Kufikia ubora wa hali ya juu kabisa kwenye jambo lolote unalofanya(world class) ni kitu ambacho kila mtu anakipenda. Pamoja na kupendwa na kila mtu na bado ni watu wachache sana ambao wanaweza kufikia ubora huo wa hali ya juu. Sio kwamba watu hao wanaoweza kufikia ubora huo ndio pekee ambao wanajaribu kufanya, wanafanya wengi ila wengi wanaishia njiani.

Kufikia ubora wa hali ya juu sana sio kitu rahisi kama kusema hivyo. Lakini pia sio kitu ambacho kinashindikana. Kwa wewe kuwepo tu hapa kwenye KISIMA CHA MAARIFA tayari upo tofauti na watu wengine wanaofikiria kufikia ubora wa hali ya juu. Wewe umeshapiga hatua zaidi na hivyo njia yako inaweza kuwa rahisi zaidi ukilinganisha na njia za wengine.

Leo tutajadili maadui kumi wa ubora wa hali ya juu. Hivi ni vitu ambavyo vinawakwamisha watu ambao wamejitoa kwa ajili ya kufikia ubora wa hali ya juu. Watu wengi hawajui maadui hawa kwa sababu ni vitu ambavyo tunaishi navyo kila siku. Kwa kuwa wewe uko mbele ya wengine, utawajua maaduia hawa na utaanza kuwaepuka mara moja ili kuweza kufikia mafanikio makubwa kwa uhakika zaidi.

Yafuatayo ni mambo kumi ambayo yanawazuia watu wengi kufikia ubora wa hali ya juu.

1. Kutafuta njia rahisi ya kufanya mambo.

Katika kufikia uboa kuna wakati utapitia mambo magumu sana. Ukikimbia mambo hayo magumu na kutafuta njia rahisi kamwe hutofikia ubora. Ni katika nyakati hizi ngumu ambapo unajifunza somo bora sana kuhusu kufikia mafanikio makubwa. Hivyo unapoona mambo ni magumu furahia maana hapo unajifunza somo muhimu.

2. Kujilinganisha na wengine.

Ukishaanza kujilinganisha na wengine sahahu kuhusu ubora wa hali ya juu au mafanikio makubwa. Hakuna mtu mwenye ndoto kama zako na hakuna mtu mwenye mawazo kama yako au hata uwezo mkubwa ulioko ndani yako. Unapoanza kujilinganisha na wengine mambo mawili yanaweza kutokea; moja kujikuta unakubali mafanikio kidogo kwa sababu wanaokuzunguka hawana mafanikio makubwa, pili, kujikuta unakata tamaa kwa kuona wanaokuzunguka wamefanikiwa sana kuliko wewe. Fuata malengo na mipango yako, usipoteze muda kujilinganisha na wengine.

3. Kuogopa kuhusu watu wengine watakufikiriaje.

Kama kuna maamuzi muhimu unataka kufanya kwenye maisha yako, na unajua maamuzi hayo ndio yatakuwezesha kufikia mafanikio makubwa, yafanye bila ya kujali watu wengine watakufikiriaje. Ukianza kujali watu wengine wanakufikiriaje utajikuta unashindwa kufanya maamuzi sahihi ili uonekane mwema au wa kawaida. Ubaya ni kwamba hakuna anayejali sana kuhusu wewe, ukifanikiwa watakusema na hata ukishindwa pia watakusema zaidi. Hivyo fanya kilicho bora kwako na sio kile ambacho unafikiria kitapendwa na wengi.

4. Kupuuza mawazo yako ya ndani.

Kuna mawazo fulani yapo ndani yetu ambayo yanaweza kutusaidia sana. Unaweza kuwa kuna jambo unataka kufanya lakini mawazo yako ya ndani yanasita sana na kuona sio maamuzi mazuri, mara nyingi mawazo haya yanakuwa sahihi. Kama kuna kitu mawazo yako ya ndani yanakikata sana jaribu kuyafuata, utajiokoa kwenye matatizo mengi. Ila pia kuwa muangalifu mawazo haya yasijekuwa kizuizi kwako kwa kuhofia kila kitu.

