Mpaka sasa tumeshajifunza nini maana ya nidhamu binafsi, faida zake na hata jinsi ya kujijengea nidhamu binafsi. Pia tumeona kwamba kujenga nidhamu binafsi sio kazi ndogo ila pia sio kwamba haiwezekani. Inahitaji kujitoa na kujipanga ili kuweza kufikia nidhamu binafsi.

Nidhamu binafsi ndio hitaji na msingi mkubwa wa kuweza kufikia mafanikio makubwa. Bila ya kuwa na nidhamu binafsi ni vigumu sana kuweza kufikia mafanikio. Nidhamu binafsi ndio itakayokufanya uweze kuendelea na mipango yako hata pale unapokutana na changamoto au vikwazo vikubwa. Nidhamu binafsi ndio inakuwezesha kuwa mvumilivu na kuweza kufikia mafanikio makubwa.

Kuna vitu vingine muhimu kufikia mafanikio makubwa.

Ni kweli kabisa kwamba ili kufikia mafanikio unahitaji kuwa na malengo na mipango na pia kufanya kazi kwa bidii na maarifa. Na pia kuna vitu vingine vingi sana unavyohitaji ili kufikia mafanikio makubwa. Lakini msingi mkubwa wa kufikia mafanikio hayo ni nidhamu binafsi.

Watu wengi wanaweka malengo na mipango kila siku, lakini mbona hawafanikiwi? Watu wengi wanafanya kazi kwa nguvu sana, lakini mbona bado wanaendelea kuwa na maisha magumu? Ukiangalia vizuri unakuta watu hawa wanakosa nidhamu binafsi. Ni kweli mtu anaweka malengo na mipango na hata anafikia kuanza hatua ya utekelezaji ila baada ya siku chache anashindwa kuendelea. Ni kweli mtu anafanya kazi kwa nguvu sana ila kazi anazofanya sio zile zenye kumpatia manufaa makubwa, au kipato  anachopata anashindwa kukitumia na kukipangilia vizuri.

Matatizo makubwa unayokutana nayo kwenye maisha ni ukosefu wa nidhamu binafsi. Watu wengi wanaoingia kwenye madeni sugu na kuishi maisha yao yote kulipa madeni chanzo kikubwa ni ukosefu wa nidhamu binafsi. Matatizo mengi ya kiafya wanayopata watu chanzo kikubwa ni kukosa nidhamu binafsi. Na hata matatizo ya kifamilia au kimahusiano yanatokana na ukosefu wa nidhamu binafsi.

Hakuna kitu chochote kwenye maisha ambacho unaweza kukitenga na nidhamu binafsi. Na kwa kuwa mafanikio kwenye maisha yanategemea vitu kama matumizi mazuri ya fedha, afya njema na hata mahusiano mazuri, kwa kukosa nidhamu binafsi unakosa vyote hivyo na hii kupelekea kushindwa kufikia mafanikio makubwa.

Anza sasa kufanya nidhamu binafsi kuwa sehemu kubwa ya maisha yako. Tekeleza ulichoahidi, fanya ulichopanga, maliza ulichoanza na boresha maisha yako kila siku. Rudia tena kusoma makala hizi za kujijengea nidhamu binafsi na yafanyie kazi yale yote uliyojifunza.

Nakutakia kila la kheri kwenye safari yako ya kufikia mafanikio makubwa.

TUKO PAMOJA.