Hakuna kitu kizuri kwenye maisha yako kama pale ambapo unaweza kudhibiti mzunguko wako wa fedha. Yaani kama unaweza kujua kiasi gani unapata na kinatoka wapi na ni kiasi gani unatumia na unakitumia wapi unakuwa na uhuru, furaha na maisha yako yanakuwa ya uhakika. Hii ndio sababu kubwa iliyofanya tuanze na kujua fedha zinakotoka na pia zinapokwenda ili kama kuna sehemu ambayo haiko sawa uanze kuifanyia kazi haraka.

Naamini mpaka sasa kama tunakwenda sambamba umeshajua ni sehemu gani ambazo uko nyuma na huenda umeshaanza kuzifanyia kazi. Kama bado hujaanza kuzifanyia kazi nakusihi uanze sasa kwani usipoanza hutokuja kuanza, nakuhakikishia hilo.

Njia nzuri ya kuweza kudhibiti mzunguko wako wa hela ni kwa kuanza na wewe mwenyewe kubadili tabia zako zinazohusiana na fedha. Kabla hujalalamika kwamba fedha unayopata ni kidogo, kabla hujalalamika kwamba kuna anayekuibia fedha naomba kwanza uanze kwa kubadili tabia yako. Tutajadili hili vizuri kwenye makala ijayo.

Leo nataka kuelezea kwa undani kidogo kuhusu utaratibu mzuri wa kujiwekea akiba ili kuwa na maisha yenye uhakika na furaha. Kama umesoma kitabu THE RICHEST MAN IN BABYLON utakuwa umeanza kupata picha kuhusu jinsi ya kutunisha mifuko iliyosinyaa(kuongeza kipato) na pia kuweka akiba.

Hapa nitazungumzia aina tatu za utaratibu unaoweza kuanza kuutumia kujiwekea akiba ili kufikia uhuru wa kifedha. Aina hizi zinatofautiana kulingana na kipato ila mtu yeyote na mwenye kipato chochote anaweza kufanya yoyote kati ya hizi. Naomba uzisome kwa makini na kama hujaanza kujiwekea akiba chagua moja na uanze kuifanyia kazi mara moja baada ya muda utaona mabadiliko makubwa sana.

1. Sheria ya asilimia kumi(10%)

Sheria hii inasema asilimia kumi ya chochote unachopata ni ya kwako na unatakiwa kujilipa mwenyewe. Kwa mantiki hii kama kweli unajijali, kila unapopata fedha kutoka kwenye shughuli zako basi asilimia kumi ya fedha hizo unatakiwa kujilipa wewe kwanza ndio uweke hayo matumizi mengine. Tatizo linalokufanya uwe na matatizo ya kifedha ni pale unapopokea fedha zako na kukimbilia kumlipa kila mtu ila ukasahau kujilipa wewe mwenyewe kiasi hiko cha asilimia kumi.

Unapojilipa asilimia hii kumi unatakiwa usahau kabisa kama ni hela yako. Ninaposema usahau kabisa namaanisha usije ukaiweka fedha hii kwenye matumizi ya sasa au hata ya baadae.

Unaweza kuwa na akaunti maalumu ambapo unaweka fedha hii ili isiwe rahisi kwako kuitumia. Kama unashindwa kabisa kuwa na akaunti ya benki unaweza kuiweka kwenye huduma za kifedha zinazotolewa na mitandao ya simu na kujijengea nidhamu ya kutokwenda kuitoa fedha hiyo.

Baada ya kuweka asilimia hii kumi kwa muda na ukafikia kiwango kizuri cha fedha unaweza kuchukua fedha hiyo na kuiweka kwenye uwekezaji ambao utazalisha fedha zaidi. Tutazungumza kwenye makala zijazo juu ya uwekezaji.

2. Sheria ya asilimia thelathini(30%)

Sheria hii inasema asilimia thelathini ya kipato unachopata hutakiwi kuiweka kwenye matumizi yako. Kwenye kipato chochote unachopata unatakiwa kuishi kwenye asilimia 70 na usidhubutu kabisa kugusa asilimia hiyo 30. Asilimia hii 30 inakwenda kwenye mgawanyiko ufuatao.

Asilimia kumi inakuwa umejilipa mwenyewe kama tulivyoona hapo juu.

