Moja ya changamoto ambazo zinawakabili wajasiriamali wengi ni kipato kidogo kutoka kwenye ujasiriamali wao au biashara zao. Watu wengi wamekuwa kwenye ujasiriamali kwa muda mrefu ila hawaoni mabadiliko makubwa kwenye kipato chao. Hali hii imefanya biashara za watu wengi kudumaa na hatimaye kufa kabisa.

Leo tutajadili njia tano unazoweza kutumia kuongeza kipato chako na hivyo kuweza kufikia mafanikio makubwa kupitia ujasiriamali. Njia hizi tano unaweza kuanza kuzitumia mara moja na kuleta mabadiliko kwenye biashara yako.

1. Weka vipaumbele vya faida.

Katika biashara au kazi yoyote unayofanya asilimia 80 ya faida yako inatokana na asilimia 20 ya juhudi zako. Na asilimia 20 ya faida yako inatokana na asilimia 80 ya juhudi zako. Hivyo unaweza kuwa unafanya kazi zako kwa juhudi sana ila unachofanya kina faida ndogo sana. Jua ni mambo gani ambayo ukiyafanya yanaleta faida kubwa na yafanye kwa ufanisi wa hali ya juu. Kama unauza bidhaa jua ni bidhaa zipi ukiuza zinaleta faida kubwa au zinatoka sana na kazana kuziuza hizo ili kutengeneza kipato kikubwa zaidi.

2. Weka thamani kubwa kwenye muda wako.

Muda una thamani kubwa sana kushinda fedha, unaweza kupata fedha zaidi ila huwezi kupata muda zaidi. Kwa vyovyote vile kuna mambo ambayo unafanya ambayo yanapoteza muda wako na hivyo kukufanya ushindwe kupata kipato kikubwa. Jua thamani ya muda wako kutokana na kiwango unachotaka kupata. Kwa mfano kama unataka kupata shilingi laki moja kwa siku na unafanya kazi masaa kumi kwa siku hii ina maana saa yako moja ina thamani ya shilingi elfu kumi. Hakikisha kila unachokifanya kwenye masaa yako ya kazi kinakuingizioa shilingi elfu kumi au kinaandaa mazingira ya wewe kutengeneza shilingi elfu kumi siku nyingine.

3. Jifunze kusema hapana.

Hapana ni neno ambalo litakuwezesha kuongeza kipato chako hasa unapokuwa mjasiriamali. Ukweli ni kwamba wajasiriamali huwa tunapata mawazo mengi mazuri kila siku, na wakati mwingine watu hutupa mawazo na kuomba tushirikiane nao kwenye kazi mbalimbali. Unaweza kufurahia mawazo haya au ushirikiano huo, lakini vinaweza kuwa ndio chanzo cha wewe kuwa na kipato kidogo. Huwezi kufanya kila kitu, na hata kama ungeweza bado huna muda huo. Chagua vitu vichache ambavyo unaweza kuvifanya kwa ubora na sema hapana kwa vingine utakavyoona ni vizuri zaidi. Ukianza kuhama hama kimawazo utashindwa kutengeneza kipato kikubwa.

4. Acha kutafuta sababu.

Mara nyingi watu wanapoona kipato chao ni kidogo huanza kutafuta sababu za kujiridhisha kwamba sio matatizo yao. Hivyo wanatumia sababu mbalimbali kama hali mbaya ya uchumi, wateja kutokuwa waaaminifu, kukosa mtaji mkubwa na hata kujiona hawana bahati, kama ndio sababu ya wao kuwa na kipato kidogo. Hizi zote ni sababu za uongo na kama ukiendelea kuzitumia utaendelea kuwa na hali ngumu ya kimapato. Tatizo kubwa la kipato chako kuwa kidogo ni wewe mwenyewe, hivyo anza kujirekebisha na utaona mabadiliko kwenye kipato chako.

5. Jifunze zaidi kuhusiana na unachofanya.

Robin Sharma, mwandishi na mhamasishaji maarufu “anasema kuongeza kipato chako mara mbili ongeza kujifunza kwako mara tatu”. Jifunze zaidi juu ya hiko unachofanya, kijue vizuri na tumia elimu hiyo unayoipata kufikia mafanikio zaidi. Kuna nafasi nyingi sana za kujifunza, vitabu, mtandao wa intaneti, semina na hata kuchukua kozi mbalimbali zinazotolewa.

Tumia njia hizi tano kutibu tatizo lako la udogo wa kipato. Unaweza kupata zaidi ya unachopata sana kama utakuwa tayari kujua makosa unayofanya sasa na kuyarekebisha.Kupitia njia hizi tano utajua ni wapi unapokosea na kama ukichukua hatua utafikia mafanikio makubwa.

Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.

TUKO PAMOJA.