Moja ya changamoto zinazowakabili wajasiriamali wengi wa kitanzania ni huduma kwa wateja. Huduma kwa wateja ni eneo muhimu sana kwenye maendeleo ya biashara yoyote. Wajasiriamali wengi, wakubwa kwa wadogo wamekuwa wakiwekeza nguvu zao nyingi katika kutafuta wateja wapya kwenye biashara zao. Wamekuwa wanafanya hivyo kupitia matangazo mbalimbali. Wajasiriamali hawa wanasahau kwamba mteja bora kabisa ni yule ambaye tayari ameshafanya biashara na wewe. Kwa sababu kama mteja huyu atapata huduma nzuri, atarudi tena na tena na pia atawaambia watu wake wa karibu na hivyo kukuongezea wateja wengi zaidi.
Haijalishi unatumia gharama kiasi gani kutangaza na kuwavutia wateja wapya, kama unahuduma mbovu kwa wateja ni sawa na unapoteza fedha zako. Kwa sababu mteja atakaposikia bidhaa au huduma yako na kuamua kuja kuijaribu, kama atapata huduma mbovu hatorudi tena kwenye biashara yako. Hivyo pamoja na juhudi zako za kutafuta wateja wapya, hakikisha eneo lako la huduma kwa wateja lipo vizuri ili uendelee kuwabakiza wateja ulionao sasa. Kama waswahili wanavyosema; ndege mmoja uliyenaye mkononi ni bora kuliko ndege wawili waliopo msituni. Hivyo basi ni muhimu kwako wewe mjasiriamali kuhakikisha mteja uliyenaye sasa anaendelea kuwa mteja wako.
Kuna mambo mengi unayoweza kufanya ili kuhakikisha mteja uliyenaye sasa anaendelea kuwa mteja wako na hata kukuletea wateja wengi zaidi. Hapa tutajadili mambo machache muhimu ambayo unatakiwa uanze kuyafanya sasa, kama bado hujaanza kuyafanya ili uweze kuboresha huduma zako kwa wateja.
Kitu muhimu sana kwako kufanya ni kumjua mteja wako vizuri. Jua wateja wako ni wa aina gani na ni aina gani ya bidhaa au huduma wanazopendelea. Pia jua ni wakati gani bora kwao kufanya manunuzi na hii itakusaidia kuweza kuwapatia huduma nzuri. Katika kumjua mteja wako hakikisha unajenga naye uhusiano mzuri ili aweze kukuona wewe kama rafiki yake na mtu unayemjali. Hakuna mtu anapenda kuonekana kama anatumiwa kupata faida, hivyo uhusiano wako na wateja wako usiwe ni wewe kufaidika tu, bali na wao kupata suluhisho la matatizo yao.
Jambo linguine muhimu la kufanya ili kuboresha huduma kwa wateja ni kujiweka kwenye nafasi ya mteja. Vaa viatu vya mteja wako na jiulize kama wewe ndio ungekuwa unapewa huduma unayoitoa je ungeendelea kununua huduma hiyo katika hali inayotolewa? Kuwa mwaminifu kwako binafsi na sahau kuhusu wewe kuwa mmiliki wa biashara, hii itakusaidia kufanya yale ambayo yatamfaidisha mteja na hivyo kumridhisha na yeye kukuletea wateja wengi zaidi. Katika kuvaa viatu vya mteja wako, hakikisha juhudi zozote unazofanya kwenye biashara yako, iwe ni kuongeza uzalishaji au mauzo zinalenga kumsaidia mteja aliyepo na yule anayekuja.
Kupokea malalamiko ya wateja na kuyafanyia kazi ni njia nyingine muhimu ya kuweza kuboresha huduma za wateja. Kuna wakati ambapo mnaweza kukwaruzana na mteja, kutokana na sababu yoyote ambayo imeleta kutokuelewana. Inawezekana kosa likawa ni lako wewe au likawa ni la mteja, bila ya kujali kosa ni la nani chukua hatua ya kusikiliza malalamiko ya mteja na ahidi kuyafanyia kazi. Kama kosa ni la kwake unaweza kumwelewesha taratibu na akakuelewa. Usiingie kwenye ubishani na mteja, maana atakachokifanya yeye ni kuacha kufanya biashara na wewe na kutafuta sehemu nyingine atakayopatiwa huduma nzuri.
Jambo la mwisho tutakalojadili hapa kuhusu kuimarisha huduma kwa wateja ni kutoa promosheni na ofa mbalimbali. Unapotoa ofa kwa wateja wako unawahamasisha kununua zaidi na hivyo kuwa karibu na biashara zaidi. Endesha promosheni au toa ofa ambayo itamfanya mteja aone anapata thamani kubvwa zaidi kwenye biashara yako kuliko anayoipata sehemu nyingine anayoweza kupata bidhaa au huduma unayotoa. Sio lazima ofa hizi ziwe na gharama kubwa sana, kitu chochote kidogo kinachoonyesha kumjali mteja kinatosha kumfanya mteja aendelee kufanya biashara na wewe.
Huduma nzuri kwa wateja ni eneo muhimu sana kwenye biashara yako. Ni rahisi kufanya biashara na mteja uliyenaye sasa kuliko mteja ambaye unatumia nguvu nyingi kumtafuta. Mtumie mteja uliyenaye sasa kupata wateja wengi zaidi.
Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.
TUPO PAMOJA.