Utajiri Wako Uko Sehemu Hii Moja Muhimu, Acha Kupoteza Muda Huko Uliko Sasa.

Kuna baadhi ya watu wakisikia neno utajiri ni kama tusi kubwa kwao. Nawaelewa sana kwa sababu wengo tumelelewa kwenye jamii ambazo zina unafiki mkubwa sana linapokuja swala la fedha na utajiri. Tumekuwa tukiaminishwa kupenda utajiri ni kama dhambi na hivyo tusiuzungumzie sana.
Lakini hiyo ilikuwa ni karne iliyopita, karne hii unahitaji kuchagua kuwa tajiri au kuwa masikini, na hakuna kati kati ya hapo. Nafikiri hili utakuwa unalielewa vizuri sana, hasa unavyoona maisha yanavyobadilika kila siku.

 
Nilipoandika kitabu KWA NINI MPAKA SASA WEWE SIO TAJIRI, mwaka 2013, kuna msomaji mmoja aliniandikia ujumbe mrefu akisikitishwa sana kwa nini nimezungumzia utajiri moja kwa moja. Kwa nini nisingezungumzia tu mtu kuwa na uhuru wa kifedha au kuwa mwema na utajiri ukafuata? Nilishangaa sana, lakini yote ni yale yale. Unaweza ukaita beleshi ni beleshi au ukaamua kuita beleshi ni kijiko kikubwa. Vyovyote unavyoamua kuita, haibadilishi maana.
Hivyo basi iwe tunataka kuwa wema, iwe tunataka kutoa huduma bora kwa wengine, iwe tunataka kuwa na uhuru wa kifedha, lakini wote tunapenda kuwa matajiri. Sijawahi kukutana na mtu ambaye anasema mimi sitaki utajiri. Japo maana zetu za utajiri zinatofautiana. Mwingine atapima utajiri kwa fedha tu, mwingine atapima kwa maisha yake na ya wanaomzunguka na vipimo vingine vingi.
Kwa hiyo mpaka sasa tunakubaliana kwamba unataka kuwa tajiri. Na hata kama kwa sasa ni tajiri bado unataka utajiri zaidi. Si ndio? Kwa sababu maisha yalivyo ni iwe unaenda mbele au unarudi nyuma, hakuna katikati. Hivyo kama huwi tajiri kadiri siku zinavyokwenda maana yake unakuwa masikini. Ni hivyo tu.
Sasa umekubali kwamba unataka kuwa tajiri. Lakini je unajua utajiri wako uko wapi? Unajua utajiri wako unaanzia wapi? Hapa ndipo changamoto kubwa ilipo, kwa sababu wengi hatujui utajiri wetu hasa upo wapi au unaanzia wapi.
Aliyepo kwenye kazi anafikiri labda akipandishwa cheo atakuwa tajiri, akipandishwa cheo na bado haoni utajiri anafikiri labda akiingia kwenye biashara ndio atakuwa tajiri. Anaingia kwenye biashara fulani anakutana na changamoto na hivyo kukosa utajiri anafikiri labda akibadili biashara ndio atakuwa tajiri. Anafanya hivyo lakini bado anakosa utajiri. Na mwishowe, kwa sababu yeye anakazana na hapati utajiri anashawishika labda wale ambao ni matajiri wametumia nguvu za tofauti kuupata, labda na yeye anazitafuta nguvu hizi lakini bado haupati utajiri. Mwisho kabisa anakuja na jibu la uhakika, UTAJIRI NI BAHATI. Na mchezo unaishia hapo.
Je umewahi kuona watu wanapitia hali hiyo? Je wewe mwenyewe umewahi kupitia hali za aina hii. Kama ndio basi hiko ndio kielelezo tosha kwamba watu hawajui utajiri wao hasa uko wapi au unaanzia wapi.
SOMA; FEDHA: Kama Unataka Kuwa Tajiri, Acha Kufanya Makosa Haya Unapokuwa Na Pesa.
Ukitaka kujua na kuona wazi kwamba watu hawajui utajiri wao unapatikana wapi, angalia njia hizi watu wanazotumia kufikiri watapata utajiri.
1. Watu wanacheza kamari.
Kuna mtu anaamini kwamba anaweza kubashiri matokeo ya mchezo na akapata utajiri mkubwa. Kila la kheri kama na wewe ni mmoja wao, kwa sababu utapoteza muda mwingi sana.
2. Watu wanaorithi mali.
Angalia watu wengi wanaopigana kurithi mali za ndugu zao au wazazi wao, ni kitu gani huwa kinatokea baada ya mali hizo kuwa kwenye mikono yao? Sina haja ya kukueleza zaidi, tafuta mifano ya wale unaowajua au waliokuzunguka.
3. Watu wanaoiba, kufisadi au kutapeli.
Nafikiri unajua njia yao huwa inaishia wapi. Ndio wanaweza kuonekana wanatajirika haraka kwa zile mali wanazoiba au kutapeli wengine, lakini baada ya muda mambo yote yanakuwa wazi na wanapoteza kila kitu.
