Baada ya kumaliza mfano ule wa maksai na farasi, Mathon alimuuliza Rodan amejifunza nini kwenye mfano ule? Rodan alijibu ni hadithi nzuri ila hajajifunza chochote. Mathon alimwambia somo la kujifunza hapo ni rahisi sana; kama unataka kumsaidia rafiki yako msaidie kwa njia ambayo haitaleta matatizo yake kwako.

Mathon alimwambia kabla hajamkopesha mtu fedha ni lazima ajiridhishe kwamba mtu huyo anaweza kurudisha fedha anazokopa. Mathon aliendelea kumwambia Rodan kwamba ana mfuko ambao huwa anaweka token kila mtu anapokopa fedha. Hivyo watu ambao hawajamlipa bado token zao zinakuwa kwenye mfuko. Pia alimwambia kwa uzoefu wake watu wanaorudisha fedha walizokopa ni wale ambao wameweka dhamana kubwa kuliko fedha walizokopa. Alimwambia kuna makundi matatu ya wakopaji, kundi la kwanza wanaweka mali zao na wanalipa vizuri, kundi la pili ni wafanyakazi wenye kipato nao pia wanalipa vizuri. Kundi ya tatu ni la watu ambao hawana mali na wala hawana kazi, hao ni wasumbufu kulipa mkopo.

Mathon aliendelea kutoa mifano ya watu ambao aliwakopesha fedha na hawakulipa na pia alitoa mifano ya watu aliowakopesha fedha na kulipa bila matatizo. Alimwambia Rodan kwamba alichojifunza ni kwamba watu wanaokopa kwa ajili ya kwenda kuzalisha fedha zaidi wanarudisha mikopo yao. Ila wanaokopa kwa ajili ya matumizi wanapata shida sana kwenye kurudisha mikopo yao.

Alitoa mfano wa mama mmoja aliekuja kukopa fedha ili ampe kijana wake akafanye biashara. Mathon alisema aliona hatari ya kijana huyo kupata hasara kwa sababu hakuwa na uzoefu ila mwanamke yule hakutaka kusikiliza ushauri wake na aliweka madini ambayo yalikuwa na thamani ya fedha anayokopa. Mathon alimpa fedha zile na kijana yule aliingia kwenye biashara ambapo siku chache baadae alitapeliwa fedha zake zote. Alimwambia Rodan kwa sasa haoni dalili za kulipwa fedha zake siku za karibuni.

Rodan aliendelea kusema vijana wana matamanio makubwa. Vijana wanapenda kutafuta njia za mkato za kupata utajiri. Na ili kupata utajiri haraka, vijana hukopa fedha bila ya kuwa na mipango mizuri. Vijana ambao hawana uzoefu hawajui ni jinsi gani madeni yanaweza kuwa kikwazo kikubwa kwao kufikia mafanikio. Mathon aliendelea kusema, hawaambii watu wasikope maana hata yeye mwenyewe amefanikiwa kwenye biashara kutokana na mikopo ila anawashauru watu kuchukua mikopo ambayo wameipangilia vizuri na wametumia busara kubwa kwenye uhitaji wa mikopo hiyo.

Rodan alimwambia umeniambia vitu vingi sana vizuri ila bado hujanijibu swali langu. je nimkopeshe shemeji yangu fedha zangu? Mathon alisema kama shemeji yake yeye angemfata na kumwomba amkopeshe fedha angemuuliza fedha hizo anakopa ni za nini? Kama atamwambia anataka kwenda kufanya biashara angemuuliza maswali yafuatayo; je una uzoefu au ujuzi na biashara hiyo? Je unajua unapoweza kununua kwa bei ndogo? Na je unajua unakoweza kuuza kwa bei nzuri? Kama atajibu hapana kwenye maswali hayo basi hafai kupewa mkopo kwa sababu wafanya biashara wanahitaji uzoefu ndio waweze kufanikiwa kwenye biashara.

Mathon aliendelea kumwabia Rodan kwamba ukikopesha watu fedha bila ya kuwa makini unaweza kupoteza fedha nyingi sana. Alisema hata kama mtu anahitaji msaada kiasi gani ni lazima uangalie jinsi ya kumsaidia bila ya wewe mwenyewe kuingia kwenye matatizo kama ilivyotokea kwa maksai na farasi. Kwa mfano ukamkopesha shemeji yako fedha zako halafu wakati anaenda kwenye biashara akaibiwa na hana njia nyingine yoyote ya kukulipa si tayari na wewe umeingia kwenye matatizo?

Mathon alimwambia Rodan awe makini na fedha zake na aziweke mahali ambapo ana uhakika zitazalisha hata kama ni kidogo sana. Alimwambia kwamba amempa siri na busara nyingi sana kuhusu kukopesha fedha. Amemwambia udhaifu wa watu katika kukopa fedha ambazo hawawezi kuzilipa. Na alimwambia kama atatumia hayo aliyomwambia yatamnufaisha kwa kiwango kikubwa sana. Ila kama atafanya bila ya busara atapata hasara kubwa na ataishi maisha ya kujutia kila siku.

Tushirikishe mambo matano uliyojifunza kwenye uchambuzi huu kwenye maoni hapo chini.

Nakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa.

TUPO PAMOJA.