Katika safari ya mafanikio kuna wakati ambapo mipango na malengo yetu huwa inajikuta inaenda hovyo tofauti na tulivyokuwa tumepanga mwanzoni. Hiki huwa ni kipindi kigumu sana kwa wengi kwa sababu malengo yote ambayo umekuwa umejiwekea yanakuwa yamekwama na umeshindwa kupata kile ulichokuwa ukikitazamia.

Wengi wetu tunapokutana na hali hii, hapo ndipo hali ya kukata tamaa hujikuta inaingia ndani mwetu. Unakuwa ni wakati ambao unakuwa unahisi maisha huna tena na wakati mwingine inakuwa inakuuma sana kila unapofikiria na kuangalia mipango yako iliyoshindwa na umepoteza muda wa kutosha.
Kuna wakati unakuwa unahisi pengine huwezi kurudi katika hali yako ya kawaida na kwamba kila kitu kimeharibika kutokana na hasara uliyoipata au mambo yako kwenda vibaya sana. Inawezekana kabisa na wewe ukawa miongoni mwa watu walioumizwa na maisha kwa namna moja au nyingine hali inayokufanya ukose tumaini katika maisha yako.
 Ninachotaka kukwambia unapokutana na hali kama hii usikate tamaa, fungua macho yako, lipo tumaini la kufanikiwa zaidi ya ulipokuwepo. Vipo vitu muhimu vya kukumbuka wakati mambo yako yanapokwenda hovyo. Vitu hivi vitakuwa nguzo kwako yakukufanya usonge mbele na kukupa faraja kila unapokutana na vikwazo vitakavyo kukatisha tamaa na kukurudisha nyuma.
Vifuatavyo ni vitu muhimu vya kukupa hamasa na kukumbuka wakati mambo yako yanapokwenda vibaya:-
1.Kila kitu katika maisha ni cha muda mfupi. 
Hiki ni kitu muhimu sana kukumbuka hasa mambo yako yanapokwenda vibaya. Hakuna tatizo katika maisha ambalo linaweza kudumu moja kwa moja. Kila kitu kipo kwa muda, kinazaliwa na kufa.
Hata matatizo uliyonayo yana muda wake, inawezekana biashara zako zinaenda hovyo, umepoteza kazi na mipango yako mbalimbali uliyojiwekea imekwama na kufa lakini ninachotaka kukwambia si kitu kila kitu kipo kwa muda.
Nafasi ya kufanikiwa tena zaidi ya ulipokuwa ipo kwani upo katika kipindi cha mpito tu. Kikubwa chukua hatua muhimu ya kujifunza kutokana na kipindi unachopita sasa. (Unaweza ukasoma pia Siri kubwa kwenyeBiashara na Maisha,kila kitu kinakufa)

 
2. Kulalamika na kuogopa hakutakusaidia kitu.
Jifunze kuwa na mawazo chanya, acha kulalamika sana wala kuogopa, unapolalamika pasipo kujua unakuwa unavuta nguvu nyingi hasi na matokeo yake unashangaa unakuwa mtu wa matatizo kila siku kama vile una mkosi au laana.
Kulalamika kwako juu ya mambo yako kwenda hovyo hakutakusaidia kitu chochote badala yake chukua hatua muhimu ya kubadilika na kuangalia fursa upya, acha kulalamika wala kujilaumu tena na Kama unaendelea kufanyakosa hili katika maisha yako utakufa maskini.
3. Maumivu ni sehemu ya kukua.
Watu wengi wanapokutana na ugumu katika maisha hasa mambo yao yanapokwenda hovyo hiki huwa ni kipindi kigumu sana kwa wengi na usipokuwa makini pia inakuwa ni rahisi  kukata tamaa.
Unapokumbana na hali hii jipe moyo kwani hakuna maumivu yanayokuja bila lengo.Vitu vizuri mara nyingi vinataka muda ili kuvifikia, usikatishwe tamaa na mambo yako kwenda hovyo wala kuumia, jifunze kitu na tambua maumivu ni sehemu ya kukua kisha songa mbele.
 4. Majeraha uliyonayo ni dalili ya ukomavu.
Unaweza ukawa umeumia  vya kutosha kutokana na kukosa au kupoteza ulichokuwa ukikihitaji hilo lisikukatishe tamaa wala usije ukafanya kosa la kuruhusu majeraha uliyonayo yakakurudisha nyuma au yakakufanya uishi maisha kwa kuogopa sana.
Kumbuka siku zote majeraha uliyonayo yanaonyesha sasa umekomaa na una uwezo wa kukabiliana na hali kama hiyo tena kwa ukomavu zaidi, jipe moyo.
5. Kila hatua uliyochukua ni mafanikio. 
Unatakiwa pia ujue hili hatua ulizochukua hadi ukafikia hapo ulipo ni moja ya hatua kubwa ya mafanikio. Usijione hufai au umekosea sana, mbio ulizozipiga sio bure umefanya kitu ambacho kinakupeleka kwenye mafanikio.
Unaweza ukajifunza vitu vingi sana kutokana na hayo unayoyaona makosa na ukafanikiwa zaidi. Tambua maisha tunayoishi hayapo katika mstari mnyoofu kama wengi wanavyofikiri, maisha yapo kama mstari uliopinda pinda nikiwa na maana upo wakati ambao ni lazima utake usitake utakutana na milima na mabonde ya maisha.
Kama unaona umekosea sana na unaumia kwa mambo yako kwenda hovyo hilo lisikutie shaka ni hatua mojawapo ya mafanikio. Ni muhimu kujua mafanikio yanapita katika hatua nyingi mojawapo ni hiyo ambayo unaona mambo yako yameenda vibaya. Chukua jukumu la kusonga mbele zaidi na sio kuganda pale ulipo.
6. Kuwa chanya muda wote.
Unapokuwa katika matatizo au mambo yako yanapokwenda hovyo kinyume na ulivyokuwa ukitarajia kitu muhimu unachotakiwa kukumbuka pia ni kuwa na mawazo chanya muda wote. Acha kulalamika wala kulaumu hata kama kutakuwa na watu unaona kama wanakucheka, wewe tabasamu achana nao kwani ni kipindi muhimu sana cha kutuliza akili yako na kupanga mipango upya ya kimafanikio.
Usipokuwa makini na kuwa mkomavu hapa utaharibu kila kitu. Fanya vitu vitakavyokupa furaha na mafanikio tena ila achana na watu hasi ambao hawatakusaidia zaidi ya kukurudisha nyuma kimafanikio
.7. Acha kusimama endeleza mipango na malengoyako tena.
Wapo watu ambao mambo yao yanapokwenda hovyo huwa ni watu wa kusimama na kuacha malengo yao kwa muda na kusikilizia maumivu. Kama una tabia hii nakushauri achana nayo mara moja kwani itakuchelewesha katika safari yako muhimu ya mafanikio.
Mambo yanapokwenda hovyo kaa chini ,tafakari, kisha nyanyuka na chukua hatua mara moja ya kusonga mbele.Muda ulionao ni mchache sana, ukisubiri sana na kusikilizia maumivu uliyonayo utachelewa, elewa Dunia inakwenda kwa kasi kuliko unavyofikiri.
Hivyo ndivyo vitu muhimu unavyotakiwa kukumbuka wakati mambo yako yanapokwenda vibaya. Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya ukombozi wa maisha  na endelea kutembelea mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kwa kujifunza mengi.
TUPO PAMOJA!

IMANI  NGWANGWALU- O767 048 035/ingwangwalu@gmail.com