Mpaka sasa tumeshajifunza mengi kwenye tabia za mafanikio na mwezi wa saba na wa nane tunaendelea kujadili jinsi ya kujenga tabia nzuri kwenye matumizi na uhufadhi wa fedha.

Kitu kikubwa ambacho mpaka sasa umeshakifanya kama unafuatilia mafunzo haya kwa ukaribu ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuanza kujijengea tabia ya kuweka akiba.

Na kama umeelewa na kuyatumia vizuri zaidi utakuwa umeshaanza kuongeza kipato chako kwa kutumia fursa nyingine zinazokuzunguka. Lengo letu kubwa sana ambalo inabidi kwa njia yoyote ile uweze kulifikia ni kuweka akiba. Maana hata kama utapunguza matumizi yasiyo ya msingi bado fedha huwa haikosi matumizi. Hata kama utaongeza kipato chako kwa kiasi gani kama huna utaratibu mzuri wa kujiwekea akiba utaendelea kuwa na matatizo ya fedha kila siku.

Kwa hiyo kama umeshaanza kujiwekea akiba nakupa hongera nyingi sana kwa sababu sasa umeshakata tiketi ya kuelekea kwenye mafanikio. Unachosubiri ni kupanda basi la kukufikisha kwenye mafanikio unayotazamia.

KUWEKA AKIBA NI HATUA TU YA KUFIKIA UHURU WA KIFEDHA.

Kama nilivyosema hapo juu kuweka akiba ni tiketi ya wewe kufika kwenye uhuru wa kifedha, kufika kwenye uhuru wenyewe ni mpaka upande basi na safari iendelee. Hivyo usibweteke kwa kuweka akiba na kufikiri mambo yamekwisha. Kuweka akiba ni hatua moja ya kufikia mafanikio na uhuru wa kifedha. Kuna hatua nyingine muhimu na zinazohitaji uelewa na umakini mkubwa ili usijekupoteza akiba yako uliyoikusanya kwa shida.

Kwa tabia hii uliyojijengea ya kuweka akiba kila baada ya muda fulani au kufikia kiwango fulani ni vyema ukaondoa fedha zako ulipoweka akiba na kuziweka sehemu nyingine ambazo zitazalisha zaidi au zitakua kwa thamani.

Ni muhimu kufanya hivyo kwa sababu uchumi wa sasa uko lege lege mno, mfumuko wa bei ni mkubwa na unaendelea kukua kila siku. Hivyo kama utakuwa na milioni moja leo, miaka kumi ijayo itakuwa na thamani ndogo kuliko sasa. Chukua mfano wa miaka kumi iliyopita ambapo sukari ilikuwa ikiuzwa kilo moja chini ya shilingi elfu moja, sasa hivi inauzwa karibu elfu mbili. Ni ongezeko la bei maradufu, hivyo kama ungekuwa na fedha zako umeweka kipindi hiko mpaka sasa ingekuwa na thamani ndogo sana.

Kwa njia yoyote unayotumia kuweka akiba iwe  ni benk au mitandao ya simu, fedha zinapofikia kiwango fulani ni vizuri kuziondoa na kuziweka sehemu ambapo zitazalisha au kuongezeka thamani.

Ni kitu gani kitaongeza thamani ya fedha au kuzalisha fedha zaidi?

Njia pekee ya kuongeza thamani ya fedha zako au kuzalisha zaidi ni kuziwekeza. Na hapo kwenye uwekezaji ndio kuna changamoto kubwa sana kwa sababu ndipo watu wanapofanya makosa makubwa na kujikuta wanarudi nyuma badala ya kwenda mbele.

Kuna sehemu nyingi sana ambazo unaweza kuwekeza fedha zako na zikazalisha au kuongezeka thamani. Kitu muhimu ni kujifunza kwanza uwekezaji unaotaka kufanya kabla ya kuweka fedha zako.

Usifanye uwekezaji kwa sababu kuna mtu fulani naye anafanya, jiridhishe kwanza na uwekezaji huo ndio uweze kuweka hazina yako uliyoichuma kwa juhudi kubwa.

Kuanzia wiki ijayo tutajadili aina za uwekezaji ambazo unaweza kuwekeza fedha zako. Pamoja na vile nitakavyoshauri bado ni muhimu na wewe kujiridhisha zaidi. Elimu na uelewa wa kile unachofanya ni muhimu sana ili kuepuka kufanya makosa ambayo ungeweza kuyazuia.

ZOEZI LA WIKI.

Wiki hii naomba tufanye zoezi moja la kufanya utafiti kidogo ni aina gani za uwekezaji ambazo zinapatikana maeneo ambayo unaishi au kufanya shughuli zako. Angalia kwa makini, uliza watu wengine na pia fuatilia taarifa mbalimbali ili kujua uwekezaji unaopatikana eneo ulipo na pia ujue gharama za uwekezaji huo. Baada ya kujua andika chini kwenye kitabu chako ulichonunua kwa ajili ya kuweka mipango hii ya fedha. Baadae tutajadili zaidi kuhusu aina za uwekezaji tunazoweza kufanya na utaangalia zile ulizoandika wewe na kuendelea kujifunza zaidi.

Kumbuka kutushirikisha yale unayojifunza kwenye utafiti wako huo mdogo kwenye RORUM ZETU ZA MAJADILIANO.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kufikia uhuru wa kifedha.

TUKO PAMOJA.