Wiki iliyopita tuliweka makala ya kijana wa kitanzania aliyeanza biashara na mtaji wa milioni nne na baada ya miaka mitatu ana zaidi ya milioni mia moja. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hiyo bonyeza hayo maandishi.

Katika makala ile tulipata kwa ufupi historia ya John Matiku na niliahidi kwamba John ataendelea kutushirikisha mbinu mbalimbali alizotumia kufikia mafanikio haya makubwa. Kwa ahadi hiyo, leo unapata makala moja wapo na nyingine zitaendelea kukujia hapa hapa AMKA MTANZANIA hivyo endelea kutembelea kila siku.

Baada ya kuweka makala ile nilipata maswali na changamoto nyingi sana kutoka kwa wasomaji wengi. Wengi walisema ni kitu kisichowezekana na wengine wakaenda mbali zaidi wakisema John amenidanganya. Naelewa yote haya kwa sababu mafanikio ya John ni makubwa sana na Watanzania wengi hatujazoe hali hiyo. Ndio maana mtandao huu wa AMKA MTANZANIA upo ili kukuonesha kwamba inawezekana na unakupatia wewe mbinu za kuweza kufikia mafanikio makubwa pia.

magori

Hapa chini John anatueleza safari yake ya kutafuta mafanikio ya kiuchumi.

Natambua kua wako watu wengi Duniani na hata hapa kwetu Tanzania ambao wametafuta na kupata mafanikio kwa njia ngumu na zenye changamoto nyingi na kubwa kuliko hata njia niliyotumia na ninayotumia mimi. Lakini lengo la makala hii nikutaka kukuonesha wewe kijana mwenzangu kua UTHUBUTU na UBUNIFU kidogo tu unaweza kukusogeza hatua nyingi mbele kuelekea kwenye mafanikio makubwa.

Hapa nimeamua kukuelezea safari yangu kuanzia chini sana ninaposema chini sana namaanisha nilichokuanacho ni elimu ya msingi tu na nauli yakwenda mjini 5000! Hapa namaanisha kuwa nilishindwa kuendelea na elimu ya sekondari kwa sababu ambazo zisingeweza kuzuilika wakati huo. (lakini kwa sasa zinazuilika)

Baada ya kuona uwezekano wa kuendelea na shule ni mdogo sana niliamua kutokomea mjini, kama vijana wengi tunavyofanya. Huko nako sikuwa na wazo kubwa sana, maana nilichokuwa naenda kutafuta huko ni maisha. Hili neno kutafuta maisha limewapotezea muda watu wengi kwa miaka mingi sana na mimi nikiwa miongoni mwao, kwa sababu kwanza unapoenda sehemu bila kujua ni kazi gani haswa inakupeleka huko, inahitaji rasilimali gani kuifanya na inahitaji ujuzi gani,  haina tofauti na kubaki ulipokua kwa sababu mazingira rafiki pekee bila ubunifu wowote hayawezi kukupa matokeo yoyote yenye maana.

Ndicho kilichotokea kwangu pia baada ya kuelekea mjini na kukaa huko miaka mitatu (2004-2006) bila mafanikio yoyote makubwa na hivyo nikaamua nirudi nyumbani ili nitumie nilivyo viacha nyumbani (kilimo na mifugo) kuona kama naweza kujikwamua. Nasikitika napo nilikwama maana rasilimali hizo hazikutosha kuleta mabadiliko makubwa. Pamoja na kwamba sikupata mafanikio makubwa mjini hasa ya fedha lakini mjini kulinisaidsia kidogo angalau kua na ujasiri (kujiamini), kutamani na kuchagua  aina ya mafanikio, nakuniongezea uelewa zaidi kuhusu maisha ya mtaani na uhusiano na jamii kwa ujumla.

Hivyo baada ya kugundua kilimo kile na zana zile kisingenitoa niliamua moja kwa moja kurudi mjini ila mara hii tofauti na mwanzo niliamua kua nitarudi nikiwa najua haswa ni nini naenda kufanya huko na nitahitaji zana gani ili kupata matokeo niliyoyakusudia. Hivyo niliamua kutafuta kazi kwa watu tunaofahamiana, nikapata huko mbeya kazi ya kuuza duka, wakati huu mimi nikiwa musoma(nyumbani). Nashukuru mungu pia kazi hii niliyoipata ilinipa fursa ya kuongeza uwelewa wangu kwa kiwango kikubwa sana. Japo ujira ulikua kidogo sana mwanzoni (40000) unaweza kudhani kwa mwaka huo 2007, ilikua kubwa lakini hasha hata kama ni kwa leo haingezidi 100,000. Hivyo bado ilikua ndogo lakini niliamini zipo fursa zaidi ndani ya kazi hiyo, na hivyo nikaamua kufanya kazi kwa bidii, kwa upendo wa hali ya juu sana na kua na matumaini makubwa kua pamoja na maslahi kidogo ila nikifanya kwa bidii siku moja itanifikisha mahali flani au kunipeleka hatua kadhaa mbele. Na kweli ndani ya mwaka mmoja uhusiano wangu na boss wangu uliimarika zaidi kiasi kwamba sasa nilianza kuaminika zaidi na kupewa majukumu makubwa zaidi nikaona kunauwezekano wa maslahi yangu kubadilika pia. Na kwa picha hii tayari nikawa na  malengo makubwa ya kujiajiri mwenyewe baada ya miaka mitano kutoka 2008-2013, niliamua mfumo wa maisha ninayoyataka, nikaamua njia nitakazotumia na kuupata na nikaanza safari ya kujibana na kuweka akiba kwa lengo la kupata mtaji wa kuanzisha biashara lengo likiwa nikujiajili ifikapo 2013.

