Katika sehemu iliyopita ya uchambuzi tuliona jinsi ambavyo Robert na Mike walikubali kufanya kazi ili wafundishwe jinsi ya kuwa matajiri. Lakini pamoja na kufanya kazi kwa ujira kidogo bado hawakupata kile walichetegemea kupata. Na hii ilimfanya Robert kuamua kuacha kazi ile kwa sababu hakuona chochote alichojifunza. Hapa ndipo alipokutana na RICH DAD ambapo alimpa somo la kwanza na muhimu sana kwenye maisha ya kila mtu ambaye anataka kujua jinsi ya kutengeneza fedha.
RICH DAD aliendelea kumweleza Robert ni jinsi gani maisha yanavyowasukuma watu ndio wengine wanajifunza na wengine wanakata tamaa. Alimwambia Robert kama atajifunza somo hilo muhimu ataishi maisha yenye uhuru wa kifedha na kusahau shida. Ila kama hatajifunza somo hilo ataishi maisha magumu ya kulaumu kazi, mshahara kidogo au bosi wake kwa maisha magumu. Na kama hatokuwa na uvumilivu atakata tamaa mapema na kukubali maisha magumu yanavyokwenda na kufa masikini.
Robert alimuuliza kwa hiyo ulikuwa unanijaribu? Rich dad alimwambia ni kama alikuwa anafanya hivyo. Alimwambia yeye Robert na Mike ndio watu wa kwanza kuw atahi kumfuata na kumuuliza awafundishe jinsi ya kupata fedha. Alisema ana wafanyakazi zaidi ya 150 lakini hakuna hata mmoja amewahi kumfuata na kumuuliza amfundishe mbinu za kuwa tajiri. Wote wanafanya kazi na kulalamikia mshahara kidogo au kumlaumu yeye kwa maisha yao magumu, na maisha yao yanaendelea kuwa magumu hata pale mshahara unapoongezeka. Wanatumia maisha yao yote kufanyia kazipesa bila ya kujua ni jisni gani pesa inapatikana.
Robert alimuuliza ni somo gani ambalo ulitaka kutufundisha hapa kwa kutufanyisha kazi kwa ujira kidogo wa senti kumi kwa saa. Rich dad akamwambia badili mtazamo wako na acha kunilaumu mimi, kama unafikiri mimi ndio tatizo utataka kunibadili mimi, lakini kama ukijua wewe mwenyewe ndio tatizo utajifunza na kukua zaidi kimaarifa. Rich dad alimwambia kama ukiendelea kuamini mimi ni tatizo utaishia kunilaumu mimi, ila ukiamini wewe mwenyewe ni tatizo utajifunza na kuweza kutatua tatizo hilo.
Robert akamwambia kama ni hivyo basi kwa kuwa unanilipa fedha kidogo nitaacha kazi. Rich dad akamwambia hivyo ndivyo wanavyofanya watu wengi. Wanapoona mshahara ni kidogo na kufikiri mwajiri wao ndio tatizo wanaacha kazi na kwenda kutafuta nyingine. Huko wanakokwenda nako wanakuta mambo ni magumu vile vile. Robert akamuuliza kwa hiyo nifanye nini, nikubali malipo haya kidogo? Rich dad akamwambia hivyo ndivyo wanavyofanya watu wengi pia, wanakubali kidogo wanachopata, wanaishi maisha magumu na familia zao huku wakiamini kwamba kama mshahara utaongezeka basi maisha yao yatakuwa bora.
Robert alianza kulielewa somo lile na akamuuliza RICH DAD, sasa ni kitu gani kitatatua tatizo hili? Rich dad aliweka mkono kwenye kichwa chake na kumwambia hiki kilichopo ndani ya kichwa chako ndio kitakusaidia kutatua tatizo hili. Rich dad alimwambia kitu kimoja ambacho kinamtenganisha yeye na wafanyakazi wake au na watu wengine ambao ni masikini ni kitu kimoja muhimu ambacho ni MATAJIRI HAWAFANYII KAZI FEDHA. Na hili ndio somo la kwanza kati ya masomo sita tutakayojifunza kwenye kitabu hiki.
Tofauti kati ya baba tajiri(RICH DAD) na baba masikini(POOR DAD)
Siku hii ambapo Robert alijifunza somo la kwanza kwamba matajiri hawafanyii kazi fedha aliona tofauti kubwa sana kati ya baba zake hawa wawili. Baba yake mzazi ambaye alikuwa masikini alimsisitiza aende shule asome kwa bidii ili afaulu vizuri kisha atapata kazi nzuri itakayomlipa vizuri. Wakati baba tajiri alimwambia ajifunze jinsi fedha zinavyofanya kazi na aweze kuzitumia zimfanyie yeye kazi.
