Habari za leo ndugu msomaji wa AMKA MTANZANIA, karibu tena kwenye sehemu yetu ya ushauri kwa wahitimu ambapo tunashauriana mambo muhimu kwenye maisha ambayo mhitimu wa elimu au mtu mwingine yeyote anaweza kuyatumia na kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yake.

Kama wiki iliyopita tulikuwa pamoja naamini nimeshakutumia vitabu na umeanza kuvisoma. Na kama una uchu kweli wa kufikia mafanikio utakuwa umeshamaliza kuvisoma! Usistuke sana, kama hujamaliza kuvisoma vimalize mapema na baada ya kumaliza kuvisoma andika vitu vyote ambavyo umejifunza katika vitabu hivyo na jinsi gani unaweza kuvitumia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Baada ya hapo anza kazi na piga kazi kweli kweli, maneno maneno au ujanja ujanja weka pembeni.

Kama kwa sababu zozote zile hukupata nafasi ya kusoma makala ya wiki iliyopita na hivyo kushindwa kupata vitabu basi isome kwa kubonyeza; Wahitimu; kujifunza ndio kumeanza rasmi.

Leo tutazungumzia jambo muhimu sana ambalo hujawahi kupata nafasi ya kufundishwa popote. Licha ya kukosa nafasi hiyo ya kufundishwa, wewe mwenyewe hujawahi kuchukua hatua ya kujifunza jambo hili muhimu sana kwenye maisha yako.

Leo tutajifunza kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii. Hatuzungumzii jinsi ya kujiunga na mtandao fulani wa kijamii au jinsi gani ya kuweka picha nzuri, hapana, hapa tutajadili jinsi matumizi ya mitandao hii yanavyoweza kuwa na mchango mkubwa kwenye mafanikio au kushindwa kwako.

mitandao kijamii

Mitandao ya kijamii ni kitu kizuri sana kuwahi kutokea duniani na uzuri ni kwamba imegundulika kwenye zama za hivi karibuni. Tunaweza kujivunia kwamba sisi ndio kizazi kilichogundua na kukuza mitandao hii ya kijamii kwa sababu karibu yote imeanzishwa na kukua ndani ya miaka kumi iliyopita.

Kuja kwa mitandao ya kijamii kumebadili kabisa mfumo wa mawasiliano baina ya watu. Mitandao hii imerahisisha sana mawasiliano na imewezesha watu wengi kutengeneza fedha kupitia biashara mbalimbali. Tuna bahati kubwa sana kuwa kwenye kizazi hiki cha mitandao ya kijamii.

Pamoja na uzuri huu wa mitandao ya kijamii, kama ilivyo kwa kitu chochote, kila penye faida pia kuna hasara. Kutokana na mapenzi yako makubwa kwenye mitandao hii unaweza usione hasara zake moja kwa moja. Ila nikudokezee leo kwamba matumizi yako ya mitandao hii yanaweza kuwa na hasara kubwa sana kwenye maisha yako kuliko faida unayopata.

Hapa tutajadili mambo matano muhimu ya kuzingatia kwenye mitandao hii ili iweze kuwa baraka badala ya kuwa laana kwenye maisha yetu.

1. Angalia sana yale ambayo unayaweka kwenye mitandao ya kijamii.

Mitandao hii imekuwa na uwezo mkubwa sana wa kutushawishi tushirikishe wengine kile tunachofanya au kuwaza. Kwa mfano ukiingia tu facebook wanakuuliza what’s on your mind(nini kipo kwenye akili yako), kisaikolojia wanakushawishi uweke pale chochote kinachokuja kwenye akili yako. Kuwa makini sana usiingie kwenye mtego huu, baadhi ya vitu utakavyoandika vinaweza kukunyima fursa unazotazamia. Kama kuna jambo ambalo usingeweza kulizungumza kama ungepewa nafasi ya kuhutubia dunia nzima basi usiliweke kwenye mitandao yako ya kijamii, ni hivyo tu. Kila unachoandika kwenye mitandao hii kinaonekana dunia nzima.

2. Usiwe na taswira mbili.

Jinsi ambavyo unataka uonekane kwenye jamii basi hakikisha kunaendena na na jinsi unavyoonekana kwenye mitandao ya kijamii. Kama kwenye wasifu wako(cv, resume) umeandika wewe ni kiongozi, mwaminifu na mchapa kazi basi ni vyema yale unayoandika kwenye mitandao ya kijamii yaendane na sifa hizo. Sasa kama utakuja kutuwekea kwenye mitandao ya kijamii matatizo yako ya kimapenzi au jinsi gani unashindwa kuamka asubuhi, tunajua ya kwamba huna sifa za uongozi kwa sababu umeshindwa kutatua matatizo yako na sio mchapa kazi kwa sababu kuamka kwako tu ni shida.

