Ni hali ya kusikitisha kwamba kushindwa kujiamini kumewazuia watu wengi sana kuweza kufikia mafanikio makubwa. Kutokujiamini ni kikwazo kikubwa kwa watu wengi kufikia mafanikio, ni sehemu ndogo sana ya watu walioweza kufikia mafanikio makubwa ni hii ni kwa sababu wanajiamini.

Kutokujiamini ni kukosa imani kwako binafsi na kwenye uwezo wako. Inaweza kutokana na wewe na kukosa au kushindwa kutengeneza taswira ya wewe kuwa umefikia mafanikio makubwa. Kutokujiamini kunakufanya ushindwa kutumia uwezo mkubwa ulioko ndani yako ili kuweza kufikia mafanikio makubwa.

Kutokujiamini ni moja ya vitu vinavyosababisha watu wengi kushindwa. Na uzuri ni kwamba unaweza kuondokana na kutokujiamini na ukaanza kuyafurahia mafanikio makubwa. Unao uwezo mkubwa wa kuondokana na hofu ya kushindwa kama kweli unayataka mafanikio kwa hamu kubwa sana.

Kuna nguvu kubwa sana ambayo ipo kwenye kujiamini ambayo inaweza kuongeza nguvu na uwezo wetu kwa kiasi kikubwa sana. Na kujiamini kunaanza na wewe mwenyewe kujua kwamba una uwezo mkubwa na unaweza kupata chochote unachotaka. Ni lazima uamini hivi kwa moyo wako wote na usijiwekee shaka yoyote.

Ni lazima kujiamini ili kufikia mafanikio makubwa.

Unaweza kuwa unajiuliza kwa nini baadhi ya watu wanaonekana kufanikiwa sana kwenye biashara kushinda wengine ambao wanafanya biashara moja na kwenye eneo moja? Au kwa nini baadhi ya watu wanapandishwa vyeo wakati kuna wengine wana vigezo sawa ila hawapati nafasi hiyo? Ukiangalia vizuri watu wanaofanikiwa sana au wanaopandishwa vyeo ni watu ambao wanajiamini sana. Ni watu ambao wanajua ndani yao wana uwezo mkubwa na wanaweza kuutumia kufanya mambo ya kipekee. Utaona hawa ni watu ambao hawaogopi kuja na mawazo mapya na kuyajaribu ili kuboresha kile wanachokifanya. Na kwa kuwa watu hawa wanajiamini huwavutia wengine kuwa karibu nao na hivyo kupendwa zaidi na kuwa na mahusiano mazuri.

Hakuna mtu ambaye anapenda kukaa na mtu ambaye hajiamini. Kama hujiamini hauvutii watu kuwa karibu na wewe kwa sababu akili yako imejaa mawazo hasi.

Kujiamini kunaondoa unyonge.

Kuna watu ambao wanapenda kuwa wanyonge katika maisha. Hawa ni watu ambao wanaamini wao hawawezi au wanaonewa na wenye nguvu au fedha. Unyonge huu hauletwi na wale wanaofikiriwa wanaonea bali unatokana na mtu kutokujiamini. Anza kujiamini sasa na uondokane na unyonge ambao unakufanya ushindwe kufikia mafanikio.

Amini kwamba hata wewe unaweza kuanzisha biashara kubwa sana na ukafikia mafanikio. Amini hata wewe unaweza kupandishwa cheo na kuwa afisa mkubwa. Kwa kuamini hivi utatengeneza mawazo chanya ambayo yatakuwezesha kufanya zaidi ili kufikia mafanikio makubwa.

Jenga kujiamini kabla ya kulala.

Kama tulivyoona kwenye makala zilizopita kuhusu subconscious mind, hii inapokea kila taarifa inayoingia na kuifanyia kazi. Moja ya njia za kujijengea kujiamini ni kusema maneno yanayoashiria kujiamini kila siku kabla ya kulala. Unapolala subconscious mind yako inapitia mawazo yale na kuanza kukujengea mazingira ya wewe kujiamini.

Kabla ya kulala fikiria na jenga taswira kwamba wewe ni mtu unayejiamini, unazungumza na watu mbali mbali na kutoa mawazo yako bila ya woga na pia umeshafikia mafanikio makubwa.

Jumuika na watu wanaojiamini.

Kama wewe umeshajijengea kujiamini halafu watu wanaokuzunguka hawajiamini watakurudisha nyuma. Kwa kuwa wewe unajiamini unaamini unaweza kufanya chochote unachotaka. Ila utakapomwambia mtu asiyejiamini mipango yako atakukatisha tamaa na kukutisha sana.

Ili kuepuka kurudishwa nyuma kujumuika na watu wanaojiamini. Kwa kuwa karibu na watu wanaojiamini unapata nguvu kubwa ya kuendelea kujiamini. Pia utapata kuungwa mkono mawazo yako makubwa ambayo yatakupatia mafanikio makubwa.

Anza leo kujijengea kujiamini, usiruhusu wazo hata moja la mashaka kuingia kwenye akili yako. Amini una uwezo mkubwa sana na unaweza kufikia mafanikio makubwa sana.

Nakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa.

TUKO PAMOJA.