Asilimia kumi nyingine inakwenda kwenye mfuko wa dharura. Hivi sijakuambia hili eh, unatakiwa kuwa na mfuko wa dharura yaani wakati wowote inabidi uwe na kiasi cha fedha ambacho unaweza kukitumia kama kukitokea dharura yoyote. Kwenye maisha kuna mambo mengi sana ambayo hayatabiriki, hivyo ni vizuri sana unapokuwa na fedha kidogo uliyoweka pembeni kukabiliana na janga lolote litakalokukumba. Inawezekana wewe au mtu wa familia yako akapata ugonjwa utakaosumbua sana, inawezekana nyumba ikaungua moto. Inawezekana gari likaharibika ghafla na mengine mengi ambayo yanakuja bila ya kubisha hodi. Hata kama una bima kwenye baadhi ya mambo kama afya au ajali bado ni muhimu kuwa na fedha ya akiba kwa sababu kuna wakati bima inaweza kufikia kikomo wakati bado wewe tatizo lako halijakwisha. Weka fedha hii na usijaribu kabisa kuitumia. Kama itakaa muda mrefu bila ya matumizi unaweza kuwa unaondoa kiasi fulani unapeleka kwenye uwekezaji na sio kwenye matumizi.

Asilimia kumi iliyobaki ni sadaka au msaada kwa wanaohitaji. Kama wewe ni muumini mzuri wa dini, karibu kila dini ina utaratibu wake wa kutoa sadaka, zaka au fungu la kumi. Hata kama wewe sio muumini wa dini bado unaweza kutumia asilimia hiyo kumi kutoa msaada kwa watu wenye uhitaji kama watoto yatima, watu wenye ulemavu, wazee na makundi mengine. Toa fedha hii kama sadaka au msaada na utapata nguvu kubwa sana ya kuendelea kutafuta.

3. Sheria ya asilimia kumi ya matumizi yako ya siku.

Sheria hii nimeitengeneza mwenyewe hivyo usishangae ukaitafuta kwenye vitabu na kuikosa. Sheria hii haina tofauti na hizo hapo juu ila ni uboresho tu kwa ajili ya watu ambao wana tatizo kubwa inapokuja kwenye kujiwekea akiba.

Kwa mfano tuseme mtu anapokea mshahara wa shilingi laki sita kwa mwezi, hivyo kwa sheria ya asilimia kumi, kila mwezi mtu huyu anatakiwa kuweka pembeni shilingi elfu sitini. Kama mtu huyu hana tabia nzuri ya kujiwekea akiba ataona fedha hiyo ni kiasi kikubwa sana na hivyo atashindwa kuiweka akiba.

Badala ya kutumia kiasi kikubwa hivyo ambacho kinaweza kukupa sababu ya kushindwa, tunakwenda kuvunja kiasi hiko kikubwa na kuwa kidogo sana kiasi kwamba huwezi kushindwa kukiweka.

Kwa mfano huo hapo juu, tuseme mtu huyu matumizi yake yote kabisa kwa siku ni shilingi elfu ishirini, kila siku inabidi aweke akiba asilimia kumi ya matumizi hayo. Hivyo kwa mtu huyu ataweka akiba shilingi elfu mbili kila siku, kiasi ambacho ni rahisi sana kufuata. Akiweka hivi mwisho wa mwezi anakuwa ameweka shilingi ngapi? Elfu sitini na hapa hajatumia nguvu nyingi.

Utaratibu huu ni mzuri sana kwa watu ambao wanapata vipato vya siku kama watu wanaofanya kazi za vibarua na wafanyabiashara wadogo wadogo.

Chagua njia moja kati ya hizo na anza kuitumia mara moja, anza kuitumia leo na usingoje kesho.

ZOEZI LA WIKI.

Wiki hii chukua kalamu na kitabu chako ulichokuwa unaandika mapato na matumizi kisha fanya mchanganuo wa njia hizi tatu na ona ni ipi itakufaa kuanza nayo. Baada ya kukamilisha mchanganuo wako fanya maamuzi ya njia utakayotumia na anza utekelezaji.

Kumbuka ukishafanya maamuzi hakuna kurudi nyuma.

Tunaweza kuendelea kujadiliana kwenye FORUM-MAJADILIANO kuhusiana na tabia hii ya matumizi ya fedha tunayoijenga.

Nakutakia kila la kheri katika kuboresha maisha yako.

TUKO PAMOJA.