Ukweli ni kwamba pamoja na kuaza na mshahara kidogo sana mabadiliko ya kiuchumi kazini yalisaidia sana mshahara wangu na wa wenzangu kuboreka ndani ya muda mfupi, si sana ila uliboreka kwa kiwango ambacho kilisaidia kunisogeza karibu na kutimia kwa malengo yangu na hivyo kufikia hatua ya kujiajiri mapema (2011 january) kabla ya 2013.

Nilianza na mtaji wa sh 4,600,000 nikianza na bidhaa chache tu za nyumbani kama magodoro, na baadhi ya vifaa vya umeme mwanzo ulikua mgumu sana kwa kweli ulikua mgumu kiasi cha kufikiria kurudi kazini ikiwa hali ile ingedumu kidogo vile. Hakukua na wanunuzi wa bidhaa kwa siku za mwanzo, hakukua na pesa ya kujikimu, hakukua na matumaini kua siku chache zijazo huwenda mauzo yatapatikana,  zaidi hali ilizidi kua ngumu siku hadi siku!

Hali hii ngumu ikageuka kuwa fursa ya soko kubwa baada ya UBUNIFU KIDOGO TU, na ikanisaidia kutengeneza mtandao wa wateja marafiki ambao nasafiri nao mpaka sasa huku kwa pamoja tukiwa tumefikia mtaji wa zaidi ya milioni 100, sasa kutoka kwenye milioni 4.6. Hatua hii ni kubwa sana kwangu si kwa sababu ya kiwango hicho cha fedha ila kwa kua hatukuwahi kuifikia hatua hiyo.

Nyuma ya mafanikio hayo ambayo ni kiasi tu ya kile ninachotamani kuona kikitokea kuna vitu vingi sana vimetokea na kwa makala hii ningependa ujifunze machache yafuatayo!

1. MAFANIKIO YOYOTE YA KIWANGO CHA JUU YANAHITAJI UBOBEVU WA HALI YA JUU SANA KATIKA JAMBO FLANI. mimi kwa miaka yangu yote ukitoa muda ule niliokua shuleni muda wangu wote nimeutumia kufanya bishara na kujifunza kuhusu biashara. Hata pale nilopokua nafanya kazi nilifanya kazi yangu kama  boss wangu (sikuwahi kufanya kama mfanyakazi) nilikua nafanya kazi yangu kama mfanyabiashara.

2. UPUNGUFU wa aina yoyote ile hauwezi kua kikwazo cha wewe kua unavyotaka kuwa hasa kama umedhamiria na umeamua unavyota kuwa.

3. UPENDO WA DHATI utakuvusha kwenyechangamoto zote, kama kunakitu nakifurahia ni kazi na eneo langu la kazi katika hali ya kawaida huwa sipitishi siku bila kufika na kufanya kazi japo kidogo kazini kwangu iwe weekend, siku kuu au vyovyote vile kazini lazima nifike.

4. KATIKA KUTAFUTA MAFANIKIO KAMA KUNA KUFA; Ufe ukiwa vitani shindwa ukiwa upo unafanya unachofanya, usiogope kufanya kitu kabisa eti kwa kuhofia itakuaje kama utashindwa. Wewe fanya kwa uwezo wako wote, ili upate matokeo halisi. Acha kijipa matokeo ya kitakachotokea kabla hujatenda.

5. USIDHALAU UBUNIFU WAKO, HATA KAMA UNAUONA NI MDOGO KIASI GANI(DUNIA INAUHITAJI!) Hebu fikiria mtu anabuni kucha za bandia ili hali anajua watu wanakucha halisi na bado anapata soko, kope bandia za macho, watu wananunua anapata hela! Fikiri tena ukubwa wa meli kubwa za mizigo lakini zinageuzwa na usukani mdogo tu, hata magari makubwa sana ya mizigo hugeuzwa popote apendapo kwenda dereva na usukani mdogo tu!  Jinsi unavyoona udogo wa vitu hivi na maajaju yake duniani ndivyo ilivyo nguvu ya ubunifu wako unaodhani ni kidogo tu, na pengine haujaufanya kazi kabisa!
AMUA KUU HESHIMU SASA UBUNIFU WAKO NA UTAONA MAAJABU.

Niwasihi watu wote ambao tuko kwenye safari hii ya kutafuta mafanikio na kwa bahati nzuri tuna mafanikio kiasi flani, kama kweli tunaamini katika ukweli tuamue kushirikishana hadithi zetu, tuwambie wenzetu ambao huwenda ndio wameanza au bado wako chini sana njia tulizotumia kupita mpaka sasa tuko hapa tulipo ili nao wanapopita kwenye changamoto wasione ni kitu kipya sana.

Hayo ndiyo aliyotushirikisha John kwa siku ya leo, kwenye makala ijayo atatuambia ni ubunifu gani aliotumia kwenye biashara yake mpaka ikampelekea kujenga mtandao wa wateja ambao wana urafiki mkubwa na yeye. Endelea kutembelea AMKA MTANZANIA ili kujifunza na pia waalike wenzako nao wasome ili wajifunze.

Kama na wewe una hadithi nzuri ya mafanikio ambayo inaweza kuwahamasisha watanzania wenzetu kuboresha maisha yao na kufikia mafanikio makubwa, tafadhali wasiliana na mimi kwa 0717396253/amakirita@gmail.com

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kufikia mafanikio makubwa.

TUKO PAMOJA.