Ili uweze kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako ni lazima uweze kuishinda hofu ya kushindwa. Kupata furaha, mapenzi, mafanikio, utajiri, ushawishi, umaarufu na hata chochote unachotaka hatua ya kwanza ni kuishinda hofu ya kushindwa.
Hatua ya kwanza ya kushinda hofu ya kushindwa ni kuelewa kwamba kushindwa ni kitu ambacho kinatokea kila siku na kwa kila mtu. Sababu kubwa inayowafanya wengi kushindwa kabisa ni kufikiri kwamba hofu ni kitu ambacho kinatakiwa kukwepwa. Wanajaribu kuepuka hofu na hivyo hawajaribu kufanya chochote na moja kwa moja wanakuwa wameshindwa.
Jinsi mtu anavyokuwa na hofu ya kushindwa ndivyo anavyokaribisha kushindwa. Hofu ya kushindwa inakuhakikishia kushindwa.
Kwa nini watu wengi wanashindwa?
1. Wanafikiri kushindwa ni kitu cha kuepuka.
2. Wanaona aibu kushindwa
3. Wanaona kushindwa kama laana au kisirani.
4. Wanakatishwa tamaa na kushindwa.
5. Wanapaniki wanapokutana na kushindwa.
6. Wanaacha kujaribu kwa kuogopa kushindwa.
Jinsi ya kutumia kushindwa ili kufikia mafanikio makubwa.
Kila mara unaposhindwa kukamilisha au kufikia kitu fulani ulichotaka unakuwa umepiga hatua kuelekea kwenye mafanikio. Kushindwa sio mwisho wa safari ya mafanikio bali ni vizingiti kwenye safari ya mafanikio
Kushindwa ni sehemu muhimu na isiyokwepeka ili kufikia mafanikio. Unajifunza mambo mengi sana kwenye kushindwa kuliko kwenye kushinda. Unaposhindwa unajua ni kitu gani hutakiwi kufanya hivyo unabaki na vile ambavyo ukivifanya utafikia mafanikio makubwa.
Kitu kikubwa cha kukumbuka ni kwamba hutakiwi kushinda mara zote, hutakiwi kushinda kila mara bali unatakiwa kushinda mara kadhaa ambazo zitakufikisha kwenye mafanikio makubwa. Hivyo unaposhindwa ni njia ya kuelekea kwenye mafanikio.
Unaposhindwa tumia kama sehemu ya kujifunza, usikate tamaa na wala usitafute visingizio vya nje. Anza na wewe mwenyewe ni vitu gani umefanya vikakufikisha kwenye kushindwa ukishavijua vitu hivi jirekebishe ili usirudie tena. Wale wanaoshindwa moja kwa moja hutafuta sababu na kuanza kulaumu pale wanaposhindwa. Hii huwafanya waamini wao hawana mchango wowote kwenye kushindwa kwao na hivyo kurudia makosa yale yale yaliyowapelekeankushindwa.
Kikubwa unachotakiwa kukumbuka wakati wote ni kushindwa sio kitu cha kuhofiwa bali ni kitu cha kupendwa ili uweze kujifunza na kuendelea.
Jinsi ya kuishinda hofu ya kushindwa.
Hofu imeleta matatizo mengi sana kwa watu zaidi ya kitu kingine chochote. Hofu ndio hisia rahisi sana kwa binadamu kuifuata. Mara nyingi hofu ya kushindwa huja na picha fulani kwenye akili zetu. Picha hizi hutuonesha ni jinsi gani hali inaweza kuwa mbaya kama tukishindwa kwa kile tunachofanya. Picha hizi hutuogopesha na kutufanya tusichukue hatua. Ili kuondoa hofu ya kushindwa unaweza kufanya mambo haya mawili;
1. Ondoa mawazo yenye picha za kushindwa.
Akili yako ya ndani(subconscious) mind inatii kila unachokiweka kwenye mawazo yako. Na mawazo haya yana nguvu kubwa ya kutokea kwenye matendo yako. Kwa mfano unapokuwa na mawazo yanayokuletea picha za kushindwa, akili yako ya ndani inapokea mawazo haya na kuanza kuyafanyia kazi. Hivyo kama unawaza kuumwa utaona unaumwa, kama unawaza kushindwa utashindwa kila wakati.
Chunga sana mawazo unayoingiza kwenye akili yako, hayo hayo ndio yatakayotokea kwenye maisha yako. Hivyo epuka mawazo mabaya na karibisha mawazo mazuri siku zote.
2.Tumia Tiba ya Tabia kuondoa hofu ya kushindwa.
Moja ya njia unazoweza kutumia kushinda hofu ya kushindwa ni kutumia tiba ya tabia. Kupitia tiba hii unafanya lile jambo ambalo unahofia kulifanya na jinsi unavyofanya hofu ndio inazidi kuondoka. Na unaweza kufanya hivi kwa kuanza kidogo kidogo ili kuzoea na baadae unaongeza mpaka hofu inaondoka kabisa. Kwa mfano kama unaogopa kuongea mbele ya watu unaweza kuanza kuongea na watu wachache halafu ukaendelea kuongea na watu wengi kidogo, baadae wengi zaidi na hatimaye kuongea na kundi kubwa la watu.
Endelea kufanya vitu unavyohofia kufanya na hofu hiyo itaondoka.
Naamini umejifunza machache kuhusu hofu ya kushindwa, anza kuyatumia ili uweze kufikia mafanikio makubwa.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)
TUKO PAMOJA.