Rich dada aliendelea kumfundisha somo la kwanza na alimwambia Robert anafurahi kwamba hakukubali kuendelea kulipwa kidogo kwa sababu kukataa kwake kule ndio kutakompelekea kujifunza zaidi na kuweza kupata kipato kikubwa zaidi. Alimwambia kinachowafanya watu wengi wakubali kufanya kazi yenye maslahi kidogo ni hofu. Wengi wana hofu kwamba bila kazi hiyo maisha yatakuwa magumu, hawatapata chakula, hawataweza kulipa kodi za nyumba na mengineyo. Na hofu hii ndio inawafanya watu waendelee kunyonywa kwenye ajira. Rich dad aliendelea kumwambia kwamba hofu hii ndio inawafanya watu walalamike kwamba yeye anawanyonya wafanyakazi wake, wakati wao ndio wanajinyonya wenyewe kwa hofu zao. Robert alimuuliza kwa nini asiwalipe zaidi, Rich dad akamjibu sina wajibu wa kufanya hivyo na akamwambia hata nikiwalipa zaidi bado matatizo yao hayataisha. Alimwambia chukua mfano wa baba yako(POOR DAD), amesoma sana na analipwa mshahara mkubwa, ila bado anashindwa kulipa gharama zake za maisha.
Alimwambia watu wanavyozidi kupata kipato kikubwa ndio wanavyozidi kuingia kwenye madeni. Hii ni kwa sababu wanakuwa hawajajifunza ni jinsi gani fedha zinafanya kazi. Na wengi wanaamini inabidi wafanye kazi kwa ajili ya kupata fedha na wakishazipata wanatumia wakati mwingine zaidi hata ya wanazopata. Rich dad alimwambia robert kama anataka kujifunza jinsi ya kufanyia kazi fedha basi aendelee kujifunza kwenye mfumo wa elimu. Ila kama anataka kujifunza jinsi ya kuifanya fedha imfanyie kazi basi yeye atamfundisha kama atakuwa tayari kujifunza. Alimwambia wengi hawapendi kujifunza jinsi ya kufanya fedha ziwafanyie kazi na hivyo kuendelea kuwa watumwa wa kazi.
Rich dad alimwambia wanaojifunza jinsi ya kuifanyia kazi fedha wanaishi maisha magumu kwa sababu wanafanya kazi kwa shida na mwisho wa mwezi wanapokea mshahara ambao bado hautoshelezi mahitaji yao. Mbaya zaidi mshahara huo unakuwa na makato mengi na hivyo kupokea kidogo zaidi. Pamoja na yote hayo bado hawajifunzi na badala yake wanaendelea kulalamika. Rich dad alimwambia kwamba yeye ana kipato kikubwa kuliko Poor dad ila poor dad analipa kodi kubwa kuliko yeye. Robert alishangazwa sana na mambo haya. Na alielewa vizuri kwa sababu kila mara alimwona baba yake akilalamika kipato hakitoshi na kodi ni kubwa.
Tunajifunza nini kwenye sehemu hii?
Kuna mambo mengi sana ya kujifunza hapa ambapo kama utaanza kuyafanyia kazi utaona mabadiliko makubwa kwenye maisha yako;
1. Ili kuwa tajiri na kufikia uhuru wa kifedha ni lazima uache kuifanyia kazi fedha na uifanye fedha ikufanyie kazi wewe.
2. Unapokuwa na kipato kidogo tatizo haliko kwenye yule anayekupa kipato hiko bali lipo kwako mwenyewe.
3. Maisha yanapokuwa magumu ndio wakati wa kujifunza kuliko kulalamika na kukata tamaa.
4. Kama una maisha magumu na fedha ni kidogo kwako, kuongezewa fedha hakutotatua tatizo lako la fedha bali ndio litazidi kuongezeka.
5. Mfumo wa elimu unatufundisha kufanyia kazi fedha badala ya kinyume chake ambapo elimu hii inapatikana kwenye maisha.
6. Watu wengi ni watumwa kwenye kazi ambazo haziwapi kipato cha kutosha kutokana na hofu kubwa waliyojijengea.
7. Utatuzi wa changamoto zote hizi uko ndani ya kichwa chako, anza kuutumia sasa.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio.
TUKO PAMOJA, TUKUTANE KILELENI.
Asanteee kwa makala nzuri
Tuko pamoja
LikeLike
Asante na wewe pia kwa kujifunza.
Karibu sana, TUKO PAMOJA.
LikeLike
kaka Mungu na akuzishie ufahamu,
LikeLike
Asante sana Godlove,
TUKO PAMOJA.
LikeLike
Kocha Amani Makirita, asante kwa uchambuzi makini ninaendelea kufuatilia uchambuzi huu kwa sababu ninajifunza mengi yanayoendelea kubadili maisha yangu.
LikeLike
Vizuri sana.
Kila la kheri katika kufanyia kazi yale uliyojifunza.
LikeLike