Karibu sana msomaji wa KISIMA CHA MAARIFA katika uchambuzi wa kitabu THE RICHEST MAN IN BABYLON. Hiki ni kitabu ambacho kinakupa maarifa na mbinu za kutatua changamoto zako za kifedha. Kitabu hiki kinakupatia mbinu zilizotumika zamani na kuufanya utawala wa BABELI kuwa utawala wenye nguvu sana. Mbinu hizi zinafanya kazi mpaka leo na kama ukiweza kuzitumia nakuhakikishia utaona mabadiliko makubwa kwenye fedha zako na utafikia mafanikio makubwa sana.

Maendeleo yetu kama taifa yanategemea maendeleo ya mtu mmoja mmoja. Kitabu hiki kinajadili maendele ya mtu mmoja mmoja. Mafanikio yanamaanisha kuweza kufanikisha kulingana na uwezo wa mtu husika. Maandalizi mazuri ni muhimu sana ili kuweza kufikia mafanikio. Matendo yetu hayawezi kuwa mazuri zaidi ya mawazo yetu, na mawazo yetu hayawezi kuwa mazuri zaidi ya uelewa wetu. Kitabu hiki kitakupatia uelewa wa fedha na kukusaidia mbinu za kupata fedha, kuzitunza na kuzifanya zikuzalishie fedha zaidi.

Kwenye kurasa zinazofuata tunapelekwa kwenye mji wa zamani wa babeli ambapo kanuni za fedha zilianza kutumika na sasa zinatumika dunia nzima. Babeli ulikuwa mji tajiri wakati huo kwa sababu wananchi wake walikuwa matajiri sana. Walitambua thamani ya fedha na walitumia mbinu za kifedha kwenye kupata fedha, kuhifadhi fedha na kufanya fedha zao kuwapatia fedha zaidi.

Mtu aliyetamani dhahabu.

Bansier ambaye alikuwa fundi magari alikuwa amekatishwa tamaa, akiwa amekaa eneo lake la kutengenezea magari, mke wake alikuwa akija kumuambia kwamba chakula nyumbani kimeisha. Bansier alikuwa amekaa bila ya kufanya chochote huku akionekana kuwa na mawazo mengi. Nyumba yake ilikuwa nje kidogo ya mji wa babeli ambapo mbele kidogo ulikuwepo ukuta ambao ulizunguka hekalu ya mfalme wa babeli. Eneo alilokuwa anaishi Bansier halikuwa na mpangilio wowote, nyumba zilijengwa hovyo na kulikuwa na mchanganyiko wa masikini na matajiri.

Pembeni ya alipokuwa amekaa kulikuwa na njia ambayo magari ya matajiri yalipita, wafanyabiashara na hata watumwa wa mfalme walipita wakiwa wamebeba maji. Kulikuwa na kelele nyingi lakini Bansier hakusikia kelele hizo kutokana na mawazo mengi aliyokuwa nayo. Bansier alistuliwa kutoka kwenye mawazo yake hayo na rafiki yake aliyeitwa Kobbi ambaye alikuwa ni mwanamuziki. Kobbi alimwomba Bansier amkopeshe shekeli mbili ambazo angemzrudishia siku inayofuata. Bansier alimwambia “kama ningekuwa na hizo shekeli mbili nisingempa mtu yeyote hata rafiki yangu wa karibu kwa sababu zingekuwa ndio hazina yangu, hakuna mtu anayekopesha hazina yake, hata kwa rafiki yake.”

Kobbi alishangazwa sana na jibu hilo na kumwambia kama hana hata shekeli mbili kwa nini amekaa tu na asifanye kazi kwa bidii kukamilisha magari ili apate fedha? Alimuuliza ni kitu gani ambacho kinamfanya ashindwe kufanya kazi kama alivyokuwa anafanya zamani? Bansier alimjibu kwamba alianza na ndoto nzuri sana na alikuwa ni mtu anayejielewa. Alifanya kazi sana na mfuko wake ulijaa shekeli, fedha na dhahabu. Alikuwa na shekeli za kutosha kuwapa omba omba na fedha za kutosha matumizi ya nyumbani na kununua urembo wa mke wake na pia alikuwa na dhahabu za kutosha hivyo kuweza kutumia fedha bila ya wasiwasi wowote. Bansier anasema alipoamka na kukuta mfuko wake bado ni mtupu na hauna hata shekeli moja mawazo ya uasi yalimuingia kwenye kichwa chake.

