Wiki iliyopita katika kipengele hiki cha USHAURI tulizungumzia umuhimu na jinsi ya kuajiri watu wenye uwezo kwenye biashara yako. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hiyo bonyeza hayo maandishi na utaisoma.

Kupitia makala hiyo tuliona ni jinsi gani mafanikio ya biashara yako yanategemea watu utakaowaajiri. Hii inafanya zoezi la kuajiri kuwa zoezi muhimu sana na hivyo kupewa nafasi kubwa sana.

Wiki hii tutazungumzia tena mchakato mzima wa kuajiri ili kuweza kuwa na wasaidizi ambao watawezesha biashara yako kufikia malengo makubwa unayotazamia.

kusaili

Kabla hatujaanza kuangalia mchakato wenyewe tuangalie maoni au changamoto tuliyotumiwa na msomaji mwenzetu.

Naomba utu andikiy mada kuhusu maswali unayo weza kumuuliza mufanya kazi wakati wa usaili ili umujue kama anafaa ku ajiriwa.asante sana kwa kuuendeleya kutuelimisha.

Samahani kwa kiswahili hiko ambacho hakijanyooka sana, msomaji mwenzetu anatokea Burundi, naamini wote tumemuelewa vizuri.

Ni hatua gani unaweza kupitia kwenye mchakato huu?
Kama alivyouliza msomaji mwenzetu hapo, maswali utakayouliza wakati wa usaili ni muhimu sana ili kuweza kujua kama mtu unayemuajiri anafaa kwenye nafasi unayotaka. Japokuwa ameomba kujua ni maswali gani unaweza kuuliza, maswali hayawezi kuwa sawa kwa kila mfanyakazi.

Hapa nitaeleza vitu ambavyo unatakiwa kuviangalia kwa mfanyakazi unayetaka kumuajiri. Baada ya kujua vitu hivi wewe mwenyewe utajua ni maswali gani unayoweza kuuliza ili kujua kama ana vitu hivi muhimu vitakavyokuwezesha kukuza biashara yako.

Kuna vitu muhimu sana vya kuangalia kwenye mfanyakazi unayetaka kumuajiri. Hapa nitazungumzia vitano ambavyo ni muhimu na unavyoweza kuvidadisi wakati wa usaili.

1. Angalia vipaji.

Ajiri watu ambao wana vipaji wa ziada tofauti na vyeti tu vya elimu. Na pia vijue vipaji vyao na ni jinsi gani vitakuwa na faida kwenye biashara yako. Utajuaje vipaji vya mtu? Hakika hili sio swali la kumuuliza mtu kwamba wewe una vipaji gani. Unaweza kujua kwa kuuliza ni vitu gani anapendelea kufanya au ni vitu gani amewahi kufanya bila ya kutegemea kulipwa na watu wakafurahia hicho alichofanya.

2. Angalia ujuzi na uzoefu tofauti.

Katika mchakato huu wa kuajiri ni muhimu sana kujua ni ujuzi au uzoefu gani unaokosekana kwenye biashara yako kwa sasa. Hivyo wakati unaajiri unaweza kujua ni jinsi gani unaweza kupata mtu mwenye ujuzi au uzoefu unaotaka wewe. Kama biashara yako unafanya na kusimamia mwenyewe hakikisha wale unaoajiri wana vitu ambavyo wewe huna. Hii itakusaidia wewe kupunguza mapungufu yako ambayo yanasababisha biashara yako isifikie malengo makubwa.

3. Ajiri watu wenye imani kwenye kile unachofanya.

Katika kitu ambacho ni kigumu kumfundisha mfanyakazi ni kujali huduma anayotoa. Kujali kunatokana na mapenzi ya mtu kwenye kitu anachokifanya. Kama mfanyakazi unayetaka kumuajiri haamini na hapendi kwa moyo mmoja aina ya biashara unayofanya mwache apite. Bila ya kujali ni kwa kiasi gani yuko tayari kufanya kazi na wewe, kama haamini au kupenda biashara unayofanya atakuangusha. Hivyo ni muhimu kujua ni kwa kiasi gani anaamini na kupenda biashara hiyo na yuko tayari kujitoa kwa kiasi gani.

4. Jua malengo ya mfanyakazi wako.

Wakati unaajiri ni vyema kujua malengo na mtazamo wa mfanyakazi unayetaka kumuajiri. Jua ni kitu gani kitamsukuma kufanya kazi anayoomba, je ni fedha? Kujifunza zaidi? Kuonekana? Kwa kujua malengo ya mfanyakazi wako itakusaidia kujua ni jinsi gani unaweza kumsaidia kutimiza malengo hayo ili na yeye aweze kukusaidia wewe kutimiza malengo yako.

5. Angalia watu wenye uwezo wa kujiongoza.

Hakika huna muda wa kuanza kusukumana na mfanyakazi wako ambaye hawezi kufanya kitu mpaka umwambie fanya kitu fulani. Mfanyakazi wa aina hii atakuwa mzigo kwako na atazidi kukurudisha nyuma. Wakati unaajiri dadisi uwezo wa mfanyakazi kuweza kujiongoza kwenye kufanya majukumu yake bila ya wewe kumsukuma au kumfuatilia sana. Hii itakupa nafasi wewe kuweza kuwekeza nguvu zako kwenye maeneo mengine ya biashara yako ili kuweza kufikia malengo yako makubwa.

Haya ni mambo matano muhimu ya kuangalia wakati unaajiri mfanyakazi ili kupata mfanyakazi mwenye uwezo mkubwa wa kukusaidia kufikia malengo yako. Kumbuka mambo haya sio rahisi sana kuweza kuyajua mara moja hivyo inaweza kukuchukua zaidi ya usaili mmoja ili kujua yote haya, Pia unaweza kumpa nafasi ya kufanya kazi chini ya uangalizi kabla ya kumuajiri rasmi ili uweze kujifunza baadhi ya vitu ambavyo hukuweza kuvijua vizuri wakati wa usaili.

Jambo la muhimu kabisa ni kumjua vizuri mfanyakazi wako na jinsi anavyoweza kukusaidia kufikia malengo yako kwenye biashara yako.

Nakutakia kila la kheri kwenye kuajiri na kujenga timu nzuri itakayokupatia mfanikio makubwa.

TUKO PAMOJA.

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa kwa email amakirita@gmail.com au simu 0717396253/0755953887.

kitabu-kava-tangazo43