5. Kushikilia mambo, badala ya kusonga mbele.

Hakuna kitu kinachoweza kuwa adui mkubwa wa mafanikio kama kushikilia mambo badala ya kusonga mbele. Kwa mfano umeingia kwenye biashara na mtu na kisha mtu huyo akakutapeli, unaweza kuchagua kusahau kuhusu mtu huyo na kusonga mbele kwa kufanya mambo yako kwa juhudi na maarifa zaidi au unaweza kuchagua kuwa unamlaumu mtu huyo kila siku kwamba ndio chanzo cha wewe kushindwa kufanikiwa kwenye biashara. Kuendelea kumlaumu ni kuendelea kupoteza muda wako. Na pia kusonga mbele haimaanishi kutojali yaliyotokea, bali umejifunza na hutorudia tena makosa uliyofanya.

6. Kuishi kwenye wakati uliopita.

Maisha ni safari ambayo tunasafiri mara moja tu, hakuna siku utakayorudia maisha uliyoishi jana. Kuendelea kuishi kwenye wakati uliopita ni sawa na kujidhulumu maisha yako. Yaliyopita yamepita na sasa unayo leo na kesho. Haijalishi umekosea kiasi gani siku zilivyopita, leo ni siku mpya ambayo unaweza kuanza upya na ukafanya mambo makubwa. Acha kuendele akufikiria vitu ulivyopoteza na fikiria unawezaje kutumia muda ulionao sasa.

7. Kufanya jambo ambalo sio sahihi kwa sababu wengine wanafanya.

Kosa ni kosa hata kama kila mtu analifanya. Kweli ni kweli hata kama ni wewe mwenyewe unafanya. Kama kuna kitu ambacho unajua sio sahihi kufanya, usikifanye hata kama kila mtu anakifanya. Kufanya jambo kwa sababu kila mtu anafanya ni adui mkubwa sana wa mafanikio makubwa.

8. Kuruhusu matatizo madogo madogo kukukwamisha.

Njia ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa ina changamoto nyingi sana. Kama utajali sana kuhusu changamoto hizo au makosa madogo madogo unayofanya kwenye safari hii yakurudishe nyuma au kukukwamisha unajiondoa kwenye nafasi ya kufikia ubora wa hali ya juu. Kumbuka changamoto ndio zinatufanya tufikiri zaidi, hivyo badala ya kukwamishwa nazo, jifunze zaidi na zivuke changamoto hizo.

9. Kupenda mambo ambayo yatakupa raha ya muda mfupi.

Kutimiza malengo na mipango yako sio kitu ambacho kinatokea haraka na hivyo inaweza kukuchukua muda mrefu sana wa kuumia ili uweze kufikia mafanikio makubwa. Kama utakubali kufanya mambo ambayo yanakuletea furaha ya haraka moja kwa moja unajizuia kufikia ubora wa hali ya juu utakaokuletea mafanikio makubwa. Moja ya vitu watu wanavyofanya iliw apate furaha ya muda mfupi na hivyo kujiondoa kwenye nafasi ya kufanya mambo makubwa ni kuangalia tv, kutumia vilevi na hata kutembelea mitandao ya kijamii. Epuka mambo hayo maana ni adui mkubwa wa mafanikio.

10. Kutokuamini kwamba unaweza kufikia ubora wa hali ya juu sana.

Unaamini kwamba wewe unaweza kuwa mfanyabiashara mkubwa sana nchini na hata duniani? Unaamini wewe unaweza kuwa bilionea? Kama huamini hivyo wala usipoteze muda wako, nenda kawashe tv, angalia masaa matatu kila siku, kunywa pombe kila siku na tembelea mitandao ya kijamii utakavyo. Kama huamini kwamba unaweza kufikia viwango vya juu sana na kuweza kufikia mafanikio makubwa hakuna kitakachoweza kukusaidia kufikia huko. Kila kitu kinaanza na imani na unapoamini unaweza ndipo unapoanza kuitafuta njia.

Hao ndio maadui kumi wa kufikia ubora wa hali ya juu. Ni mambo ambayo watu wamezoea kuyafanya kila siku. Yaepuke ili uweze kufikia mafanikio makubwa na kuboresha maisha yako na ya wale wanaokuzunguka.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa.

TUPO PAMOJA.