Karibu msomaji wa AMKA MTANZANIA kwenye kipengele hiki cha ushauri kwa wahitimu. Kupitia kipengele hiki tunatoa ushauri kwa wahitimu ambao ndio wanaingia mtaani, ushauri huu unawafaa hata wahitimu wa muda mrefu ambao wameshapata kazi au bado wanatafuta kazi. Ushauri huu pia unamfaa kila mtu hivyo hata kama haupo kwenye kundi la wahitimu unaweza kujifunza mambo mazuri kwa kuendelea kusoma hapa.

Wiki iliyopita tuliangalia umuhimu wa kujiwekea mwenyewe maana ya mafanikio ili kuweza kuishi maisha utakayoyafurahia. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala ile isome kwa kubonyeza; WAHITIMU; Hongereni kwa kumaliza masomo, nendeni mtaani mkajifunze upya maana ya mafanikio.

Leo tunaangalia umuhimu wa kujifunza katika dunia ya sasa ambayo inakwenda kwa kasi kubwa sana.

Kama umefurahi sana baada ya kuhitimu masomo yako na kufikiri kusoma ndio kumeisha nina habari mbaya sana kwako. Kama umejiambia sasa kitabu pembeni mpaka utakapopata nafasi ya kuongeza elimu kama shahada ya uzamili au uzamivu naomba uendelee kusoma hapa kwa makini maana upo kwenye njia ambayo inakupoteza.

Habari mbaya sana kwako ni kwamba sasa kujifunza ndio kumeanza rasmi, huu ndio wakati ambao unahitajika kusoma mara mbili au hata mara tatu ya ulivyokuwa unasoma wakati uko masomoni. Usipojifunza kwenye ulimwengu huu wa sasa ni kwamba umekata tiketi ya kuelekea kwenye kushindwa na kufa masikini.

kujisomea4

Kwa nini kujifunza ndio kunaanza rasmi?

Kujifunza ndio kunaanza rasmi kwa sababu kwa miaka zaidi ya 15 uliyokaa kwenye mfumo wa elimu kuna vitu vingi sana ambavyo hukupata nafasi ya kufundishwa. Na vitu hivyi ndio muhimu sana kuliko hata cheti ulichopewa au utakachopewa siku za karibuni.

Vitu kama umuhimu wa kuweka malengo na mipango kwenye maisha, umuhimu wa kuwa na nidhamu binafsi, elimu ya fedha binafsi, kujenga tabia za uongozi, kugundua na kuweza kutumia vitabu vyako hukupata nafasi ya kuweza kufundishwa kwa kina. Hivi ni vitu ambavyo ni muhimu sana ili uweze kuishi maisha ya mafanikio na yenye furaha.

Kwa kuwa hukupata nafasi ya kufundishwa vitu hivi na wewe mwenyewe hukutaka kujifunza, labda kwa kutokujua au kwa kutopata muda wa kutosha wa kuweza kujifunza ya shule na hayo.

Sasa sababu zote huna, kama ulikuwa hujui basi ndio umejua leo na kama ulikuwa huna muda sasa ndio umeupata rasmi. Sasa una muda ambao hakuna kujiandaa na kazi za darasani, hakuna kujiandaa na mtihani, hivyo ni wewe kujipanga na kujifunza vitu vingi uwezavyo.

Uzuri wa dunia ya sasa ni kwamba unaweza kujifunza chochote unachotaka kujifunza. Elimu iko wazi kwenye vitabu, kwenye mitandao, na hata kwenye filamu au video za vitendo.

Unaanzia wapi kujifunza?

Ubaya wa elimu hii ninayokuambia uipate ni kwamba haina mtaala na haina mtihani na vibaya zaidi haina cheti. Kwa kukosa vitu hivi hakuna anayesukumwa sana kuitafuta na hata anayeipata kwa njia hii ninayoitoa anaweza kuipuuza. Elimu hii ni muhimu sana kwako kwani ndio itakayokuletea mafanikio makubwa sana/

Mimi ni ushahidi unaoishi kwa jinsi elimu hii ilivyoweza kunisaidia kwenye maisha yangu. Unaweza kujua zaidi kuhusu hili kwa kusoma makala; Hivi ndivyo tabia ya kupenda kujisomea ilivyoboresha maisha yangu, inawezekana na kwako pia.

