Kila mmoja wetu anapenda kupata mafanikio kwenye maisha. Tunataka kubobea kwenye kile tunachofanya na pia tunataka kupata fedha nyingi kwa kile tunachofanya. Lakini sio watu wote ambao wanafikia mafanikio makubwa katika mambo wanayofanya. Ni wachache sana wameweza kufikia mafanikio ya ngazi za kimataifa yaani world class.

Ni kitu gani kinawafanya watu wachache kuweza kufikia mafanikio makubwa sana huku wengi wakiendelea kuteseka na kushindwa kufika huko? Je wanaofikia mafanikio makubwa walizaliwa na bahati? Je waliumbwa tofauti na wengine? Majibu yote ni hapana, wanaofikia mafanikio ni watu wa kawaida kama sisi, na wengine wameanzia chini kuliko hata sisi.

Kitu kikubwa kinachowatofautisha wanaofikia mafanikio makubwa na wanaokuwa kawaida sio tofauti ya kuumbwa au uwezo bali ni tofauti ya mambo wanayofanya. Ukiangalia kwa makini watu waliofikia mafanikio makubwa wanafanya mambo tofauti na watu wengine ambao wanashindwa kufikia mafanikio makubwa.

Sasa leo hii utayajua mambo 30 unayotakiwa kuanza kufanya leo kama bado huyafanyi ili uweze kufikia mafanikio makubwa sana. Mambo mengi tutakayojadili hapa tulishayajadili mara kwa mara, hapa utayapata yote kwa pamoja. Kumbuka kufikia mafanikio makubwa haijalishi ni kazi gani unafanya, bali juhudi zako na mipangilio yako. Hivyo kwa kazi au shughuli yoyote unayofanya sasa, au unayotarajia kuanza kufanya una uwezo mkubwa wa kufikia mafanikio makubwa sana.

Haya hapa ndio mambo 30 unayotakiwa kufanya ili kufikia mafanikio makubwa;

1. Jua ni kitu gani unataka kwenye maisha na kwenye kile unachofanya. Baada ya kujua hilo, weka malengo na mipango itakayokufikisha pale unapotaka kufika.

2. Kumbuka kila tatizo lina suluhisho, kama kuna kitu kinakushinda sasa ni kwamba hujajua suluhisho lake ni nini. Na kila mtu ana tatizo ambalo linahitaji kutatuliwa. Jinsi utakavyoweza kutatua matatizo ya watu wengi, kupitia kile unachofanya ndivyo unavyoweza kufikia mafanikio makubwa.

3. Unahitaji utulivu mkubwa sana kwenye dunia ya sasa ambayo ina usumbufu wa kila aina. Kuwa na muda wako mwenyewe wa kufanya mambo ambayo yatakupatia mafanikio makubwa.

4. Kabla hujasaidiwa inabidi usaidie wengine. Kwa maneno mengine kabla hujapokea inabidi utoe, usiseme huna cha kutoa, kila mtu anacho cha kumpa mwingine.

5. Penda sana kile unachokifanya, kama hukipendi huwezi kufikia mafanikio makubwa. Naweza kusema kipende sana zaidi ya watu wengine wote wanavyokipenda.

6. Jua vizuri kile unachofanya, yaani kijue nje ndani kushinda watu wote wanavyokijua dunia nzima. Jifunze kila siku na yatumie yale unayojifunza kuendeleza utaalamu wako.

7. Amka asubuhi na mapema, huu ni muda mzuri sana wa kufanya mambo yako au kujifunza kwa kujisomea. Ni muda ambao hauna usumbufu, hakuna atakayekupigia simu na pia hakuna atakayetaka kukuuliza chochote. Wakati huu dunia nzima imelala, na wewe unafanya kazi hivyo unaishinda dunia nzima. Hakikisha unapata masaa mawili asubuhi kabla ya kuondoka kwenda kwenye shughuli zako za kila siku. Masaa haya mawili yatumie kujisomea, kutafakari, kupanga siku, kupitia malengo, kufanya mazoezi na mambo mengine yatakayokusaidia kufikia mafanikio makubwa.

8. Jitoe kujifunza kitu kipya kila siku kuhusiana na kazi au shughuli unayofanya. Mafanikio makubwa yanapatikana kwa wale wanaojifunza kila siku, jinsi unavyojua zaidi ndivyo unavyoweza kufikia mafanikio makubwa zaidi.

9. Usiangalie simu yako wakati una mkutano muhimu na mtu, ni ukatili na watu wakatili hawafikii mafanikio makubwa. Fanya kitu kimoja kwa wakati mmoja, simu isikuzuie kufanya mambo yako muhimu.

10. Kila mara fanya jambo ambalo unaogopa kulifanya kwenye shughuli zako. Mambo haya ndio yanayokuzuia wewe kufikia mafanikio makubwa. 

11. Tatizo ni tatizo pale tu unapoamua kulichukua kama tatizo, vinginevyo inakuwa ni changamoto tu na utaweza kuitatua.

12. Acha kulalamika na kulaumu wengine. Uko hapo ulipo kutokana na maamuzi ambayo uliyafanya mwenyewe, kama unataka mabadiliko anza kuchukua hatua. Usilalamikie wazazi, mwajiri, mshirika kwenye biashara au serikali kwa tatizo lolote unalopata. Ukifanya hivyo huwezi kufikia mafanikio makubwa.

