Debasir aliendelea kuelezea hadithi yake ya jinsi alivyonunuliwa kama mtumwa baada ya kukimbia madeni nyumbani.

Aliendelea kusema kwamba mke wa yule aliyemnunua kama mtumwa alimwambia kama yeye sio mtumwa aoneshe kweli kwamba yeye sio mtumwa. Alimwambia awe tayari kurudi kulipa watu wote wanamdai ili aweze kuishi kwa uhuru. Kwa mwaka mzima Debasir alikuwa anaishi kama mtumwa ila hakukubali hali ile. Hakuweza kabisa kukaa na watumwa wengine kwa sababu alihofia kufanya hivyo kungemfanya na yeye awe na fikra kama za watumwa na hivyo kuwa mtumwa wa kweli.

Siku moja Sira, yule mke wa bwana aliyemnunua Debasir kama mtumwa alimwambia Debasir kwamba mama yake anaumwa na hivyo aandae Ngamia wawili kwa ajili ya kwenda kumtembelea mama yake. Aliandaa ngamia hao na safari ya kwenda kwa mama yake ilianza. Walipofika nyumbani kwa mama yake, Sira aliwaambia wale watumwa wengine waondoke na kumwambia Debasir je una roho ya mtu huru au roho ya mtumwa? Debasir alijibu ana roho ya mtu huru. Akamwambia aoneshe kama kweli ana roho hiyo ya mtu huru. Alimwambia achukue Ngamia wale na atoroke na yeye atamwambia mume wake kwamba alitoroka na ngamia bila ya yeye kujua.

Debasir alimshukuru sana na akaanza safari yake ya kuondoka. Japokuwa hakuwa anajua njia vizuri, usiku kucha alisafiri, alipanda ngamia mmoja na mwingine alimswaga. Aliendelea na safari siku iliyofuata na mchana alifika kwenye jangwa ambapo hakukuwa na mtu wala mnyama yeyote. Na jangwa lile lilikuwa na mawe ambayo yaliumiza miguu ya ngamia wale na hivyo kushindwa kutembea kwa mwendo wa kasi. Aliendelea na safari kila siku, huku maji na chakula kikimuishia na jua lilikuwa kali sana na hivyo kuchoka sana. Siku ya tisa alikuwa amechoka sana na alikata tamaa na kuona hapo ndio ulikuwa mwisho wa maisha yake maana angekufa. Alilala chini usiku kucha na ilipofika asubuhi aliamka, aliona ni siku nzuri na ngamia wake walikuwa wamelala pembeni yake. Hakuona dalili yoyote ya maji au kitu cha kula. Alianza kufikiria kwamba siku hii nzuri anayoiona huenda ndio siku yake ya mwisho ya maisha. Akili yake ilikuwa inafikiria vizuri sana na alijiona ni wa muhimu tena. Akiwa pale alijiuluza tena swali aliloulizwa na sira, je mimi ni mtu huru au mtumwa? Alifikiria kama mimi ni mtumwa basi nilale hapa mpaka nitakapokufa na kama mimi ni mtu huru basi niendelee kupambana mpaka nitakapofika babeli, nikalipe madeni ya watu na nimfurahishe mke wangu.

Baada ya kufikiria hivi anasema dunia yake yote ilibadilika. Alijiona ni kama mtu aliyekuwa anaiangalia dunia kupitia kioo cha rangi na sasa kioo kile kimeondolewa na hivyo anaiona kwa uhalisia. Alianza kuona tena thamani ya maisha yake. Alidhamiria kurudi babeli na alisema akifika atawafata watu wote wanaomdai na kuwaambia kwamba atawalipa. Alisema madeni yake ni adui yake ila watu waliomkopesha ni marafikizake maana walimwamnini na kumpa fedha. Kwa kufikiria hivi alipata nguvu ya ajabu ambayo ilimwezesha kuendelea na safari. Hakuwa na chakula, hakuwa na maji ila alipata msukumo mkubwa sana wa kwenda kupambana na adui yake ambaye ni madeni na kurudisha urafiki na wale waliomkopesha fedha.

Anasema baada ya kuanza tena safari alikutana na maji, alipita nchi yenye ardhi yenye rutuba, akapata matunda na baadae akaipata njia ya kurudi babeli. Alisema akili ya mtu huru huangalia maisha kama mfululizo wa matatizo yanayotakiwa kutatuliwa, na kuyatatua ila akili ya mtumwa huishia kulalamika, naweza kufanya nini wakati mimi ni mtumwa?

Debasir alimuuliza Arkad, ambaye alikuwa anampa hadithi ile, vipi kuhusu wewe? Je njaa uliyonayo inakufanya uweze kufikiria vizuri? Je upo tayari kuchukua njia ambayo itakurudishia heshima yako? Je unaweza kuiona dunia kwa rangi yake halisi? Je upo tayari kulipa madeni yako na kuwa mtu huru na unayeheshimika? Arkad alimjibu, umenionesha maono mapya, naona roho ya mtu huru ikinijia.

Mtu mmoja aliyekuwa anasikiliza alimuuliza swali Debasir, nini kilitokea baada ya kurudi? Debasir alimjibu, penye nia pana njia. Kwa kuwa nilikuwa na nia nilitafuta njia, nilimfata kila anayenidai na kumwomba anivumilie mpaka pale nitakapoanza kupata kipato na nitalipa deni lote. Anasema wengi walimpokea vizuri na walikubaliana nae. Wengine walimpokea kwa hasira. Katika watu wale waliokuwa wanamdai mmoja alimsaidia sana, alikuwa mkopesha fedha. Baada ya kujua kwamba Debasir alikuwa anahudumia Ngamia kule utumwani alimuunganisha na mfanya biashara wa ngamia pale babeli na alitumia ujuzi wake wa ngamia na kuweza kufanya biashara nzuri na hatimaye kulipa kila deni alilokuwa anadaiwa. Anasema baada ya kulipa madeni yale alikuwa mtu wa kuheshimika na aliweza kurudiana na mke wake na hata wazazi wake walikuwa na furaha.

Tunajifunza nini hapa?

Kupitia hadithi hii ya Debasir kuna mambo mengi sana ya kujifunza ambayo yanatokea kwenye maisha yetu ya kila siku. Moja kubwa sana ni utumwa wa madeni ambao watu wengi wanao na hivyo kuishi maisha ya woga na wasiyoyafurahia na hata kukosa heshima kwenye jamii.

Pili ni tofauti kati ya mtu mwenye roho ya mtu huru na mtu mwenye roho ya mtumwa. Mtu huru anachukulia maisha kama mlolongo wa matatizo yanayotakiwa kutatuliwa na anayatatua, mtumwa anafikiria matatizo hayo na kulalamika kwamba yeye hawezi kufanya chochote. Hivi ndivyo tulivyo na watumwa wengi kwenye jamii zetu, ambao wanaendeshwa tu na maisha bila ya kujua wafanye nini.

Tatu, penye nia pana njia. Na ukiwa na nia ya kweli huwezi kukatishwa tamaa na kitu chochote.

Tushirikishe mambo mengine matano uliyojifunza kwenye sehemu hii ya uchambuzi hasa kwa hadithi hii ya Debasir. Kama nilivyosema yapo mengi ya kujifuza, tushirikishane mambo matano ambayo kila mtu amejifunza kwenye hadithi hii. Soma makala hii na iliyopita ili kupata picha nzima ya hadithi yote.

Nakutakia kila la kheri kwenye safari ya kufikia mafanikio makubwa na uhuru wa kifedha.

TUPO PAMOJA.