Kwa miezi miwili sasa, kila siku ya jumatano tumekuwa tukikuletea makala ya ushauri kwa wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu. Katika miezi hii miwili tumejifunza mambo mengi sana na kama umeanza kuyatumia utaona mabadiliko makubwa sana siku za mbeleni.

Kama hukupata nafasi ya kujifunza katika makala zilizopita unaweza kuzisoma makala zote hapa kwa kubonyeza maandishi haya.

Leo ndio siku ya mwisho kwa makala hizi za ushauri kwa wahitimu. Utaendelea kujifunza mambo mengine mengi kupitia AMKA MTANZANIA na pia KISIMA CHA MAARIFA.

wahitimu

Leo nataka nikukumbushe kwamba kuna uwezo mkubwa sana ambao uko ndani yako. Uwezo huu ni mkubwa sana zaidi ya unavyoutumia sasa. Na huenda hujapata nafasi ya kusikia hili kwa sababu katika mfumo wa elimu, uwezo wako ulikuwa unalinganishwa na wa  wengine kupitia mitihani.

Sasa ndio umepata nafasi ya kuonesha uwezo huu mkubwa ulioko ndani yako. Uwezo huu mkubwa uliko ndani yako ndio utakaokuwezesha kufikia mafanikio makubwa sana kwenye maisha yako.

Unawezaje kutumia uwezo huu mkubwa kufikia mafanikio makubwa?

Kama wewe ni msomaji mzuri wa AMKA MTANZANIA utakuwa umejifunza kuhusiana na hili kwenye makala nyingi sana zilizopita. Ila kama sio msomaji au hujaelewa vizuri unawezaje kuanza kutumia uwezo wako kufikia mafanikio makubwa nitaeleza hapa kwa ufupi.

Hapa nitaeleza mambo kumi au hatua kumi muhimu za kufuata ili kuweza kuishi maisha yenye mafanikio makubwa kwa kutumia uwezo mkubwa ulioko ndani yako.

1. Chagua kitu kimoja unachotaka kufanya kwenye maisha yako. Usifikiri unaweza kufanya kila kitu, huna muda huo na hata ukijaribu utagusa juu juu tu na hutapata mafanikio makubwa. Hivyo andika mahali sasa hivi kwamba unataka kufanya nini kwenye maisha yako.

2. Weka malengo na mipango kwenye maisha yako. Usiishi tu kama watu wengine wanavyokwenda, weka malengo ambayo yatakufikisha mbali zaidi.

3. Jifunze kila kitu unachoweza kuhusiana na kitu hiko ulichochagua kufanya. Soma vitabu, soma majarida, soma mitandao, onana na wataalamu na kadhalika, kuwa na njaa kali sana ya kujifunza kitu hiko.

4. Anza kufanyia kazi kitu hiko ulichochagua, anza kidogo, kutambaa ni bora kuliko kukaa. Acha kabisa kutumia zile sababu zinazotumiwa na walioshindwa au wanaoelekea kushindwa,

5. Usimlaumu au kumlalamikia mtu yeyote, kama kuna jambo hulipendi au hulitaki libadilishe, kama huwezi achana nalo na uendelee na mengine yenye maana kwako.

6. Jitofautishe na wengine, kuwa wa kipekee na usifuate kundi. Ukianza kuiga yale yanayofanywa na wengine utaishia kuwa wa kawaida kwa sababu watu wengi ni wa kawaida. Ila kwa kuwa wewe unataka kufikia mafanikio makubwa unahitaji kuwa wa kipekee.

7. Kuwa mbunifu, kila mmoja wetu ni mbunifu, na hata wewe ni mbunifu. Tumia ubunifu wako kuweza kufanya mambo ya kitofauti ili uweze kufikia mafanikio makubwa.

8. Amka mapema kila siku na upate muda wa kujifunza kwa kujisomea, kupangilia siku yako na hata kutafakari malengo ya maisha yako.

9. Tengeneza bahati yako mwenyewe. Kama mpaka sasa unaamini walifanikiwa walipata bahati basi uko kwenye njia ambayo sio sahihi. Hakuna bahati inayokuja tu, bahati inatengenezwa. Na ili uweze kutengeneza bahati yako fanya maandalizi ya kutosha, kabla hujakutana na fursa.

10. Kuwa na mtizamo chanya. Kushinda au kushindwa kunaanzia ndani yako. Kama unaamini unaweza au utafanikiwa hilo ndio litatokea. Kama unaamini huwezi au utashindwa hilo ndio litakalotokea. Hata ukifanyiwa kitu gani, utapata majibu yale uliyotengeneza kwenye kichwa chako. Kuwa makini na fikra zako, zinaweza kuwa sumu kwako.

Naamini kwa haya machache utaendelea kujifunza zaidi ili uweze kufikia mafanikio makubwa zaidi. Pia nikukaribishe sana kwenye KISIMA CHA MAARIFA ili uweze kujifunza kila siku na kuweza kufikia mafanikio makubwa. Kujua JINSI YA KUJIUNGA NA KISIMA CHA MAARIFA bonyeza maandishi hayo na utapata utaratibu.

Nakutakia kila la kheri katika safari hii ya mafanikio uliyoianza. Kumbuka safari hii haina mwisho na kila siku ni kujifunza.

TUKO PAMOJA KWENYE SAFARI HII, TUTAKUTANA KILELENI.