13. Tafuta mtindo wako mwenyewe, kuwa wa kipekee na usiige(usikopi na kupesti). Kila aliyefikia mafanikio makubwa aliweza kujitofautisha na watu wengine.Kimbia mbio zako mwenyewe na usifuate kundi, hivi ndivyo unavyoweza kuwa tofauti na kufikia mafanikio makubwa.

14. Kumbuka una uwezo mkubwa kuliko unaotumia sasa na pia unathamani kubwa kuliko unayolipwa au kutengeneza kwa sasa. Kupata mafanikio makubwa zaidi ya unayopata sasa, tumia uwezo mkubwa ulio ndani yako kuliko unavyoutumia sasa.

15. Kama hujajiandaa vya kutosha, hujajiandaa kabisa. Usiwe vuguvugu, kuwa moto sana ili kile unachokifanya ukifanye kwa viwango vya juu sana.

16. Pale unapofikiri kwamba unajua kila kitu ndio hujui chochote. Pale unapofikiri umemaliza ndio kwanza unaanza. Mafanikio hayana mwisho.

17. Unapofikia mafanikio ndio inabidi uzidi kuwa na njaa ya kujifunza zaidi na kuendelea kufanya zaidi. Mafanikio yanalevya, ni rahisi kusahau yale yaliyokufikisha kwenye mafanikio na hatimaye ukashindwa vibaya sana. Hiki ndio kinachotokea kwa wale ambao walikuwa na mafanikio makubwa na ghafla wakaanza kushuka, walisahau kuendelea kufanya yale yaliyowafikisha kwenye mafanikio hayo.

18. Kupata mafanikio mara mbili ya unayopata sasa, fanya mara mbili ya unavyofanya sasa. Ni rahisi kama hivyo, anza kufanya hivyo leo na utaona mabadiliko makubwa.

19. Wekeza kwenye maendeleo yako binafsi, watu wote waliofanikiwa sana wanafanya hivi. Soma na sikiliza vitabu, hudhuria semina mbalimbali na pia pata mafunzo yanayohusiana na kile unachofanya.

20. Hupati bahati bali unatengeneza bahati. Hivyo kama unataka kuwa na bahati jiandae vya kutosha.

21. Pata muda wako mwenyewe kila siku, katika muda huu ndio unaweza kupatamawazo mazuri yatakayokuwezesha kufikia mafanikio makubwa.

22. Tafakari siku yako kabla ya kulala kila siku, andika yale uliyofanikisha na pia andika yale uliyoshindwa na nini utarekebisha ili kupata matokeo mazuri zaidi siku inayofuata.

23. Kama hakuna wanaokupinga au kukushangaa kwa mambo unayofanya, hakuna kikubwa unachofanya na huwezi kufikia mafanikio makubwa. Ili uweze kufikia mafanikio makubwa ni lazima uwe tofauti na wengine na ukiwa tofauti kuna watakaokupinga na wengi watakushangaa kwa yale unayofanya, kama mpaka sasa hakuna wanaokupinga au kukushangaa haupo kwenye njia ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa.

24. Pata muda wa kutosha wa kupumzika, itakusaidia kupata nguvu za kuweza kufanya mambo ambayo ni muhimu kwako kufikia mafanikio makubwa.

25. Nunua tv ndogo, kuwa na maktaba kubwa. Kwa maneno mengine tumia muda mdogo sana kwenye kuangalia tv na tumia muda mwingi sana kwenye kusoma na kujifunza. Hivi ndivyo wanavyofanya waliofikia mafanikio makubwa.

26. Kumbuka jinsi unavyoweka malengo makubwa ndivyo unavyozidi kukua na kuwa imara pale unapofikia malengo hayo. Acha kujishusha na kujidumaza kwa kuweka malengo madogo, hayana msaada wowote kwako.

27. Maliza chochote unachoanza na kimalize vizuri hata kama ni kigumu kiasi gani. Kuna mambo mengi sana utakayojifunza.

28. Linda sana jina lako, ni uwekezaji mzuri sana kwako. Heshima yako ni muhimu ili uweze kufikia mafanikio makubwa. Usiipoteze kwa mambo ambayo hayana msaada kwako na hata kwa wengine.

29. Kwenye shughuli unayofanya lenga kuwa wa kipekee, usitake kuwa wa kawaida tu. Weka historia kwa jinsi unavyofanya mambo yako kwa utofauti. Kama unafanya biashara mpe mteja wako huduma nzuri ambayo hajawahi kuipata kokote, itakulipa sana.

30. Mashaka yako ni uongo kwako, hofu zako ni usaliti kwako. Usikubali vitu hivi viwili vikurudishe nyuma katika safari yako ya kufikia mafanikio makubwa.

NYONGEZA; Kumbuka unao uwezo wa kuibadili dunia, kwa kazi au biashara yoyote unayofanya una nafasi kubwa sana ya kuibadili dunia na kuwa sehemu bora zaidi. Anza kufanya hivyo kwa tendo moja moja na kwa mtu mmoja mmoja, baada ya muda utaona jinsi ambavyo utakuwa umeleta mabadiliko kwenye maisha ya watu wengi.

Wewe ni mshindi, wewe utafikia mafanikio makubwa sana. Kumbuka mambo haya na yapitie kila siku na uyatekeleze kwenye maisha yako. Utafikia mafanikio makubwa sana na kuweza kuibadili dunia.

Najua unaweza, naamini utafanya hivyo.

TUKO PAMOJA KATIKA SAFARI HII NA TUTAKUTANA KILELENI, HAKUNA TUTAKAYEMUACHA.