Mara nyingi tumekuwa tukiona wajasiriamali waliofanikiwa na sisi kutamani sana kufikia mafanikio kama hayo. Kila siku tumekuwa tunapata hadithi mbalimbali za watu ambao walianzia chini kabisa ila baada ya muda wameweza kufikia mafanikio makubwa sana kupitia ujasiriamali. Ni hadithi za aina hii ambazo zinatufanya tuone inawezekana kupata mafanikio makubwa sana kwenye ujasiriamali na hivyo kusukumwa kuingia kwenye ujasiriamali.
Kuna hatua tatu muhimu kwenye safari ya ujasiriamali ambazo ni muhimu sana kila mjasiriamali kujifunza. Katika kila hatua kuna mambo mengi ya kujifunza ili kuweza kufikia mafanikio makubwa zaidi. Utajifunza mambo hayo leo katika makala hii.
Hatua ya kwanza; wazo zuri na shauku kubwa ya kufanya ujasiriamali.
Hatua ya kwanza ya safari ya ujasiriamali inaanza na wazo zuri la biashara na shauku kubwa ya kutimiza wazo hilo. Huu ni wakati ambapo mtu unakuwa na matumaini makubwa sana kwamba wazo lako ni wazo bora na litaleta mabadiliko makubwa kwa wengine na wewe kukuletea faida kubwa. Baada ya wazo hili unaweka malengo na mipango ya kufanikiwa kupitia wazo hilo. Utaandaa mchanganuo wa biashara, utaweka makisio ya faida na kila unapoupitia mchanganuo unafarijika sana kwa sababu faida kubwa sana inaonekana na unakuwa umepanga kuipata baada ya muda kidogo wa kuwepo kwenye biashara.
Hatua hii ya kwanza ndio inayowafanya wengi kuingia kwenye ujasiriamali na huwapa watu ujasiri na udhubutu wa kuchukua hatua.
Hatua ya pili; hatua ya kujifunza, mambo kuwa magumu.
Hatua ya pili inaanza pale ambapo umeshakamilisha mipango yako yote kama ulivyoainisha kwenye mchanganuo wa biashara. Umeshafungua eneo la biashara au ofisi, umeshaweka vifaa vyote unavyohitaji, umeshatangaza kwa wateja husika na sasa unasubiri wateja wajipange kwa mamia au maelfu kupata bidhaa zako au huduma yako. Hivi ndivyo ulivyokuwa umepanga kwenye mipango yako, lakini ukweli ni kwamba haitokei hivyo. Wateja uliotegemea watakuja wengi huwaoni na hata wachache wanaokuja wanaweza wasifanye manunuzi makubwa.
Hatua hii ndio hatua ngumu sana kwenye ujasiriamali, ni hatua ambayo huwakatisha wajasiriamali wengi tamaa na hivyo kujikuta wanaacha safari hiyo ya ujasiriamali. Kimsingi hii ndio hatua muhimu sana kwenye ujasiriamali. Kwa sababu ni kupitia hatua hii ndio mjasiriamali anatakiwa kujifunza zaidi. Anatakiwa kujifunza ni kitu gani hakifanyiki vizuri au ni vitu gani vichache akivifanya vitaleta mabadiliko makubwa kwenye biashara yake. Ni wakati huu ambapo mjasiriamali anatakiwa kufanya marekebisho kwenye mipango yake ya awali ili kuweza kuendana na hali ilivyo.
Hatua hii inahitaji uvumilivu mkubwa sana ili kuweza kuivuka la sivyo utaishia kukata tamaa na kuona ujasiriamali haukufai wewe.
Hatua ya tatu; kupata mafanikio makubwa na yasiyo na kikomo.
Hatua hii ni pale ambapo mjasiriamali anakuwa maeshapita kwenye kipindi kigumu, ameshajifunza ni mambo gani yanamletea faida na yapi hayana faida kwake. Katika hatua hii mjasiriamali anakuwa anapata mafanikio makubwa sana na mambo sio magumu kama awali. Ni katika hatua hii tunawaona wajasiriamali wengi waliofanikiwa na kushawishika kuingia kwenye ujasiriamali bila ya kujua kuna hatua nyingine walizipitia katika safari yao. Jambo kubwa la kufanya katika hatua hii ni kuendelea kujifunza zaidi na kuona ni jinsi gani unavyoweza kukua na kupanua wigo wako wa biashara.
Kama ndio unapanga kuingia kwenye ujasiriamali zijue vizuri hatua hizo na jiandae kuzipitia bila ya kukata tama. Kama tayari uko kwenye ujasiriamali inawezekana uko kwenye moja ya hatua hizo, jua jinsi ya kutumia vizuri hatua hizi ili kuweza kupata mafanikio makubwa. Ni muhimu sana wajasiriamali kujipanga vizuri kwa hatua ya pili maana hii ndio inawaondoa wajasiriamali wengi kwenye biashara.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya ujasiriamali.
TUPO PAMOJA.