuweka akiba. Kwa sababu unajua fedha hii niliyopokea kiasi fulani kinakwenda kwenye akiba bila hata ja kujadiliana na nafsi yako. Tumia nia hii kufikia uhuru wako wa kifedha.

ZOEZI LA WIKI.

Wiki hii naomba tusome kitabu THE RICHEST MAN IN BABYLON, kukipata bonyeza maandishi hayo ya kitabu. Kitabu hiki pia unaweza kukipata kwenye maduka ya vitabu au hata wauzaji wengine wa vitabu. Pia kitabu hiki kimetafsiriwa kwa kiswahili na kinaitwa MTU TAJIRI WA BABELI, unaweza kukipata kwa wauza kitabu.

Hiki ni kitabu kizuri na muhimu sana kukisoma kama unataka kujenga tabia ambazo zitakupeleka kwenye uhuru wa kifedha. Kitabu hiki kinaeleza jinsi mtu anavyoweza kutoka kwenye umasikini na madeni na kuwez akuwa na uhuru wa kifedha na kuw atajiri mkubwa.

Kitabu hiki ni kifupi sana na unaweza kukisoma na kumaliza ndani ya masaa mawili. Nimewahi kukituma kitabu hiki kwa wasomaji wengi ila sasa nakituma tena na hata kama uliwahi kukisoma nakusihi ukisome tena. Kuna vitu vizuri utakavyovipata kwa kurudia kusoma.

Wakati unaendelea kusoma ktabu hiki tunaweza kuendelea kukichambua kwenye forum yetu ya FORUM-MAJADILIANO ili kushirikishana yale tukiyojifunza.

Nakutakia kila la kheri kwenye safari yako ya uhuru wa kifedha.

TUKO PAMOJA.