Siku chache zilizopita kulikuwa na habari moja iliyokuwa inazunguka kwenye mitandao kuhusu mtangazaji mmoja maarufu aliyeamua kujiuzulu kazi. Licha tu ya kujiuzulu aliamua kuweka barua yake ya kujiuzulu kwenye mitandao na kuwaambia watu kwamba hayo ndio maamuzi aliyochukua.
Nilipata bahati ya kuiona barua yake hiyo na nimeona kuna mengi ya kujifunza kutokana na habari hii. Pamoja na kwamba baadhi ya watu walimlaumu kwa kitendo chake cha kuweka barua hiyo hadharani, sisi hatutaangalia huko, tuangalie ni kipi cha kujifunza hapa. Na pia sitataja jina kwa kuwa hapa hatujadili usahihi au makosa aliyofanya bali tunajifunza kutokana na hili.
Kabla hatujaendelea barua yenyewe ni hii hapa;
Kama ulivyoona kwenye picha hapo juu mtangazaji huyu alifanya kazi kwenye shirika husika kwa miaka kumi na nne(14). Pamoja na miaka yote hii sababu kubwa iliyomfanya kujiuzulu kazi ni maisha magumu(gharama kubwa za maisha) na hivyo kwenda kutafuta njia mbadala kama alivyoandika kwenye barua yake.
Tunaona ni jinsi gani ajira za Tanzania zilivyokuwa na matatizo, kwa sababu kwa miaka kumi na nne mtu anaendelea kuvumilia tu na mwishowe mambo yanamshinda kabisa. Iwe sababu hii ndio hasa iliyomfanya kujiuzulu au kuna sababu nyingine, bado ajira za Tanzania zina tatizo kubwa.
Je na wewe unasubiri miaka kumi na nne?
Kama upo kwenye ajira unasubiri nini? Miaka iendelee kwenda ukiamini siku moja mambo yatakuwa vizuri?
Kama ndio unasubiri hiko umeshaumia ndugu yangu. Kama kazi yako kwa sasa haikuridhishi au kipato hakikutoshi, kuendelea kuing’ang’ania hakutakupatia nafuu yoyote. Sana sana utaendelea kutumikia fedha na usijue maisha yako yanaelekea wapi.
Katika uchambuzi wa kitabu cha RICH DAD POOR DAD unaoendelea kwenye KISIMA CHA MAARIFA, Rich Dad alimwambia Robert, tatizo kubwa la wafanyakazi wanapoona kipato hakiwatoshi huanza kumlaumu bosi au mwajiri wao. Na hata pale kipato kinapoongezwa ndio wanazidi kuingia kwenye madeni.
Unaweza kukataa hili? Ni mara ngapi mshahara umeongezwa tangu umeanza kazi ila maisha ndio yanazidi kuwa magumu? Hii ni kwa sababu hujui tatizo hasa ni nini na hivyo unaishia kumlaumu mwajiri au mazingira kutokana na hilo.
Na hiki ndicho alichokifanya mtangazaji huyu, baada ya kuondoka kwa mwanzo amekwenda kuajiriwa kwingine. Sasa hivi anaweza kuona mambo yatakuwa mazuri, ila kama hajajipanga au hajajua tatizo hasa linaanzia wapi ataishia kwenye hali ngumu kama kule alikotoka mwanzo.
Hivi ndivyo ajira zilivyo, zimekosa adabu.
Sasa ufanye nini kwa wewe ambaye upo kwenye ajira?
Kama wewe ndio mfanyakazi na umekuwepo kwenye kazi kwa muda sasa ila kila siku maisha yanazidi kuwa magumu ufanye nini?
Kuna mambo mengi sana unayoweza kuanza kufanya leo hii ambayo yatabadili hali hii siku zijazo, sitaweza kueleza yote hapa ila cha kwanza ambacho nitakushauri ufanye ni KUJIUNGA NA KISIMA CHA MAARIFA(bonyeza hayo maneno kupata utaratibu wa kujiunga). Fanya hivyo mapema sana na ukiwa huko utajifunza jinsi ya kuweza kuanza kuweka akiba hata kama una kipato kidogo na jinsi gani uanze kuwekeza na kuongeza thamani ya fedha zako hata kama haupo tayari kuacha kazi kwa sasa.
Ndani ya KISIMA utaboresha maisha yako na utaacha kumlaumu mwajiri au bosi wako na kuanza kuchukua hatua.
Usikubali kuendelea kuishi maisha ya matamanio, una uwezo mkubwa zaidi ya unaotumia sasa, una thamani kubwa kuliko unavyolipwa sasa, tatizo ni kwamba hujajua na kwa kuwa hujajua unaendelea kutumiwa na kuwa mtumwa.
Kama unahitaji la kweli la kujiunga na kisima cha maarifa ila gharama zinakushinda kwa sasa wasiliana nami kwa email amakirita@gmail.com na tutaweka utaratibu mzuri sana wa jinsi ya kufanya malipo yako.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya mafanikio.
TUKO PAMOJA, TUTAKUTANA KILELENI