MAKALA HII IMEANDIKWA NA IMANI NGWANGWALU WA TANGA TANZANIA.

Kuna wakati katika maisha unaweza ukajikuta unakata tamaa au unashindwa kuendelea mbele kama ulivyokuwa ukitarajia. Hii yote inatokana na pengine mfukoni huna kitu, mipango yako mingi inakuwa imekwama na kukufanya ukose tumaini la kusonga mbele.

Hali hii inapotokea ya kukosa pesa au mapato yako yanapokuwa duni ni ukweli usiopingika kwa wengi huwa inawakatisha tamaa na kuwafanya waone hawana tena maisha.

Inawezekana ni kweli kimapato uko hoi na pengine unachokuwa ukikipata ni riziki yako ya kila siku na hali hii umekuwa nayo miaka mingi na huipendi. Kama upo katika hali hii ya kushindwa mara kwa mara katika maisha na huoni malengo na mipango yako yakitimia makala hii ni yako. Kipo kitu cha muhimu unachotakiwa kufanya ili ufanikiwe na kuondokana na kushindwa.Pengine unajiuliza ufanye nini basi? unachotakiwa kufanya ni kujenga imani ya kumudu. Hii ndiyo imani unayotakiwa kuwa nayo ili ufanikiwe.

Ni lazima uweze kujiambia wewe mwenyewe unaweza kufanikiwa. Kamwe hutakiwi kujiambia huwezi na ulipofika ni basi. Jipe moyo wa kuweza halafu fanya kitu katika maisha yako. Hata wenye mafanikio hawakuwa na taarifa kutoka kwa mtu yeyote bali kutoka ndani mwao.

Ni taarifa ya kujiambia wanaweza huku ndani mwao wakiwa na ari hiyo ya kuweza bila kujali wanakabiliwa na vikwazo gani ndiyo iliyowasaidia kuwafikisha hapo walipo.Taarifa ya kama utafanikiwa zaidi ya ulipo ni lazima ujipe mwenyewe mara kwa mara na usisubiri mtu akuambie utafanikiwa.

Kuanzia leo ukimudu kuwa na imani hii ya kujiambia mwenyewe kuwa utafanikiwa, utafanikiwa kweli. Shughuli zile zile ambazo huwa unazifanya umekata tamaa utazifanya ukiwa na hali tofauti kabisa. Kazi zitakuwa nyepesi, mipango itaenda vyema na mabadilko yataanza kuonekana.

clip_image002

Hata wewe unaweza kama wanavyoweza wengine ambao unawaona waajabu kutokana na mafanikio yao. Utagundua na kukiri kwamba mafanikio yanaweza kwenda kwa mtu yeyote ili mradi tu mtu huyo aamini kwamba atafanikiwa.

Kuna wakati unaweza ukaogopa au unaweza ukawa na wasiwasi kama nikweli utafanikiwa. Hii yote inatokana na malezi au mazingira au jamii uliyokulia ambayo pengine inaamini kuwa na mafanikio makubwa ni kujichulia au kuringa.

Unachotakiwa kufanya kwa sasa bila kusita ni kuwa na fikra zeye picha na kauli za mafanikio, kwenye nafsi yako ni lazima kusisitiza kuwa utafanikiwa hata kama utakutana na vikwazo vya aina gani. Ukiweza kujipa imani hii utafanikiwa kwa sababu mafanikio ya kwanza ya binadamu ni kujua namna ya kufikiri vizuri na kutumia mawazo yako vizuri pia.

Usije ukafikiri hata siku moja ukifanikiwa sana utakuwa umekosea au ni dhambi kama ambavyo baadhi wanavyoamini katika maisha yao ya kila siku. Usidhani kuamini katika kufanikiwa ni vibaya kama baadhi ya jamii zetu zinavyotufundisha ambapo kule vijijini mtu akivuna mazao mengi sana wengine huanza kuamini kwamba mtu huyo atapata msiba au mkosi.

Katika maisha yako jenga imani ya kufanikiwana utafanikiwa kweli. Achana na hadithi ya sizitaki mbichi hizi, unachotakiwa kuwa nacho ni kumiliki mafanikiona na kuwa na pesa za kutosha.

Kwahiyo kama unaamini kabisa kutoka moyoni mwako au unahisi pengine hutafika popote kimafanikio, ujue wazi kabisa ni kweli hautafanikiwa na utakufa maskini. Lakini hujachelewa bado kwa sababu umelifahamu hili mapema unachotakiwa kufanya ni kubadili hiyo imani yako na kujenga imani ya kumudu kufanya kitu chanya katika maisha yako.

Unaweza ukabadili imani hii kwa kuanza kuamini kuwa utafanikiwa kama hao unawaona wamefanikiwa na mafanikio yatakuwa yako. Tambua kwamba mafanikio ya mtu hayaangalii sura, mtu , rangi wala jinsia bali namna mtu anavyoamini katika mafanikio na kutenda.

Pia unaweza ukabadili mtazamo au imani yako kwa kujifunza vitu mbali mbali kupitia mtandao huu wa AMKA MTANZANIA hapa utajifunza mambo mengi yatakayo weza kujengea imani ya kumudu kufanikiwa.

Na ili uweze kumudu kuitumia imani hii na umiliki mafanikio makubwa nakushauri anza kujifunza juu ya kuweka malengo makubwa utakayoweza kuyafikia. Ukishajua vizuri juu ya kujiwekea malengo yako utafanikiwa na kusonga mbele.

Fungua macho yako, tazama mbele zaidi na chukua hatua dhidi ya maisha yako. Karibu sana na endelea kutembelea mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kwa kujifunza mengi.

TUPO PAMOJA!

UNAWEZA KUWASILIANA NA MWANDISHI WA MAKALA HII IMANI NGWANGWALU KWA 0767048035.

KAMA NA WEWE UNA MAKALA NZURI ULIYOANDIKA NA UNAFIKIRI INAWEZA KUWAAMSHA WATANZANIA TAFADHALI NITUMIE KWENYE amakirita@gmail.com

MAKALA ISIWE IMEWEKWA KWENYE BLOG AU CHOMBO KINGINE CHA HABARI, IWE IMETUMIA KISHWAHILI RAHISI NA KINACHOELEWEKA NA IWE NA MANENO KATI YA 500 NA 1000 KARIBU SANA.