Bansier alimwambia Kobbi wakae na kuzungumzia hatima ya maisha yao kwa sababu wao wote ni vijana na wanamatatizo sawa. Alimwambia wote walishapata fedha miaka iliyopita ila bado maisha yao ni magumu. Na pia alisikitishwa sana kwa sababu waliishi kwenye mji tajiri sana ila wao bado ni masikini. Alimuuliza kwa nini wao wanashindwa kupata fedha na dhahabu nyingi zaidi ya matumizi wao na kuwa na uhuru? Bansir aliendelea kusema kwamba hata watoto wao wanafuata nyayo za baba zao na hivyo watakuwa na maisha magumu kifedha, na hilo watalipeleka hata kwa wajukuu na vitukuu.

Kobi alishangazwa na aliyokuwa anaongea Bansir na kumwambia kwanzia wamekuwa marafiki hakuwahi kumsikia akiongea maneno kama hayo. Bansir alisema kwamba kuanzia alfajiri mpaka giza linaingia anafanya kazi ngumu ya kutengeneza gari zuri kushinda mengine, akiamini kwamba iko siku mungu atamuona na kumfanya nae awe tajiri lakini haoni hilo likitokea. Akasema amejitoa sana kufanya kazi kwa nguvu zake zote ila haoni malipo yakifanana na nguvu anazoweka. Aliuliza tatizo lao ni nini? Kwa nini wao hawana fedha na dhahabu za kuwafanya wawe na maisha mazuri kama watu wengine?

Kobbi alimjibu hata yeye anashangaa kwa nini wao wana maisha magumu. Anasema amekuwa akitengeneza muziki mzuri sana kuliko watu wengine wote na amekuwa akifanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa sana ila anashangaa kwa nini wana maisha magumu kama watumwa wa mfalme. Alisema watumwa wa mfalme wanafanya kazi kila siku bila ya kupumzika na hawana chochote cha kufurahia zaidi ya kuamka kufanya kazi, kula na kulala. Aliuliza kwa nini wao ni watu huru ila wanaishi kama watumwa.

Kobbi alimwambia Bansir watafute na kujifunza ni vitu gani wale wenye dhahabu za kutosha wanafanya nao wafanye hivyo. Alimwambia huenda kuna siri wanayoitumia ila wao hawaijui ndio maana maisha yao yanakuwa magumu. Walimkumbuka Arkad ambaye ni mtu tajiri sana pale babeli. Walianza kumsifia kwamba ana utajiri mkubwa mpaka mfalme huwa anamuomba ushauri kwenye mambo ya fedha. Bansir alisema kwa utajiri alioko nao Arkad kama angekutana naye usiku angemuibia mfuko wake wa fedha, Kobbi alimwambia huo ni ujinga kwa sababu utajiri wa mtu haupo kwenye mfuko wa fedha bali kwenye akili yake. Walisema ana utajiri mkubwa sana na hivyo atakuwa na mbinu nzuri kuhusu utajiri. Walishauriana wamtafute Arkad ili wamuombe awape seri za yeye kuwa tajiri mkubwa pale babeli. Mwanzoni walikuwa na wasiwasi kama atakubali ombi lao ila walipeana moyo kwamba hakuna tatizo kwenye kumuomba mtu akupe ushauri.

Hivyo walikubaliana siku hiyo hiyo wamtafute Arkadi ili awafundishe mbinu za kuwa marajiri. Na pia walikubaliana wawachukue wenzao ambao walikua pamoja ili nao wakajifunze mbinu hizo.

Tunajifunza nini hapa?

1. Kuna watu wengi wanaofanya kazi sana ila hawaoni wakisonga mbele.

2. Matatizo ya fedha yanaanzia kwa wazazi na yanarithiwa kwa watoto, wajukuu na hata vitukuu.

3. Watu waliofanikiwa wanazo siri za mafanikio na wanazitumia kuendelea kupata mafanikio.

4. Kufanikiwa unatakiwa kujua kile wanachofanya waliofanikiwa na wewe ukifanye.

5. Utajiri wa mtu haupo kwneye fedha au mali anazomiliki bali upo kwenye akili yake na hata kama akipoteza fedha zote anaweza kuzipata tena.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kufikia mafanikio makubwa.

TUPO PAMOJA, TUTAKUTANA KILELENI.