TIBA YA NNE; Linda hazina yako isipotee.

Kisirani kinapenda sehemu yenye mafanikio, fedha za mtu zinatakiwa kulindwa vizuri sana la sivyo zinapotea. Ni busara kuweza kupata kiasi kidogo cha fedha na kukilinda vizuzi kabla ya kupata kiasi kikubwa zaidi. Arkad alianza na maelezo hayo siku ya nne. Kila mtu ambaye anamiliki fedha nyingi hushawishika kuwekeza sehemu ambazo zinatoa faida kubwa tena kwa muda mfupi. Mara nyingi marafiki na ndugu huingia kwenye uwekezaji wa aina hii na kumshawishi mtu naye aingie.

Msingi wa kwanza wa uwekezaji ni usalama wa mtaji unaoweka kwenye uwekezaji. Je ni busara kushawishika na faida kubwa wakati mtaji wote unaweza kupotea, hapana, alienbdelea kuongea Arkad. Adhabu ya kufanya maamuzi ya hatari ni kupoteza. Chunguza kwa makini aina ya uwekezaji unayotaka kufanya kabla ya kuweka fedha zako ulizozipata kwa jasho. Usitamanishwe na kupata faida kubwa kwa haraka.

Arkad aliendelea kuwaambia kwamba kabla ya kumkopesha mtu yoyote fedha zako, jiridhishe kwanza kama ana uwezo wa kukulipa. Na pia angalia sifa ya ke ya kufanya hivyo usije ukatoa zawadi ya fedha yako uliyoipata kwa shida. Arkas aliwaambia uwekezaji wake wa kwanza alipata hasara kwa sababu hakufanya uchunguzi wa kutosha. Alimuamini mtengeneza matofali kwamba anaweza kununua madini ya thamani kitu kilichomfanya apoteze fedha zake. Arkad aliwaambia wajifunze wasijekuingia kwenye makosa kama hayo na kama wanaona hawawezi kujua vizuri usalama wa uwekezaji waombe ushauri kwa watu ambao ni wazoefu.

Arkad aliwaambia hii ndio tiba ya nne ya mifuko iliyosinyaa; linda hazina yako isipotee kwa kuwekeza maeneo ambayo mtaji wako utakuwa salama na unaweza kuchukua faida inayotokana na uwekezaji wako. Omba ushauri kwa wazoefu wa fedha na fanya busara ndio ikuongoze katika uwekezaji.

TIBA YA TANO; Fanya sehemu unayoishi kuwa uwekezaji wenye faida.

Arkad alianza siku ya tano kwa kuwaambia, kama mtu anaweza kuishi kwa kutumia sehemu ya tisa ya kipato chake na sehemu hiyo ya tisa akaweza kuwekeza kwenye kitu ambacho kitampa faida na maisha yake yakaendelea kuwa bora basi mtu huyu atapata mafanikio haraka zaidi. Alisema watu wengi wa babeli wanakuza watoto wao kwenye maeneo ambayo sio mazuri, wake zao hawapati sehemu nzuri za kufanya kazi zao na hata watoto wao hawapati maeneo mazuri ya kufanya michezo yao.

Aliendelea kuwaambia hakuna familia inayoweza kuyafurahia maisha kama hawaishi kwenye nyumba yao wenyewe. Hivyo napendekeza kila mtu awe na nyumba yake. Aliwaambia ni kitu ambacho kinawezekana kwa mtu aliyejipanga kwa sababu ardi inapatikana na kuna sehemu nyingi ambazo mtu anaweza kukopa fedha na kujengea nyumba yake kisha akaendelea kulipa kidogo kidogo kama alivyokuwa analipa kodi kwenye nyumba ambayo sio ya kwake. Alisema kwa kuwa na nyumba inapunguza gharama za maisha na hivyo mtu kuwekeza kipato chake zaidi.

Arkad aliwaambia hii ndio tiba ya tano; miliki nyumba yako mwenyewe.

TIBA YA SITA; Jihakikishie kipato chako cha baadae.

Arkad alianza siku ya sita kwa kuwaambia; Maisha ya kila binadamu yanaanzia kwenye utoto na kuelekea kwenye uzee, hivi ndivyo maisha ya watu wengi yanavyokenda kama wasipofariki mapema. Hivyo ni vyema kwa kila mtu kufanya maandalizi ya kipato kizuri kwa siku za mbeleni hasa anapokuwa mzee na kuwa hana nguvu za kufanya kazi. Somo hili litakuwezesha kuwa na mfuko uliotuna wakati ambao huna tena uwezo wa kufanya kazi.

Arkad aliwaambia, mtu yeyote ambaye anazijua sheria za fedha na akapata fedha nyingi sana kwa kupitia sheria hizo, ni lazima afikirie kuhusu siku zijazo. Ni lazima aweke mipango ya muda mrefu ujao ili wakati ambapo amezeeka aweze kuendelea kuwa na maisha mazuri.

Arkad aliendelea kusema kuna njia nyingi ambazo mtu anaweza kuzitumia kujijengea usalama wa siku zake za mbeleni;

1. Kutafuta sehemu salama kwenye nyumba yake na kuficha fedha zako. Japo hii sio njia ya usalama sana.

2. Kununua ardi au nyumba ambayo itaongezeka thamani kadiri siku zinavyokwenda.

3. Kuwekeza fedha yako kwa watu wanaokopesha fedha na wakawa wanakupa riba kila baada ya muda na ukaendelea kuwekeza riba hiyo.

