Unapokuwa mjasiriamali hakuna kiwango cha mwisho cha mafanikio unachoweza kufikia, hii ina maana kwamba unaweza kufikia mafanikio makubwa zaidi ya hayo uliyonayo sasa. Tofauti na mwajiriwa ambaye mshahara wake unajulikana na hata ka autaongezeka ni kidogo sana, mjasiriamali unapanga kipato chako mwenyewe na hivyo unaweza kukiongeza bila ya kuomba au kuzuiwa na mtu yeyote. Lakini pamoja na uhuru huu mkubwa wa kuweza kufikia mafanikio makubwa sana, bado wajasiriamali wengi wanashindwa kufikia mafanikio makubwa. Inawezekana wewe ni mmoja wa wajasiriamali ambao umekuwa na hamu kubwa ya kufikia mafanikio lakini unashindwa kufikia.
Leo tutajifunza mambo matano ambayo yanawazuia wajasiriamali wengi kufikia mafanikio makuwa na jinsi unavyoweza kuepuka au kujirekebisha.
1. Kutokuweka malengo makubwa.
Hakuna kitu kizuri kama kuweka malengo kwenye maisha. Ni kupitia malengo ndio utaweza kujua kama unakwenda mbele au unarudi nyuma, kama upo kwenye njia sahihi au unapotea. Wewe kama mjasiriamali ni muhimu kuwa na malengo ya muda mrefu na ya muda mfupi. Na pia malengo hayo yawe makubwa na yakusukume kufanya kazi zaidi ili kuweza kuyafikia. Weka malengo ya miaka kumi. mitano, miwili, mmoja na pia weka malengo ya kila mwezi na kila wiki. Baada ya kuweka malengo weka mipango itakayokufikisha kwenye malengo hayo na anza kuifanyia kazi mipango hiyo mara moja.
2. Kutokujifunza kila siku.
Ni muhimu sana kujifunza kila siku ili kuweza kufikia mafanikio makubwa. Jifunze kutoka kwenye uzoefu wako mwenyewe, jifunze kutoka kwa wengine na muhimu zaidi jifunze kwa kujisomea. Kila siku hakikisha unajifunza kuhusiana na kile unachofanya. Utakapokijua vizuri kile unachofanya utakuwa na uwezo mkubwa wa kukifanya kwa ubora wa hali ya juu na hii itakusaidia kufikia mafanikio makubwa.
3. Kuridhika haraka.
Baadhi ya wajasiriamali huridhika haraka kwa mafanikio kidogo wanayopata. Huona kama wamefanya kitu kikubwa sana na hivyo kujisahau na kuacha kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuacha kujifunza. Hali hii hupelekea ukuaji wao kudumaa na kushindwa kufikia mafanikio makubwa. Endelea kuwa na njaa ya mafanikio hata pale unapopata mafanikio. Njaa ya mafanikio ndio itakayokuwezesha kufikia mafanikio makubwa zaidi ya hayo uliyonayo sasa. Siku utakayoanza kuona umefikia mafanikio makubwa sana na huwezi kuendelea zaidi, ndio siku utakayoanza kuporomoka.
4. Matumizi mabovu ya fedha.
Fedha ndio damu ya biashara yoyote ile, kama isipoangaliwa na kutumiwa vizuri inaweza kupelekea biashara kufa. Matumizi mabovu ya fedha imekuwa kikwazo kikubwa sana kwa wajasiriamali kuweza kufikia mafanikio makubwa. Kushindwa kujua ni faida kiasi gani unapata kutokana na ujasiriamali unaofanya na pia kuingia kwenye madeni yasiyo ya muhimu kunaweza kukufanya ushindwe kufikia mafanikio makubwa. Jifunze kuwa na matumizi mazuri ya fedha zako na utaona mafanikio makubwa sana kupitia ujasiriamali wako.
5. Matumizi mabovu ya muda.
Muda ndio kitu ghali kushinda vitu vyote duniani. Kila mtu ana masaa 24 tu kwa siku, hakuna awezaye kutengeneza muda zaidi ya hapo hata awe na fedha kiasi gani. Kama ukitumia muda wako vibaya na ukapotea hutaweza kuupata tena, yaani haurudi tena. Jua ni vitu gani vina uzalishaji mkubwa na vinahitaji sana muda wako na acha kufanya mambo yanayokupotezea muda. Pia jua thamani ya muda wako ili unapopotea ujue ni kiasi gani cha fedha unapoteza.
Wewe kama mjasiriamali mafanikio yako yapo kwenye mikono yako. Unapokuwa na malengo na mipango mizuri, ukajifunza kila siku kile unachofanya na kufanya kazi kwa bidii hakuna kitakachokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Unaweza kufikia mafanikio makubwa sana zaidi ya uliyonayo sasa, amua sasa na anza kufanyia kazi maamuzi yako ili ufanikiwe.
Nakutakia kila la kheri kwenye biashara au ujasiriamali unaofanya.
TUKO PAMOJA.