Kama umesoma makala hiyo utaona nimesoma vitabu zaidi ya 200 ndani ya miaka miwili, unafikiri haiwezekani? Nitakupa mpango mzuri wa kuvisoma vitabu vingi ndani ya KISIMA CHA MAARIFA. Ila kabla hujafika kwenye vitabu hivyo vingi kuna sehemu ambayo ni lazima uanzie. Kuna vitabu vingi sana ambavyo unaweza kuvipata na kujifunza, ila kuna vitabu ambavyo napenda kumshauri kila mtu aanze kuvisoma kwani hivyo vitamfanya kujitambua yeye mwenyewe na kuyaelewa mazingira yanayomzunguka.

Kuna vitabu vitatu ambavyo vimechangia kubadili maisha yangu kwa kiwango kikubwa sana. Ningependekeza kila mtanzania avisome.
1. THINK AND GROW RICH
Hiki kimenisaidia kuweza kufikia uwezo mkubwa ulio ndani yangu na kuniwezesha kuona fursa nyingi zinazonizunguka.
2. RICH DAD, POOR DAD
Hiki kimenisaidia kuhusu utofauti kati ya elimu ya darasani na elimu halisi ya mtaani. Kimenisaidia kuona mambo ambayo nilifichwa darasani na ambayo ni ya msingi sana ili kufanikiwa.
3. THE RICHEST MAN IN BABYLON
Hiki kimenisaidia kuhusiana na maswala yote yanayohusuana na fedha kuanzia kuweka akiba mpaka kuwekeza. Kimeniwezesha kuweza kujilipa mimi mwenyewe hata kwa kipato kidogo sana na kuweza kujenga akiba iliyotosha kuanzia biashara.
Hivyo ni vitabu ambavyo natamani kila mtanzania avisome. Kama huna vitabu hivi nitumie email kwenye amakirita@gmail.com na nitakutumia vyote vitatu bure kabisa.

Pia jiunge na mtanzania kwa kubonyeza maandishi haya na kuweka email na utakuwa unatumiwa vitabu vizuri vya kujisomea.

Sina muda wa kusoma vitabu vyote hivi.

Nafikiri hii ndio sababu ya kujinga sana ambayo unaweza kujipa ili usipate elimu hii muhimu. Sasa nataka nikuambie una muda mwingi kuliko ambao unafikiri unao. Kama hujui upate wapi muda soma makala hii; Jinsi ya kupata masaa mawili ya ziada kila siku, uhakika.

Siri kubwa ya kuweza kufikia mafanikio kubwa ni uwezo wa kujifunza mambo mengi. Haijalishi utaajiriwa, utajiajiri au utafanya biashara, kujifunza na kujisomea ni kitu ambacho unatakiwa kukifanya kila siku kwenye maisha yako. Uwezo wako wa kujifunza ndio utakaokupatia nafasi nzuri kwenye kazi na kukuwezesha kuendelea sana. Kama mpaka sasa hujalijua hilo soma makala hii; Uwezo na Nia ya kujifunza ndio vitakutoa na sio ufaulu wa darasani. Soma makala hiyo na ujue kile ambacho waajiri wengi wanakitafuta kwa wafanyakazi wao.

Kikubwa ninachokuomba uondoke nacho hapa leo ni kuweka utaratibu wa kujisomea kila siku, ndio namaanisha kila siku. Utaona matunda yake baadae.

Tafadhali sana washirikishe wengine makala hii ili nao wajifunze mambo haya mazuri.

Nakutakia kila la kheri katika kuyaboresha maisha yako.

TUKO PAMOJA. 

kitabu-kava-tangazo43