Tofauti ya chanzo cha utajiri na njia ya kufikia utajiri.
Unajua kuna utajiri wenyewe, halafu kuna ile njia ya kufikia huo utajiri. Na hapa ndipo watu wengi wanaposhindwa kuelewa na ndio maana wanapoteza muda mwingi na wasipate vyote.
Watu wengi wamekuwa wakifikiri njia ya kufikia utajiri ndio utajiri wenyewe, na hivyo wanakazana sana, lakini mwisho wa siku hawafiki kule wanakotaka.
Zipi ni njia za kufikia utajiri?
Chochote kile ambacho unakifanya, cha kukuingizia kipato au cha kutoa mchango wako ndio njia ya utajiri kwako. Na njia hii haiwezi kuwa sawa kwa wote.
Kwa mfano kuna watu ambao wameajiriwa na wana maisha bora sana, na hapo hapo kwenye kazi hiyo hiyo na kipato hiko hiko wengine wana maisha mabovu sana.
Kuna watu ambao wanafanya biashara na wana mafanikio makubwa sana. Na hapo hapo kuna watu wanafanya biashara hiyo hiyo na kwa kiwango hiko hiko lakini wana maisha mabovu sana.
Umeshaanza kuona tofauti? Kwamba njia hii hii moja, kuna ambao wanafanikiwa na kuna ambao wanashindwa. Ndio maana nakuambia hii ni njia na sio utajiri wenyewe, kuna chanzo kikuu cha utajiri ambacho ukishakijua, basi njia yoyote unayochagua lazima itakufikisha kwenye utajiri unaotaka.
SOMA; Sababu Kumi Kwa Nini Ni Muhimu Sana Wewe Kuwa Tajiri.
Ni kipi chanzo kikuu cha utajiri?
Chanzo kikuu cha utajiri kila mmoja wetu anacho, kila mmoja wetu amepewa bure, huhitaji kuingia gharama ya ziada ili kukitumia. Kipo hapo na huenda hujawahi kukitumia. Na kama ukianza kukitumia, basi hakika utaona mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yako.
Chanzo kikuu cha utajiri ni akili yako mwenyewe. Ndio utajiri wako unaanzia na upo kwenye akili yako, hayo mengine yote unayofanya ni njia tu ya kufikia utajiri. Ndio maana kwenye njia moja kuna ambao wanafanikiwa na ambao wanashindwa. Tofauti ya watu hawa wawili ipo kwenye akili zao tu, na sio pengine popote.
Akili yako ndio inayoweza kukufikisha wewe kwenye utajiri unaotaka, akili yako ndiyo inayoweza kukuletea wewe mafanikio makubwa. Na kwa kusisitiza ni kwamba uko hapo ulipo sasa, na hivyo ulivyo kutokana na kile kinachoingia na kutoka kwenye akili yako.
Lakini sio akili hii uliyonayo sasa.
Ndio akili yako ndio chanzo kikuu cha utajiri wako, lakini kuna angalizo hapo, sio akili hiyo uliyonayo sasa. Akili uliyonayo sasa imekufikisha hapo ulipo, na ukiendelea nayo itazidi kukupoteza.
Hivyo unahitaji kufanya mapinduzi makubwa kwenye akili yako. unahitaji kuanza kuitengeneza akili yako kuelekea kwenye yale mafanikio unayoyataka. Na hili linawezekana kama kweli umeamua.
Unawezaje kutengeneza akili yako kukupeleka kwenye utajiri?
Kuna njia 25 za kuitengeneza akili yako kuelekea kwenye utajiri, na njia hizi zimejadiliwa vizuri kwenye kitabu KWA NINI MPAKA SASA WEWE SIO TAJIRI. Kitabu hiki kipo kwa mfumo wa pdf, kinatumwa kwa email na unaweza kukisomea kwenye simu au kompyuta. Na kinauzwa kwa tsh elfu tano(5,000/=). Kukipata kitabu hiki tuma fedha tsh 5,000/= kwenye namba 0717 396 253 au 0755953 887 kisha tuma email yako kwenye moja ya namba hizo na utatumiwa kitabu mara moja.
Una haki ya kuwa tajiri na utajiri sio dhambi kama ambavyo ulikuwa unaaminishwa huko nyuma. Anza kutumia akili yako sawa sawa na chochote utakachogusa kitakupeleka kwenye utajiri mkubwa.
Nakutakia kila la kheri katika safari hii nzuri ya utajiri uliyoichagua, hutajutia kwa sababu utaendelea kufanya kwa ubora na kuwa na maisha bora.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
AMKA CONSULTANTS

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: