Moja ya faida kubwa za kuwa mjasiriamali ni kwamba unakuwa na uhuru na muda wako. Tofauti na mtu aliyeajiriwa ambaye anahitajika kufika kazini kabla ya saa mbili na hawezi kuondoka mpaka saa kumi, wewe mjasiriamali una faida kubwa kwa kuamua ufanye nini na wakati gani.

Pamoja na kuwa na uhuru huu mkubwa wa muda bado sio wajasiriamali wote ambao wanaweza kupangilia na kutumia muda wao vizuri. Kwa kushindwa kupangilia muda vizuri unajikuta unapoteza muda mwingi na hivyo kushindwa kufikia mafanikio makubwa unayotazamia.

Muda ni kitu muhimu sana kwa binadamu, ila ni kitu muhimu zaidi kwako wewe mjasiriamali. Poteza milioni kumi utaweza kupata nyingine ila poteza saa moja hutaweza kulipata tena. Ndio maana ni muhimu sana wewe kujifunza matumizi mazuri ya muda katika ujasiriamali wako.

Leo tutajadili mambo matatu muhimu ya kufanya ili kuwa na matumizi mazuri ya muda.

1. Jua thamani ya muda wako.

Ni muhimu sana kujua thamani ya muda wako ili ujue unapopotea ni kiasi gani cha fedha unapoteza. Kwa mfano kama umepanga kila mwezi upate shilingi milioni kumi, igawe hiyo kwenye siku ambazo utafanya kazi. Kama utafanya kazi siku tano kwa wiki, kwa mwezi itakuwa siku ishirini. Ukigawa milioni kumi kwa siku ishirini inakupa laki tano kwa siku, Ukigawa laki tano kwa masaa utakayofanya kazi kwa siku, tuchukue mfano unafanya kazi masaa kumi itakuwa shilingi elfu hamsini kwa saa moja. Kwa hiyo kila saa yako moja ya kazi ni shilingi elfu hamsini. Hivyo chochote utakachofanya kwenye muda wako wa kazi kiwe na thamani hiyo. Tofauti na hapo unapoteza muda. Fanya mahesabu yako kutokana na kiwango ulichopanga kupata na ukishajua gharama ya saa yako moja usiipoteze bila ya kuzalisha au kuandaa mazingira ya kuzalisha kiasi hiko cha fedha.

2. Kuwa na orodha ya vitu utakavyofanya kila siku.

Usianze siku ukiwa hujui ni vitu gani unavyotaka kufanya kwenye siku hiyo, hili ni kosa kubwa linalowafanya wajasiriamali wengi kujikuta hawajui wafanye nini na kwa muda gani. Kila siku kabla ya kulala au kila siku unapoamka chukua kijitabu chako cha mipango(kama huna kijitabu hiki, nunua na uwe nacho) na andika mambo utakayofanya kwenye siku hiyo. Anza na mambo yale magumu ndio ufanye mepesi. Hii ni kwa sababu mwanzo wa siku unakuwa na nguvu na utulivu wa kutosha. Kwa kuwa na utaratibu huu wa kuorodhesha mambo unayofanya kwa siku kutakuwezesha kutumia muda wako vizuri. Unapopangilia mambo yako kwa orodha unajikuta unafanya mambo yako kwa wakati na kufikia mafanikio makubwa.

3. Acha kufanya mambo ambayo hayana uzalishaji mkubwa.

Wewe kama mjasiriamali tayari unajua ni vitu gani ukivifanya vinaleta tija kubwa kwenye biashara yako. Na pia unajua ni vitu gani unaweza kuvifanya vizuri. Vitu vingine vyote ambavyo havina tija sana ila ni muhimu kufanyika tafuta mtu mwingine wa kufanya. Na kama kuna vitu ambavo ni muhimu kufanyika ila huwezi kuvifanya vizuri tafuta mtu anayeweza kufanya vizuri na mpe jukumu hilo. Unaweza kuona kwa kufanya hivi unaongeza gharama ila itakulipa sana baadae. Kwa sababu kama wewe utapata muda wa kushughulikia vizuri mambo yenye uzalishaji mkubwa utapata faida kubwa kuliko hata ile unayomlipa yule anayekusaidia mambo madogo madogo au usiyoweza kuyafanya vizuri.

Unaweza kufikia mafanikio makubwa kama mjasiriamali kama utakuwa na matumizi mazuri ya muda wako. Unahitaji nidhamu nzuri sana kwenye matumizi ya muda ili uweze kuutumia vizuri. Ni afadhali upoteze fedha kuliko kupoteza muda. Utumie muda wako vizuri kwa kujua ndio kitu muhimu kwako ili kufikia mafanikio.

Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.

TUKO PAMOJA