Katika maisha yangu nina uhakika mkubwa sana wa kupata kile ninachotaka, yaani kwa kifupi nina uhakika mkubwa wa kufikia malengo na mipango niliyojiwekea. Nina uzoefu mkubwa kwenye hilo kwa sababu nimeweza kufikia mengi sana kwa kuwa na imani hii. Je ni kitu gani kinanipa uhakika mkubwa wa kulifia malengo yoyote ninayojiwekea? Leo kuna siri kubwa nitakayokushirikisha ambayo kama na wewe utaanza kuitumia utaona mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yako.

Kabla sijakudokezea siri hii naomba nikushirikishe malengo yangu makubwa kwenye maisha huenda umeyasahau au hukuwahi kupata nafasi ya kuyajua. Pamoja na malengo mengi niloyoweka kwenye maisha yangu, kuna mawili makubwa sana ambayo napenda kuyasema wazi kwa watu wote ambao ni wa karibu kwangu. Lengo langu kubwa la kwanza ni kuwa bilionea na la pili kuwa raisi wa nchi yangu Tanzania. Fungua maneno hayo kusoma ili kuelewa zaidi.

Nina uhakika wa kufikia malengo hayo makubwa mawili kutokana na siri hii kubwa ninayokwenda kukuambia leo.

Katika vitabu na mafundisho mengi niliyopata nimekutana na falsafa nyingi sana ambazo nazitumia kwenye maisha yangu na ninaona mabadiliko makubwa. Moja ya faslafa hizo ni kutoka kwa Zig Ziggler, kuna falsafa yake moja nzuri sana ambayo imenisaidia kuweza kufikia malengo makubwa sana.

Kabla sijakushirikisha falsafa hii ili na wewe uanze kuitumia, naomba nikupe hadithi moja fupi ambayo Zigler alipenda kuitumia. Hadithi yenyewe inakwenda hivi;

Bwana mmoja alifariki na alipofika ahera alipewa nafasi ya kwenda peponi au motoni. Kwa kuwa hakuwa na uhakika aliomba atembezwe sehemu zote mbili halafu atachagua ni wapi pa kwenda. Alipelekwa motoni akakuta watu wamekaa kwenye meza ya duara mbele yao kuna vyakula vizuri sana tunavyovipenda duniani. Ila hakuna aliyekuwa anakula na wote walikuwa wameisha kwa njaa kubwa waliyokuwa nayo.

kujilisha2

Baada ya pale alipelekwa peponi na alikuta watu wamekaa vile vile kwenye meza ya duara na vyakula vizuri mbele yao. Ila kikubwa alichoona hapa watu walikuwa wanakula kwa furaha na walikuwa na afya njema.

kulisha

Baada ya ziara zile yule bwana alichanganyikiwa, aliuliza ni kipi kinawafanya walioko peponi kula kwa furaha wakati walioko motoni wanakufa kwa njaa na vyakula viko mbele yao?

Aliyekuwa anamtembeza alimpa jibu moja; hukuangalia vizuri, watu wote waliko peponi na waliko motoni wana umma wenye urefu wa mita moja, ni vigumu sana kujilisha mwenyewe kwa umma mkubwa hivyo. Walioko peponi waliweza kula kwa sababu kila mmoja aliamua kumlisha aliyeko upande wa pili wa meza(kumbuka wamekaa meza ya duara) hivyo kila aliyelisha naye alilishwa. Kule motoni kila mtu alishindwa kula kwa sababu alikuwa anafikiria kujilisha yeye kwanza, kitu ambacho hakiwezekani kutokana na ukubwa wa umma waliokuwa wanatumia. Hivyo walikuwa wanakufa huku wakijiona.

Unajifunza nini kwenye mfano huu?

Hapa ndipo Zigler anapokuja na falsafa yake maarufu ambayo kwa kiingereza inasema; you can have everything in life you want if you help enough other people get what they want. Kwa kiswahili unaweza kusema; unaweza kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako kama utawasaidia wengi zaidi kupata kile wanachotaka.Ni hayo tu, hii ndio siri kubwa unayoweza kuanza kuitumia leo kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

saidia2

Badili mtazamo wako kutoka kufaidika wewe kwanza na kuwa kuwasaidia wengi zaidi kupitia kazi, biashara au huduma unayotoa. Jinsi ambavyo wengi watakavyonufaika na kazi yako ndivyo na wewe utakavyofanikiwa.

Hii ni sheria ya asili kabisa na inafanya kazi kwa kila mtu duniani bila kujali rangi, dini, umri au kabila. Yeyote anayetumia sheria hii ana uhakika wa kufanikiwa sana na yule asiyeitumia ni vigumu sana kufanikiwa na hata akifanikiwa mafanikio hayo hayadumu kwa muda mrefu.

Unapanda kabla ya kuvuna, unatoa kabla ya kupokea na japo kuni zitakupatia moto ni lazima uweke moto kwanza, huwezi kukaa mbele ya kuni na kuziambia nipe moto zikakupa, unaweka kwanza moto kidogo halafu zinakupa moto mkubwa sana.

Kabla sijawa bilionea nitakuwa nimeshatengeneza mabilionea wengi sana, nina uhakika na hilo. Kama na wewe unataka kuwa mmoja wa mabilionea hao karibu twende pamoja kwenye safari hii.

Napenda kutumia neno TUKO PAMOJA kwa sababu namaanisha kweli kwamba kwa yule ambaye atakwenda pamoja na mimi atafikia mafanikio makubwa sana kwenye maisha yake. Kwa yeyote ambaye atajifunza yale ninayojifunza na akayatumia kwenye maisha yake nina uhakika mkubwa atafanikiwa. Ila kama hutatumia yale unayojifunza na kubadili maisha yako tutakuwa pamoja kwa maneno lakini mwisho wa siku utabaki nyuma na kuanza kulalamika haiwezekani kufikia malengo makubwa.

Anza sasa kujifunza na kutumia yale unayojifunza kwenye maisha yako. Haijalishi una miaka 18 au una miaka 60, haijalishi kama wewe ni mchaga au mzaramo, kinachojalisha ni wewe kuamua kuchukua hatua na kubadili maisha yako.

Anza kubadili mtazamo wako na kutaka kusaidia wengi zaidi ili na wewe uweze kufikia mafanikio makubwa zaidi. Kama ni mfanyakazi fanya kazi yako kwa mapenzi makubwa ya kusaidia wale wanaonufaika na kazi yako. Kama ni mfanya biashara hivyo hivyo fanya biashara yako kwa mtazamo wa kuwasaidia wanaonunua bidhaa au huduma zako kutatua matatizo yao, usiangalie tu ni faida kiasi gani unapata.

Anza kuwasaidia wengine kwa kuwasirikisha makala hii ambayo inaweza kuwafungua kwa kiasi kikubwa. Hapo chini kuna sehemu ya kushare facebook na twitter, fanya hivyo na pia waambie wengine wengi watembelee AMKA MTANZANIA ili nao waweze kufikia malengo yao makubwa.

Nakutakia kila la kheri katika kuwasaidia wengine kufikia ndoto zao ili na wewe uweze kufikia ndoto zao.

TUKO PAMOJA KATIKA SAFARI HII.