Tunapozungumzia kuhusu hofu na kuwataka watu wasihofie matukio ya kimaisha na kujitahidi kuyapokea kama yanavyokuja na kutulia kabla hawajajiuliza wafanye nini, hatuna maana kwamba binadamu hatakiwi kuwa na hofu katika maisha yake. 
Ukweli ni kwamba, hofu ni kama kitu cha kimaumbile ambacho humfanya binadamu aweze kuishi. Bila kuwa na hofu kabisa, kuna uwezekano hapo wa kuwa na tatizo la kiakili. Hii ni kwa sababu hofu huweza kumsaidia binadamu kuweza kukwepa maafa na kusonga mbele.


Kuna zile hofu ambazo hizo tunaweza kusema ni kama lazima ziwepo. Kwa maisha haya na maumbile yetu binadamu, hizi hatuwezi kuzikwepa. Lakini hofu ambazo tunasema ni tatizo, ni zile hofu ambazo unakuwa nazo za kuogopa sana kesho kuliko kawaida. 

Najua kila mmoja wetu anapenda kuishi maisha ya kujali leo, yenye utulivu isiyo na hofu za kesho zaidi, yaani akawa anajali leo tu na siyo kesho au kesho kutwa. Wengi wetu tumekuwa tukijikuta tukiishi leo kimwili, lakini kiakili na kihisia tunafikiria sana kuhusu kesho na vurugu zake.

  
Kama binadamu wangekuwa wanaishi siku moja baada ya nyingine, dunia ingekuwa ni mahali pa amani sana. Nina maana wangekuwa wanajali yale ya leo tu, siyo ya jana na ya kesho. Lakini, ni vigumu kwetu kujali ya leo tu kwa sababu hatujui namna ya kumudu jambo hilo.

Kama unataka kuishi leo tu au kuishi siku moja baada ya nyingine,  unapaswa kuamua. Hakuna jambo lisilowezekana kufanywa hadi mtu aamue. Jiambie kwamba, unataka kuanzia sasa kukabiliana na kila jambo kwa kadiri linavyokuja na siyo kwa kadiri unavyolifuata.

Ukishaamua fanya jaribio hili. Kwa mfano, jitahidi sana kufikiria na kutenda lile unalotakiwa kulitenda kwa siku hiyo tu. Kama unadaiwa na unatakiwa kulipa deni hilo kesho na unajua hutaweza, achana na jambo hilo. Hili ni suala la kesho , iwe unaliweza au huliwezi.

Hii haina maana kuwa hutakiwi kupanga malengo na mipango yako katika maisha yako, hapana. Panga namna utakavyolilipa deni hilo, lakini usikalie kutwa nzima kuumia kwa maumivivu kwa sababu eti kesho hutaweza kulipa deni lako. Ukiumia leo sana, kesho ikifika utaumia kwa kufanya kitu gani?

Ni vema kuiacha hiyo kesho ifike, halafu ikifika utajua hapohapo kesho ufanye nini. Kupanga namna ya kulipa deni ni tofauti na kupoteza muda kujiingiza kwenye hofu kwa kufikiri itakavyokuwa hiyo kesho. Wacha hiyo kesho ije, isikuumize leo, hapo utakuwa umemudu kutawala hofu zako za kesho.

Ili uweze kumudu vizuri kukabiliana na hofu zako za kesho jifunze kutochanganya siku. Jua kwamba, leo ni leo na inajitegemea na kwa vyovyote hailingani na kesho. Iache leo iitwe leo, ishi leo tu utakuwa na amani moyoni. (Soma pia Hivi Ndivyo Unavyoweza Kufaidika Na Hofu Ulizonazo)

Hofu zozote ulizonazo juu ya maisha yako unaweza kuzimudu na kuzishinda leo endapo utaamua. Hebu tuchukulie kwa mfano, unataka kuacha kunywa pombe. Ukiacha kunywa leo, hesabu kwamba, umeacha kunywa leo. Kesho ikifika, usiseme kwamba, ulimudu kuacha kunywa jana, hapana.

Haja yako haikuwa kuacha kunywa pombe jana, bali leo na hata hiyo jana ulisema ‘Kuanzia leo naacha kunywa pombe’. Leo siyo kesho, ni leo. Kumbuka kila siku ni siku mpya na hivyo, kila jaribio tunalolifanya la kuacha tabia fulani, inabidi liwe jipya kwetu pia kila siku. 

Vivyo hivyo kwenye suala la kuishi kwa siku moja. Kwa kuwa kila siku ni siku mpya, inabidi tuishi hadi iishe, ili isije ikatuharibikia kabla hatujaitumia. Kuishi leo leo, yaani kujali kuhusu leo na kuachana na hofu za kesho, ni suala la mazoea pia.

Ili uweze kufanya hivyo, jiambie kila siku kwamba, unataka kuishi kwa siku hiyo tu. Kwa hiyo, anza kujaribu kuishi leo leo, ili uone umemudu kwa kiasi gani hofu ulizonazo juu ya maisha. Je, hofu zako umeweza kuzimudu kuepuka hata hofu yakushindwa kufanya jambo jipya?

Sawa, unadaiwa kodi ya nyumba na mwenye nyumba anakuja kesho, nawe huna fedha. Usijali, ishi leo, shughulikia yale ya leo leo na sio kuegemeza kichwa magotini, kuishi kesho, yaani kufikiria mwenye nyumba jinsi atakavyokutoa kwenye nyumba yake.

Mbona hajakutoa na kama atakutoa si usubiri aje akutoe! Ukimudu kuishi leo katika mazoezi, hatimaye utajikuta unaanza kujenga tabia hiyo. Maisha yako yatakuwa kwa siku inayohusika tu, hayatatambaa vizingiti vya kesho au kesho kutwa ambazo hazipo.

Kumbuka jambo moja. Hata kama tatizo litakuwa kubwa kwa kiasi gani, hatimaye ni lazima litafikia tamati. Kulikubali na kulikabili bila hofu ndiyo njia pekee ya kulifikisha kwenye tamati kimafanikio. Hivyo ndivyo unavyoweza kumudu kuondoa hofu za kesho, zinazokusumbua na kukutesa.

Nakutakia mafanikio mema, endelea kutembelea AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA kwa kujifunza na kufanya mabadiliko makubwa katika maisha yako.

TUKO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.

IMANI NGWANGWALU – 0767048035/ingwangwalu@gmail.com