Baada ya Robert na Mike kukubaliana wamuombe baba yake Mike awafundishe kuwa matajiri Mike aliongea na baba yake jioni na alikubwali kukutana nao siku inayofuatia.

Siku hiyo Robert na Mike walifika ofisini kwa baba yake Mike, pale walikuta wafanyakazi wa baba yake Mike wakimsubiri. Ilionekana ni ofisi yenye vitu vilivyochoka na vya zamani. Wakati wamekaa wanasubiri baba yake Mike alitokea na akasema Mike ameniambia mnataka kujifunza jinsi ya kutengeneza fedha, wakajibu ndio.

Baba yake Mike alikubali kuwafundisha ila aliwaambia hatawafundisha kwa mtindo wa darasani. Aliwaambia watamfanyia kazi ndio awafundishe, hatafundisha kwa nadharia bali kwa vitendo kama inavyofanyika shuleni. Aliwaambia watamfanyia kazi kila siku ya jumamosi kwa masaa matatu na kila saa moja atawalipa senti kumi. Robert alisema jumamosi anakwenda kwenye michezo, baba yake Mike alimwambia chagua michezo au kujifunza. Robert aliamua kukubali kujifunza.

Jumamosi iliyofuata Robert na Mike waliripoti kwenye eneo lao la kazi ambapo walikuwa wanamsaidia mmoja wa wafanyakazi wa baba yake Mike. Ilikuwa ni kazi ya kupanga vitu na wakati mwingine kufanya usafi. Baada ya masaa matatu kila mmoja alipewa senti zake 30 na kuondoka. Wlifanya hivi kwa wiki tatu bila ya kitu kingine cha ziada, wanafanya kazi, wanapewa ujira wao na kuondoka.

Jambo hili lilimkera sana Robert kwa sababu aliahidiwa atafundishwa ila hakuwahi kumuona tena baba yake Mike. Alikasirishwa sana na hali ile na alimwambia Mike kwamba anaacha kazi ile. Mike alimwambia baba yake alisema Robert atakapokuwa tayari kuacha kazi amwambie ili akutane nao. Robert aliposikia vile alimuuliza ina maana tulikuwa tumewekwa kwenye mtego? Mike alimwambia inawezekana.

Hitaji la kulipwa.

Baada ya Robert kupata taarifa za baba yake Mike kutaka wakutane nae pale atakapokuwa anataka kuacha kazi, alipata hasira sana. Hata baba yake Robert alichukia sana na kusema baba yake Mike anawatumikisha na anakwenda kinyume na haki za watoto. Baba yake Robert alimwambia Robert adai haki yake na atake kuongezwa mshahara.

Jumamosi iliyofuata Mike alienda kwenye ofisi ya baba yake Mike na aliambiwa asubiri ataonana nae. Alikaa muda mrefu pale bila ya kumuona, alizidi kupata hasira sana na alikuwa tayari kumvaa baba yake Mike kutokana na kitendo chake cha kumtumikisha. Saa moja baadae baba yake Mike alimwambia aingie ofisini na alipofika alimwambia nimesikia unataka kuacha kazi au uongezwe mshahara. Robert alimjibu kwa hasira kwamba hujatimiza ahadi yako, uliahidi tukufanyie kazi kisha utatufundisha lakini hujawahi kutufundisha.

Robert alimwambia maneno makali sana kwamba hajali wafanyakazi wake, anawatumikisha na kuwalipa kidogo. Ana tamaa ya fedha nyingi na hajali watu wengine. Na pia hatimizi ahadi yake ya kuwafundisha. Baba yake mike alimwambia mbona nimekuwa nawafundisha? Robert alijibu kwa hasira hujawahi kutufundisha hata siku moja kwa wiki zote tatu ambazo tumefanya kazi.

Baba yake mike alimuuliza Robert kufundisha maana yake ni kuonge n kutoa mhadhara? Robert alijibu ndio na ndivyo wanavyofundishwa shuleni. Rich Dad alimwambia maisha hayafundishi hivyo, alimwambia maisha ndio mwalimu bora na huwa hayazungumzi bali yanakusukuma. Na kila yanapokusukuma ndio yanakuambia amka kuna kitu cha kujifunza. Maisha yanamsukuma kila mtu, baadhi wanajifunza, baadhi wanakata tamaa. Wanaokubali kujifunza wanaendelea, wanaokata tamaa wanaacha.

Tunajifunza nini kwenye sehemu hii?

Katika sehemu hii kuna mambo mengi sana ya kujifunza, baadhi ni;

1. Ni muhimu sana kujifunza kitu unachotaka kwenye maisha yako.

2. Unapotaka kitu kuna vitu vingine inabidi uviache hata kama unavipenda kiasi gani. Kwa mfano ilibidi Robert akubali kufanya kazi siku ya jumamosi japo ilikuwa siku ya michezo.

3. Maisha ndio mwalimu bora, kila siku yanatufundisha bila ya kutupa maneno kama inavyofanyika darasani.  Anayeweza kujifunza kutokana na changamoto za kila siku za maisha anaweza kufikia mafanikio makubwa.

Tukutane kwenye sehemu ijayo ya uchambuzi huu wa kitabu.

Karibu sana, TUKO PAMOJA.