M afanikio kwenye ujasiriamali yatatokana na kiasi cha mauzo unachofanya. Na kisi cha mauzo yako kinatokana na jinsi unavyowajua wateja wako na kuweza kufanya nao biashara vizuri. Wajasiriamali na wafanya bishara wengi wanafikiri wateja wote ni sawa na hivyo kujaribu kufanya nao biashara kwa mtindo mmoja. Hali hii imekuwa ikileta shida sana kwenye biashara kwa sababu kuna aina tofauti za wateja kama ilivyo aina tofauti za haiba za watu.

Leo utajifunza aina tatu tofauti za wateja na jinsi unaweza kufanya nao bishara ili uweze kufikia mafanikio makubwa. Katika kipindi ambacho nimekuwepo kwenye ujasiriamali nimekuwa nikijifunza tabia mbalimbali za wateja na nimeweza kuziweka katika makundi matatu. Japo kuna aina nyingi sana za wateja ukienda kiundani, hapa nakupa makundi matatu ambayo ni rahisi kujua mteja yupo kwenye kundi gani ana uweze kufanya naye biashara vizuri.

1. Wateja ambao wanajua wanachokitaka.

Hawa ni wateja ambao wanajua ni nini wanataka na wakijua wewe unaweza kuwapatia kile wanachotaka wanafanya biashara na wewe bila ya kusua sua. Hawa ni wateja ambao wakishajua kwamba wewe unatoa bidhaa au huduma fulani wanalipia kisha wanapata bidhaa au huduma waliyolipia. Wateja wa aina hii ni wazuri sana na kama wateja wote wangekuwa wa aina hii biashara ingekuwa rahisi sana kufanya.

Ili kutunza na kuendelea kuwa na wateja wa aina hii, jenga uaminifu mkubwa nao. Wakijua kwamba unawajali na unajali maslahi yao wataendelea kufanya biashara na wewe kwa muda mrefu. Ila ukileta tamaa na kutaka kupata zaidi kwa kuwa hawakusumbui utawapoteza kabisa.

2. Wateja wanaohitaji uhakika zaidi.

Hawa ni wateja ambao umeshawaeleza bidhaa au huduma unayotoa ila bado wanasuasua kufanya maamuzi ya kununua. Wateja hawa wanapendelea kupata maelezo zaidi na uhakika zaidi kwamba bidhaa au huduma unayowauzia itatatua matatizo yao au itafanya kile ambacho umesema itafanya. Wateja hawa wanaweza wasifanye maamuzi ya kununua mara moja na wakaenda kuomba ushauri kwanza kwa watu wao wa karibu au kufikiria zaidi. Ni wateja ambao hawana haraka na kama ukifanikiwa kuwashawishi ukafanya nao biashara na wakapata kile walichokuwa wanataka watakuwa wateja wako wa muda mrefu.

Ili kuweza kufanya biashara na wateja wa aina hii hakikisha unawapa maelezo ya kutosha na kuwapa uhakika kwamba bidhaa au huduma unayowauzia itawasaidia. Pia unaweza kuwapa muda wa kutumia bidhaa au huduma hiyo na kama isipowasaidia warudishe na kurudishiwa fedha. Kwa njia hii utawapa uhakika mkubwa na utafanya nao biashara kwa muda mrefu.

3. Wateja ambao hawapo tayari kufanya biashara.

Aina ya tatu ya wateja ni wateja ambao hawako tayari kufanya biashara. Kwa kifupi tunaweza kusema hawa ni wateja ambao ni wasumbufu. Wateja hawa kwanza wanakuja kwenye biashara yako, unazungumza nao vizuri na mwishowe wanakuambia wamependa bidhaa au huduma yako ila bei ni kubwa sana hivyo punguza. Unapopunguza kwa kiwango cha kawaida abacho umeweka cha kuwapunguzia wateja, wateja hawa bado hutaka punguzo zaidi. Ukiwapa punguzo zaidi hapo ndio matatizo yanaanza, watachukua bidhaa au huduma hiyo na baada ya muda mfupi watarudi kulalamika kwamba haijawasaidia na ukiwauliza vizuri unakuta hawajaitumia kama inavyohitajika kutumiaka. Wateja wa aina hii watakusumbua sana na unaweza kuiona biashara ni chungu.

Ili kuweza kufanya biashara na wateja wa aina hii waeleweshe kwamba bidhaa au huduma hiyo ni muhimu kwao na punguzo kubwa la bei wanalotaka haliwezekani. Kama wataendelea kusisitiza upunguze zaidi bei ni bora usifanye nao biashara maana watakusumbua sana na ushindwe kuwahudumua vizuri wateja wengine.

Anza kuwapanga wateja wako katika makundi hayo matatu na wapatie huduma ambayo itawafanya wafurahie kuendelea kufanya biashara na wewe.

Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.

TUPO PAMOJA.