Arkad aliendelea kuwaambia mtu yeyote anayepuuza kujipanga kwa siku zijazo atakuwa na maisha magumu sana baadae.

Arkad alisema na hii ndio tiba ya sita; jihakikishie kipato chako siku za mbeleni ambapo utakuwa umezeeka na huwezi tena kufanya kazi.

TIBA YA SABA; Ongeza uwezo wako wa kipato.

Arkad alianza siku ya saba kwa kusema; Leo nitaongelea tiba muhimu sana ya mifuko iliyosinyaa, sitaongelea fedha bali nitawaongelea nyie wenyewe. Nitaongelea vitu ambavyo vipo kwenye akili na maisha ya watu vinavyowazuia kupata mafanikio. Arkad aliwaambia siku moja kijana alimfuata na kumwomba mkopo. alipomuuliza sababu yake ya kutaka mkopo alimjibu kipato chake hakitoshelezi matumizi yake. Alimwambia kwa hali hiyo yeye sio mteja mzuri kwa wakopeshaji wa fedha maana hana uwezo wa kulipa fedha anayokopa. Arkad alimwambia unachohitaji wewe ni kuongeza kipato chako zaidi, alimuuliza ni kitu gani umefanya ili kuongeza kipato chako? Alimjibu amejitahidi sana kufanya kipato chake kiongezeke na ameshamfuata mwajiri wake mara sita ndani ya miezi miwili amuongeze mshahara lakini bado hajaongezewa.

Arkad aliwaambia kipato kinaongezeka kwa mtu kuanz akujiendeleza yeye mwenyewe. Aliwaambia alipokuwa mwandishi aliona wenzake wanapata fedha nyingi kuliko yeye, hivyo alijifunza ni vitu gani wanavyofanya. Alipojua vitu hivyo muhimu na kuvitumia kwenye kazi yake aliona mabadiliko makubwa. Arkad aliwasisitiza sana wajifunze zaidi kuhusiana na kazi au biashara wanayofanya na hii itawaongezea kipato chao mara dufu.

Arkad aliwaambia jinsi unavyojua zaidi ndivyo unavyolipwa zaidi. Mtu anayetafuta kujifunza zaidi kwa kile anachofanya atatajirika zaidi.

Arkad aliwaambia hii ndio tiba ya saba ya mifuko iliyosinyaa; Kujifunza zaidi na kuwa na busara zaidi ili kuongeza ufanisi wako na hivyo kuongeza kipato chako.

Arkad alimaliza kwa kuwaambia hizo ndio tiba sana za mifuko iliyosinyaa. Aliwaambia wajifunze na kuyafanyia kazi mambo yote hayo na wataona mabadiliko makubwa. Aliwaambia kuna fedha nyingi sana Babeli kuliko wanavyoweza kufikiri. Aliwaambia kayafanyieni kazi haya niliyowafundisha na mtapata utajiri mkubwa sana.

Na wewe msomaji wa KISIMA CHA MAARIFA yafanyie kazi mambo haya saba uliyojifunza na utaona mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yako. Mambo yote haya yako kwenye uwezo wako na unaweza kuanza kuyafanyia kazi leo. Hebu tujikumbushe tena tiba hizi saba za mifuko iliyosinyaa;

1. Weka sehemu ya kumi ya kipato chako(jilipe wewe kwanza)

2. Dhibiti matumizi yako, weka bajeti ya matumizi yako, jua ni kiasi gani utatumia kwa chakula na kiasi gani kwa starehe, lakini bajeti hiyo isizidi sehemu ya tisa ya kipato chako.

3. Ifanye Akiba yako izae zaidi, ifanye kila fedha yako ikufanyie kazi ili uweze kuzalisha utajiri zaidi na hivyo utatengeneza mfereji wa utajiri utakaoendelea kutiririsha utajiri hata kama hufanyi kazi.

4. Linda hazina yako isipotee, linda hazina yako isipotee kwa kuwekeza maeneo ambayo mtaji wako utakuwa salama na unaweza kuchukua faida inayotokana na uwekezaji wako. Omba ushauri kwa wazoefu wa fedha na fanya busara ndio ikuongoze katika uwekezaji.

5. Fanya sehemu unayoishi kuwa uwekezaji wenye faida, miliki nyumba yako mwenyewe.

6. Jihakikishie kipato chako cha baadae, jihakikishie kipato chako siku za mbeleni ambapo utakuwa umezeeka na huwezi tena kufanya kazi.

7. Ongeza uwezo wako wa kipato, kujifunza zaidi na kuwa na busara zaidi ili kuongeza ufanisi wako na hivyo kuongez akipato chako.

Yafanyie mambo haya saba kazi kuanzia leo na utaanza safari yako ya kufikia mafanikio makubwa.

Nakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa unayotazamia.

TUPO PAMOJA.

P.S Tushirikishe ni mambo gani umejifunza katika tiba hizi saba za mifuko iliyosinyaa kwenye maoni hapo chini. Hata kama nimeshaandika hapo juu, fanya zoezi hili kwa sababu litakusaidia kujifunza zaidi na kujitoa zaidi kufanyia kazi yale uliyojifunza.