Nguvu kubwa ya kufanya na kukamilisha mipango yetu ipo ndani ya akili zetu. Tunajifungia kwenye gereza la akili zetu kwa kufanya yale ambayo tunayafanya kila siku. Hatuiachii akili yetu uhuru wa kutambua na kutumia fursa nyingine ambazo zinapatikana. Tatizo kubwa la wengi wetu, kutokana na woga au kutokujiamini hawaruhusu akili zao kufikiria mbali zaidi ya pua zao.

Madhara ya aina hii ya akili ni makubwa sana kwenye maisha yetu. Aina hii ya kufikiri inasababisha mtu anashindwa kufanya mambo makubwa na hivyo kushindwa kufikia mafanikio makubwa. Matendo ya mwanadamu yanaweza kwenda mbali zaidi na kufikia mafanikio makubwa sana kama ataruhusu akili yake iweze kufikiri makubwa zaidi. Mambo yote tunayofanya yanazaliwa kwenye mawazo yetu, hivyo unapokuwa na mawazo yaliyofungwa huwezi kufikia mafanikio makubwa.

Ni kwa sababu tunashindwa kuipa akili yetu uhuru ndio maana tunashindwa kugundua nguvu kubwa iliyoko ndani yetu ya kuweza kufikia mafanikio makubwa. Hivyo tunaishi na kufa tukiwa bado hatujatumia uwezo mkubwa ulioko ndani yetu.

Naamini kabisa kwamba kila mtu anaweza kujitoa kwenye kifungo hiki cha mawazo na kuweza kufanya mambo makubwa yatakayomuwezesha kufikia mafanikio makubwa. Tunavyofikiri ndivyo tunavyohisi na ndivyo tunavyotenda, iwe unafikiri kidogo au kikubwa, chanya au hasi. Fikra zako ndio zinaweza kukufanya ufikie mafanikio au ushindwe kufikia mafanikio.

Tatizo au kikwazo chochote unachokutana nacho unaweza kulitatua kwa kuanzia kwenye mawazo yako. Jinsi unavyofikiri ndio itakuwezesha kuondoka kwenye tatizo au kuendelea kuwepo kwenye tatizo.

Jiulize mzswali haya na kujijibu na kisha ufuate ushauri uliotolewa.

1. Je unapenda kujitetea? Je unapenda kukwepa majukumu na kutafuta sababu unaposhindwa kutimiza majukumu yako?

Ushauri; Kumbuka kila unapokubali jukumu lolote ni lazima ulitekeleze kwa kiwango cha juu sana. Ukishindwa kutimiza majukumu yako usitafute sababu wala kujitetea chukua hatua ya kurekebisha wapi ulipokosea.

2. Je unawalaumu wengine kwa kushindwa kwako? Je unaposhindwa unatafuta visingizio vya watu, hali au mazingira.

Ushauri; Kwenye maisha yako ya kila siku, inapotokea umeshindwa au umekwaruzana na mtu usiishie kulalamika tu na kulaumu wengine. Chukua hatua ya kujua ni jinsi gani wewe umechangia na ujirekebishe.

3. Je unashindwa kuzuia hasira zako? Inapotokea umekwaruzana na mtu au mmeshindwa kuelewana je unajikuta unashindwa kuzuia hasira zako na kuchukua maamuzi ambayo baadae unayajutia?

Ushauri; Kila unapojikuta kwenye mazingira yanayokutengenezea hasira epuka kufanya maamuzi yoyote. Kaa kimya na jitahidi kuondoka kwenye mazingira hayo. Kama ni tatizo utalisuluhisha baadae ukiwa umeshatulia.

4. Je unakosa kujiamini? Je huamini kama mawazo yako yanaweza kuleta mabadiliko au unayaona hayana maana? Je unategemea mawazo na maoni ya wengine ndio yaongoze maisha yako?

Ushauri; Amini ya kwamba wewe ni mtu ambaye una uwezo mkubwa na uwezo huo unaanzia kwenye mawazo yako. Heshimu mawazo yako na yafanyie kazi ili yaweze kukuletea mafanikio makubwa.

5. Je unatabia ya kufikiria vitu vya karibu tuu? Je unafikiria utapata nini leo au siku chache zijazo bila ya kuangalia miaka mitano, kumi au hata ishirini utakuwa wapi?

Ushauri; Maamuzi yoyote unayofanya fikiria miaka kumi au hata ishirini ijayo yatakufikisha wapi. Kama unaona hayatakuwa na manufaa makubwa kwako achana nayo.

Katika vikwazo vyovyote utakavyokutana navyo kwenye maisha yako jua ya kwamba suluhisho linaanzia kwenye mawazo yako. Pia maamuzi unayochukua hakikisha yanakuwa na manufaa kwako kwa muda mrefu.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)

TUKO PAMOJA.