Katika kujijengea tabia za mafanikio mwezi huu wa kumi na mbili tunajadili jinsi ya kuachana na tabia ya kuahirisha mambo. Tabia ya kuahirisha mambo ni tabia ambayo imeathiri watu wengi sana na kuwafanya washindwe kufikia malengo yao.

Wiki iliyopita tuliona maana ya tabia ya kuahirisha mambo na kwa nini watu wanajikuta wakifanya tabia hii. Leo tutajadili hasara za tabia hii ya kuahirisha mambo. Tutaangalia ni jinsi gani tabia hii ya kuahirisha mambo ilivyo na madhara kwako.

Ni rahisi sana kupanga mambo ambayo unataka kufanya na unajua ili uweze kufikia mafanikio unahitaji kufanya mambo hayo. Lakini mambo unayopanga kufanya sio rahisi kiyafanya kama ilivyo kuyapanga. Ni katika hali hii ya ugumu wa kufanya mambo inapokuwa rahisi zaidi kusema nitafanya kesho kuliko kuendelea na jukumu ambalo ungetakiwa kulimaliza leo. Nitafanya kesho limekuwa kaburi la ndoto nyingi sana na kimekuwa chanzo kikubwa cha watu wengi kushindwa kufikia mafanikio.

Zifuatazo ni hasara za tabia ya kuahirisha mambo;

1. Unashindwa kufikia malengo na mipango yako.

Kwa kuwa na tabia ya kuahiridha mambo unashindwa kutekeleza malengo na mipango yako. Hii ni kwa sababu kuna ugumu ili kuweza kufikia malengo yako na hivyo unapoendekeza tabia ya kuahirisha mambo utashangaa muda unakwenda ila huna dalili zozote za kufikia malengo yako.

2. Inakuondolea kujiamini.

Pale ambapo unakuwa mtu wa kuahirisha mambo hata kujiamini kwako kunapungua. Hii inatokana na kwamba hujawahi kupanga kufanya kitu na ukaweza kukifanya kweli katika muda ambao umejipangia. Unajiamini pale ambapo unajua sehemu kubwa ya maisha yako unaisimamia wewe, unajua wewe ndio unayaongoza maisha yako. Ila pale unapokuwa na tabia ya kuahirisha mambo, maisha yako yanakuwa kama yanaendeshwa na matukio. Maana ukisema sasa natska kufanya jambo fulani, linatokea tukio ambalo ni rahisi kufanya na hivyo kuahirisha mpango wako mzuri.

3. Inakuletea msongo wa mawazo.

Tabia ya kuahirisha mambo ni moja ya vitu vinavyowajengea watu msongo wa mawazo. Kwa kawaida watu hawapendi kutekeleza majukumu yao mpaka pale wanapoona muda unakaribia kuisha. Kwa mfano mfanyakazi ana majukumu ya kuandaa ripoti ila kila mara anahirisha, inapofikia siku kwamba ripoti hizo zinahitajika anajikuta anafanya kazi usiku na mchana huku akiwa amepaniki. Yote haya aliyatengeneza mwenyewe kwa kuendekeza tabia ya kuahirisha mambo.

4. Unakosa watu wa kushirikiana nao.

Ni vigumu sana kupata mtu wa kushirikiana nae kama una tabia ya  kuahirisha mambo. Hakuna mtu anayeweza kuvumilia kila siku mambo yakiahirishwa bila hata ya sababu za msingi. Unahitaji sana ushirikiano wa watu wengine ili uweze kufikia mafanikio. Na ushirikiano wa watu unaohitaji ni wale ambao wamekutangulia kidogo, sasa watu hawa wako makini sana namuda wao. Wewe unapokuwa mtu wa kuahirisha mambo huwezi kuendana na watu hawa.

5. Unakosa fursa kubwa.

Fursa zipo nyingi sana na zipo kila mahali, ila fursa hizi zinaonekana na wale waliojiandaa kuziona fursa. Kama wewe hujajiandaa huwezi kuziona fursa, utaishia kuona wengine wakifanya huku wewe kutokujua ni kipi ufanye. Hii inasababishwa na tabia ya kuahirisha mambo na hivyo hata kufanya mambo ya msingi kama kujiandaa na fursa unaona huwezi kwa muda unaotaka kufanya hivyo.

Njia nyingine ambapo tabia ya kuahirisha mambo inakunyima fursa ni pale unapochelewa kuchukua hatua. Unaweza kuiona fursa nzuri ila kutokana na tabia ya kuahirisha mambo ukachelewa kuchukua hatua. Wakati wewe unaendelea kuahirisha mambo wanatokea wengine wanaikamata fursa hiyo na wewe unabaki ukishangaa tu.

Tabia ya kuahirisha mambo imekuwa ni kaburi la ndoto nyingi kubwa. Fursa nyingi zimepitwa kutokana na tabia ya kuahirisha mambo.

Wiki ijayo tutajadili jinsi ya kuondokana na tabia hii ya kuahirisha mambo.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kufikia mafanikio makubwa.

TUPO PAMOJA.