Mbaya zaidi ni kwamba siku hizi waajiri wanaangalia mitandao hii kumjua mtu wanayekwenda kumuajiri. Hivyo unaweza kuwa na cv nzuri yenye sifa za kutosha ila wakikutafuta kwenye mitandao ya kijamii wanakuona kama mtu mwingine, na hivyo wanashindwa kukuamini na kukuajiri.

Na sio waajiri tu wanaotumia taswira yako ya kwenye mitandao, mtu yeyote ambaye unataka kufanya naye jambo la msingi atakuangalia kwenye mitandao hii. Naomba nikiri hata mimi mtu yeyote anayependekeza tufanye jambo fulani kwa pamoja, huwa namuangalia kwanza kwenye mitandao ya kijamii anaandika vitu vya aina gani, na hii imekuwa ikiniwezesha kujua kama jambo tunalotaka kufanya tutafanikiwa au la.

3. Usipoteze muda wako kwenye mitandao hii.

Tatizo jingine kubwa la mitandao ya kijamii ni unyonyaji wa muda. Naweza kusema mitandao hii inanyonya muda zaidi ya kitu kingine chochote duniani. Unaweza kuingia kuchungulia kidogo ila ukajikuta nusu saa inaisha huku ukiendelea kushuka tu. Na ubaya zaidi ni kwamba mambo mengi unayoangalia hayana faida kubwa kwenye maisha yako.

Punguza nusu ya muda unaotumia kwenye mitandao hii, ukiweza kufanya hivi pia utapunguza mambo unayoweka ambayo yatakuharibia wasifu wako. Muda wako ni wa thamani sana kishinda kufuatilia nani kala bata wapi, au nani kapendana na nani. Weka kipaumbele kwenye maisha yako na ingia huku kuchungulia tu ni kitu gani kinaendelea duniani.

4. Chagua mitandao utakayokuwepo.

Kama upo facebook, twitter, instagram, linkedin, google+, pinterest na wakati huo huo unatumia whatsapp, bbm, viber na telegram basi huna maisha. Ndio namaanisha huna maisha kwa sababu unaweza kupata wapi muda wa kuingia kwenye mitandao yote hiyo? Hapo bado hujaweka simu za kawaida na meseji za kawaida.

Chagua mitandao mishache ambayo utapenda kuwa unaitumia kwenye muda kidogo utakaopata. Facebook ndio maarufu sana, hivyo unaweza kuwa mmoja wapo kwa sababu utakutana na watu wengi. Nakushauri kama upo makini na unataka kukutana na watu wenye taaluma mbalimbali tumia sana linked in na weka vitu vitakavyoonesha umakini wako. Katika mitandao ya kijamii ambapo unaweza kufaidika kwa kiasi kikubwa basi ni linked in.

Kama huna biashara yoyote ambayo unaifanya kwa njia ya mtandao, mitandao miwili kwa mfano facebook na linked in inakutosha kabisa, huko twitter na instagram unapoteza tu muda wako. Unaweza kufuta akaunti zako leo hii na utajishukuru sana baadae kwa hatua hiyo ya kushujaa uliyochukua leo.

Vile vile kwenye mitandao hii ya kutumiana ujumbe kama whatsapp, bbm, viber n.k chagua mmoja utakaokuwepo, kama whatsapp na pia punguza muda unaotumia huko kutumiana jumbe ambazo hazina faida yoyote kwenye maisha yako.

5. Tafuta jina lako GOOGLE(JIGUGO)

Nenda www.google.com sasa hivi halafu weka jina lako na utafute. Utaletewa taarifa na picha zote ambazo umewahi kuziweka kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii. Pia utaletewa taarifa za watu waliowahi kukuzungumzia kwenye mitandao mbalimbali. Kama kuna taarifa au picha ambayo usingependa ionekane nenda pale ulipoiweka na ukaifute. Kwa kufanya hivi utaanza kusafisha wasifu wako wa kwenye mitandao.

Kikubwa sana ninachokuomba uondoke nacho hapa ni kupunguza muda unaotumia kwenye mitandao ya kijamii sasa na kutumia muda huo kufanya mambo ya msingi. Kwa mfano nimeshakutumia vitabu vitatu, hebu tumia muda unaopoteza kwenye mitandao ya kijamii kusoma vitabu hivi na kisha kuja na mpango wako mzuri wa kuboresha maisha yako na kufikia mafanikio makubwa. Kama hujapata vitabu hivi nitumie email kwenye amakirita@gmail.com na uniambie unahitaji vitabu vitatu, richdad poor dad, think and grow rich na the richest man in babylon, kisha nitakutumia vitabu hivyo.

Nakutakia kila la kheri kwenye safari yako ya kuboresha amisha yako.

TUKO PAMOJA.

Tafadhali washirikishe marafiki zako waliopo kwenye mitandao hii ya kijamii ili nao waweze kujifunza mambo haya mazuri.

kitabu-kava-tangazo432